Sheria Leo.Mtu au Jamii kujihami na Mkondo wa Sheria ni sababu ya watu Kujichukulia Sheria Mkononi
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu wa Sheria Leo kwenye mtandao wako wa Uliza Sheria. Kama kawaida yetu lengo la kukuletea makala hizi fupi ni kukusaidia kuishi kwa mujibu wa sheria kila siku.tumekuwa na mfululizo wa makala zinazohusu tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi. Leo tunakwenda kuangalia sababu mojawapo ya watu kujichukulia sheria mkononi ikiwa ni Wanajamii kuwa na Hofu ya kuhusika kwenye mkondo wa sheria. Karibu tujifunze.
Mtu au Jamii kujihami na mkondo wa sheria
Mtu au jamii kwa kujua kuwa endapo sheria itafuatwa basi hataonekana kuwa hana haki njia pekee ni kujichukulia sheria mkononi ili alazimishe haki ijapokuwa si yake au yao.
Yapo mazingira ambayo yanamsukuma mtu kujichukulia sheria mkononi kwa sababu anajua kuwa endapo suala husika litafuta mkondo wa sheria basi itabainika kuwa hana haki ile ambayo anadhani anayo. Hivyo njia pekee ni kutumia nguvu, ubabe na fujo dhidi ya mtu mwengine au taasisi ambaye anazo haki zote endapo sheria itafuata mkondo wake.
Mazingira ya namna hii unayaona sana katika migogoro ya ardhi baina ya jamii au mtu na jirani yake. Kila mmoja anaijua mipaka yake na inawezekana alama zimewekwa au maeneo yamepimwa na hati zimetolewa. Lakini utaona upande mmoja unaibua mgogoro na upande mwengine ambao hauna sababu zozote za msingi.
Aina ya migogoro ya namna hii ni ngumu sana kupata suluhu kwani mwalifu anatumia kila njia ili sheria isichukue mkondo wake ikiwezekana hata kutoa hongo ili apatiwe haki isiyo yake. Dhuluma, ushahidi wa uongo na hata mbinu za mauaji dhidi ya wapinzani wa mtu katika kuhakikisha anafanikiwa kupata anachotaka.
Ndio maana kwa mtazamo wangu naona migogoro mingi iliyo mahakamani haikupaswa kuwepo mahakamani kwa sababu si migogoro kwa hakika bali ni dhuluma.
Hatua za kuchukua
- Hakikisha masuala yako ambayo unafanya yapo kwa mujibu wa sheria ili kuepusha usumbufu usio wa lazima kutoka kwa watu ambao wanapenda kuanzisha migogoro pasipo sababu za msingi.
- Endapo wewe unakumbwa na hali hii jambo la msingi kufanya ni kuanza mara moja mchakato wa kisheria dhidi ya yule anayeanzisha mgogoro usio na sababu.
- Mchakato wa kisheria baada ya kumalizika na kupata usiishie hapo bali endelea kufuatilia na gharama za kukusumbua kutokana na mgogoro ulianzishwa na mtu huyo.
Huu ni mfululizo wa baadhi ya sababu ambazo tumezichambua kila moja inavyoweza kuchangia uwepo wa tabia ya watu na jamii kwa ujumla kujichukulia sheria mkononi. Kwa vyovyote vile na kwa hali yoyote jamii iliyostaarabika hufanya mambo kistaarabu haikabiliani na moto kwa moto bali hukaa chini na kutafakari chanzo cha tatizo na namna bora ya kutatua tatizo husika. Hatujawahi kuona wala hakuna ushahidi wa kutosha kuwa uhalifu unapungua kutokana na hatua kali wanazochukua jamii dhidi ya uhalifu au matendo maovu kupungua kutokana na hatua kali zinazochukuliwa na jamii. Tuwe na muda wa kutosha na kufungua mjadala mpana kwetu sote kama wadau kuona njia bora zaidi. Hatuwezi kujua kwa tabia hii ya kujichukulia sheria mkononi ni wangapi wasio na hatia wameangamia kwa kukosa subira, je, ni nani miongoni mwetu anaweza kufuatia kuwa muhanga wa tabia hii ambayo sisi tunaishiriki na kuishabikia kila kukicha.
Chukua tahadhari kabla ya kufanya maamuzi ya kijumla na kujichukulia sheria mkononi kwani yanaweza kukugarimu siku zijazo wakati wengine wakiwa kwenye nafasi ya kufanya maamuzi juu ya hatma yako na hapatakuwa na nafasi ya kujitetea.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema.
Wako
Isaack Zake, Wakili