34. Utatuzi wa Migogoro ya Kazi kwa njia ya Usuluhishi
Utangulizi
Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Tunaendelea kuchambua sheria hii yenye mahusiano ya mfanyakazi na mwajiri katika mfululizo wa makala. Katika makala iliyopita tuliangalia kwa utangulizi juu ya utatuzi wa migogoro ya kazi kwa kuzungumzia taratibu za usuluhishi, uamuzi na mahakama. Leo tunaanza kuchambua kila njia ya utatuzi wa mgogoro kwa kuanza na Usuluhishi ‘mediation’. Karibu tujifunze.
Usuluhishi
Hii ndio njia ya awali kabisa na msingi katika mfumo wa utatuzi wa migogoro ya kazi. Taasisi yenye mamlaka ya kufanya usuluhishi kwa mujibu wa sheria za kazi ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ‘The Commission for Mediation and Arbitration’ CMA. Kama tulivyoona kwenye makala za awali juu ya Taasisi za Kazi tulichambua muundo na majukumu ya Tume hii.
Maana ya usuluhishi ni mchakato wa utatuzi wa mgogoro ambapo mtu huru anawasaidia wadaawa yaani mwajiri na mfanyakazi kuzungumza na kufikia suluhu ya tatizo au mgogoro wao. Katika usuluhishi mtu huru hana mamlaka ya kulazimisha pande mbili zipatane bali atatumia uzoefu wake katika migogoro kuwashauri namna bora ya kumaliza mgogoro wao. Sheria za Ajira zimetoa fursa ya matumizi ya usuluhishi kama njia ya awali ya kutatua mgogoro kwa haraka kuliko njia nyingine.
Hatua za kufikia ngazi ya Usuluhishi
Zipo hatua ambazo anapaswa kuzingatia mwajiri au mfanyakazi zinazoongozwa na sheria za Ajira ili kumwezesha mgogoro wake kuwasilishwa Tume kwa ajili ya usuluhishi.
Sheria ya Ajira kwa kupitia kanuni zake imeandaa fomu maalum ambazo mwajiri au mfanyakazi au chama cha wafanyakazi wanatumia kwa ajili ya kuwasilisha mgogoro mbele ya Tume. Ufuatao ni mchakato wa kufungua mgogoro
- Kujaza fomu ya kufungua mgogoro mbele ya Tume
Sheria ya Ajira imeandaa fomu maalum za kufungua mgogoro inaitwa CMA Form No.1. Hii ni fomu maalum ambayo mwathiriwa wa mgogoro wa kiajira anapaswa kuijaza ndani ya siku 30 tangu mgogoro wa kazi kutokea. Wengi huwa wanapoteza muda wakijaribu kutafuta suluhu nje ya utaratibu wa kisheria. Ni muhimu sana kuzingatia suala la muda katika maswala ya kisheria. Mfano umeachishwa kazi na hujaridhika chukua hatua mapema ndani ya siku 30 wasilisha mgogoro wako Tume kwa kujaza fomu CMA No.1.
- Kuhakikisha nakala halisi ya fomu imetumwa kwa upande wa pili
Sheria ya Ajira inaelekeza kuwa nakala ya kufungua mgogoro lazima iwasilishwe kwa upande ule unaolalamikiwa na kupata udhibitisho kuwa nakala imemfikia muhusika. Hapa pamekuwa na changamoto sana hasa kwa waajiri kuwa wakaidi kupokea fomu za mgogoro. Sheria imeelekeza njia mbali mbali zinazoweza kutumika ikiwa kuwasilishwa kwa mkono, au kwa anuani ya Posta, barua pepe au kutumia wakala wa vifurushi. Endapo unapata changamoto ya kuwasilisha kwa njia za kawaida ni vizuri kutumia wakala wa kupeleka barua ili upatiwe risiti kama udhibitisho kuwa fomu imemfikia upande wa pili.
- Kuwasilisha fomu mbele ya Tume
Mara baada ya kuhakikisha kuwa upande ambao unalalamikiwa una taarifa juu ya hatua za kuwasilishwa mgogoro, upande unaofungua mgogoro utawasilisha Form CMA.No.1 mbele ya Tume ikiwa na udhibitisho kuwa upande unaolalamikiwa tayari wameshapewa nakala yao. Udhibitisho huo unaweza kuwa sahihi na muhuri wa mwajiri au mfanyakazi au chama cha wafanyakazi, au risiti kuonesha kuwa nakala ilipelekwa kwa huduma ya wapeleka barua.
- Kupata wito wa kuitwa mbele ya Tume kwa ajili ya Usuluhishi
Hatua inayofuata ni kazi ya Tume kufungua shauri na kutoa namba ya shauri na kisha kuandaa wito wa kuitwa shaurini kwa pande zote mbele ya Msuluhishi kwa muda na tarehe itakayoamuliwa na Tume. Ni kazi ya aliyefungua mgogoro kuhakikisha kuwa wito wa kuitwa shaurini unamfikia mlalamikiwa kama vile ilivyomfikia fomu ya kufungua mgogoro yaani CMA Form No.1.
Hitimisho
Kama tulivyoona leo hatua kadhaa za kufanya mgogoro wa kiajira kufunguliwa mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi. Wafanyakazi wengi na waajiri hawazingatii suala la muda wa kufungua shauri na wajibu wa kupokea wito au nakala ya mgogoro kufunguliwa. Wafanyakazi wanapoteza muda kwa kwenda ofisi ambazo hazihusiki kabisa na masuala ya utatuzi wa mgogoro wao, yapo mashauri mengi ya kazi unayakuta Polisi au ofisi za wakuu wa wilaya n.k huko sipo mahali pa kutatua mgogoro wa kazi bali ni mbele ya Tume. Pia zipo hadaa za waajiri kwa kuwapotezea wafanyakazi muda kwa kuwaambia maswala yao yanashughulikiwa wasubiri huku tayari wamewaachisha kazi. Mfanyakazi ukishaona kuwa umeachishwa kazi na ujaridhika na utaratibu husika basi chukua hatua mapema, tafuta ushauri kwa wanasheria ili kupata usaidizi wa mapema.
Usikose kufuatilia makala nyingine ya ufafanuzi juu ya usuluhishi kama njia ya kutatua mgogoro wa kazi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Muhimu
Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .
‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’
Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.
Wako
Isaack Zake, Wakili.