Sheria Leo. Kutokuwa na Imani na vyombo vya Upelelezi ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Kutokuwa na imani na vyombo vya upelelezi. Karibu tujifunze.

Imani katika Vyombo vya Upelelezi

Ndugu msomaji imani katika mfumo wa sheria ni jambo muhimu sana ili mfumo huo uweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayotarajiwa. Kama tulivyoeleza katika makala iliyopita juu ya mchakato wa kisheria una hatua mbali mbali na kuhusisha vyombo vingi.

Jamii yetu kwa sehemu kubwa haina imani na mchakato wa kisheria hasa kwenye suala la upelelezi. Hii inatokana na ukweli kuwa mara kwa mara sababu za kiupelelezi zimekuwa zikitolewa mahakamani na kusababisha mashauri kuchukua muda mrefu. Wananchi wanaofuatilia kesi na mashauri mbalimbali mahakamani wamekuwa wakijiuliza maswali mengi pasipo majibu kuhusiana na sababu hii ya ‘upelelezi haujakamilika’

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inatoa utaratibu mzuri zaidi kuhusiana na suala la upelelezi na kufikishwa kwa kesi mahakamani kwa mtuhumiwa. Upo muda wa ukomo ambao haupaswi kupita katika kukamilisha upelelezi wa shauri au shitaka. Kushindikana au kutokuzingatiwa kwa utaratibu wa kisheria kunaamsha wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusiana na hatma ya mashauri mahakamani na hasa muda.

Zipo nyakati upelelezi unachukua muda mrefu kiasi kwamba hata upatikanaji wa mashahidi na ushahidi juu ya tukio vinapotea au vinasahaulika.

Ni vyema kueleweka kwa wananchi kuwa upelelezi kuchelewa si suala la makusudi linalofanywa na taasisi husika bali kwa sehemu kubwa ni changamoto aidha za kimfumo au rasilimali. Changamoto hizo ni kama;

  • Uhaba wa watendaji wa kutosha katika ofisi za upelelezi kulinganisha na idadi ya matukio wanayopaswa kupeleleza
  • Uhaba wa vitendea kazi vya kutosha katika kutimiza majukumu ya upelelezi
  • Kasi ya sayansi na teknolojia katika uhalifu haviendani na kasi ya ujuzi kwa watendaji wa ofisi ya upelelezi, n.k

Kutokana na changamoto hizi watu wanashindwa kufahamu kuwa ucheleweshaji wa mashauri au umakini katika hatua za upelelezi kutofikia viwango husika mara kwa mara vinasababishwa na uhaba wa rasilimali.

Hatua za kuchukua

  • Serikali ina wajibu wa kuwekeza katika mafunzo madhubuti kwa wataalam wa ofisi ya upelelezi kuendana na kasi ya sayansi na teknolojia. Unaweza ukawa na watendaji wachache lakini wenye weledi wa kutosha kutimiza majukumu husika
  • Serikali kuruhusu mfumo huru wa kuwa na taasisi za upelelezi binafsi ambazo zinaweza kusaidia kukamilisha majukumu ndani ya muda mfupi kwa ufanisi mkubwa. Hii tumeona katika nchi zilizoendelea mbinu hii imesaidia si tu kupunguza uhalifu bali na kuvumbua njia mpya za kupambana na uhalifu. Kwa lugha ya kiingereza inaitwa ‘ Private Investigation’
  • Wananchi kutoa ushirikiano unaotakiwa kwa vyombo vinavyohusika na upelelezi endapo watatakiwa kufanya hivyo pasipo kudai maslahi yoyote. Hii imekuwa tabia kwa watu wengi ili washirikiane na Jeshi la Polisi kukomesha uhalifu wanahitaji walau wapate ‘chochote’ kutoa taarifa muhimu. Kwa jinsi hii tunalea uhalifu ambao madhara yake ni juu yetu.

Ndugu mwananchi ni muhimu kufahamu kazi hii ya kupeleleza uhalifu si kazi ndogo inahitaji muda wa kutosha, rasilimali watu na hasa zaidi vifaa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Tusivunjike moyo kutokana na mchakato kuchukua muda mrefu bali tuweze kutoa ushirikiano unaohitajika kupambana na uhalifu. Kazi hii haiwezi kufanywa na askari peke yao kwani wao ni wa kutafuta taarifa tu. Taarifa zote zinatoka miongoni mwetu kwani hakuna uhalifu unaofanyika kwa siri hata kama mwalifu ni mtu mmoja peke yake kuna namna mtu mwengine anaweza kupata taarifa kabla au baada ya uhalifu kutokea.

Pia ni rai yangu kwa vyombo vinavyohusika na upelelezi kuwa wananchi wangependa suluhu za uhalifu zipatikane mapema ili kurudisha imani ambayo kwa kiasi kikubwa imepungua ndio maana wanaamua kuchukua sheria mkononi. Watu wana wasiwasi na usiri wa taarifa wanazotoa ni vyema kuzingatia weledi na ulinzi wa vyanzo vya taarifa na kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia uhalifu. Utendaji na umakini ukionekana kwa wananchi ni dhahiri imani yao kwa vyombo husika itarudi na kutoa ushirikiano zaidi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema na mwanzo mwema wa 2018.

Wako

Isaack Zake, Wakili