45. Dai la Kurudishwa Kazini

Utangulizi

Karibu tena ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi. Kwa sehemu kubwa tumeichambua sheria ya kazi katika maeneo mbalimbali na kueleza dhana kadhaa kuhusiana na ajira. Mfululizo huu unaoanza kwenye makala ya leo tutakuwa tukijibu hoja na maswali mbalimbali yanayohusiana na ajira ambayo tuliyapokea kwa njia ya simu, e-mail na kuwashauri wadau husika. Ili kutoa mwanga kwa jamii nzima tumeona tuyajadili maswali haya na kuyatolea ufafanuzi.

Lengo letu ni kusaidia kwa kadri inavyowezekana wadau wa sheria ya ajira yaani mwajiri na mfanyakazi kutimiza wajibu wao ili kupata haki zao. Karibu kwenye makala ya leo inayokwenda kujibu swali linalosema

Nini unaweza kudai endapo umeachishwa kazi isivyo kihalali?

Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

Kuachishwa kazi

Kwa kupitia makala zilizopita tumejadili hoja hii ya kuachishwa kazi isivyo kihalali au kuachishwa kazi kihalali. Kwa ufafanuzi zaidi rejea makala husika.

Maana rahisi ya kuachishwa kazi isivyo halali ni kuachishwa kazi pasipo sababu halali au za msingi au kuachishwa kazi pasipo kufuata taratibu halali za sheria ya kazi.

Wafanyakazi wengi huwa hawajishughulishi na kufahamu haki zao muda wawapo kazini, lakini kazi inapokoma ghafla ndipo hali ya kuchanganyikiwa inajitokeza na hata kukosa utulivu wa kutosha kujua ni haki zipi unaweza kuzipata. Pasipo utulivu wengi hukimbilia tu kufungua mgogoro Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pasipo kujua ni nini hasa wanadai na hivyo kujikuta wanadai kidogo kuliko wanavyostahili au wanadai vibaya na hivyo kukosa kabisa.

Leo tunakwenda kuangalia aina mojawapo ya dai ambalo mfanyakazi anaweza kuomba mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi yaani CMA.

Dai la Kurudishwa Kazini

Sheria ya ajira inatoa nafuu au kuruhusu mfanyakazi kuomba kurudishwa kazini. Kwa lugha ya kiingereza dai hili au nafuu hii inaitwa ‘Reinstatement’. Endapo itadhibitika kuwa mwajiri alimwachisha mfanyakazi pasipo kufuata taratibu husika basi Tume inaweza kumwamuru amrudishe kazini pasipo masharti yoyote.

Msingi wa dai hili ni kumrudisha mfanyakazi katika nafasi yake aliyokuwa awali katika kazi pasipo kuathiri chochote kile kuhusu kipato au maslahi yake.

Wafanyakazi wengi wanapokuwa wamefukuzwa au kuachishwa kazi wanahofu kuomba dai hili kwa msingi kuwa mwajiri atatafuta namna nyingine ya kuwaondoa kazini.

Faida za Dai la kurudishwa Kazini

  • Kumhakikishia mfanyakazi usalama wa kazi yake ‘job security’
  • Kumrudisha mfanyakazi kwenye nafasi yake aliyoipoteza isivyo halali
  • Mfanyakazi kulipwa mishahara yote aliyopaswa kulipwa tangu amesitishiwa ajira isivyo halali mpaka arudipo kazini
  • Endapo mwajiri hatokuwa radhi kumrudisha mfanyakazi kazini atalazimika kumlipa mishahara yote kipindi akiwa nje ya kazi pamoja na fidia ya mishahara isiyopungua miezi 12

Hasara za Dai la kurudishwa kazini

Kutekelezwa kwa dai hili kunaweza kuleta hasara kadhaa kwa mfanyakazi ambazo anapaswa kuzifahamu

  • Hali ya uhasama baina ya mfanyakazi na mwajiri inaweza kujitokeza
  • Mwajiri anaweza kutokubali kumrudisha mfanyakazi kazini
  • Mwajiri anaweza kutengeneza mazingira yatakayomlazimisha mfanyakazi kuacha kazi hapo baadae.

 

Hitimisho

Kama nilivyoeleza mwanzo wa makala hii kuwa ipo changamoto ya kutokujua ni kitu gani unapaswa kudai endapo umeachishwa kazi isivyo halali. Dai la kurudishwa kazini lina faida kubwa kwa mfanyakazi kama ikidhibitika mbele ya Tume kuwa aliachishwa isivyo halali. Ni vyema pia wakati wa kujaza fomu ya madai yaani CMA Form No.1 kupata usaidizi au ushauri wa kisheria ili usikose nafuu ambayo ina maslahi zaidi. Kumbuka kuwa Tume haiwezi kukupa kitu ambacho hukuomba kama dai au nafuu ya kisheria ni muhimu kujua unataka nini.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Muhimu

Ikiwa una maswali au kuna eneo la kisheria ungependa kupata ufafanuzi basi nafasi ni yako na ndio msingi wa mtandao huu wa Uliza Sheria. Wasiliana nami na kuuliza maswali mbalimbali ili tuyachambue kwenye makala zijazo kwa njia ya e mail zakejr@gmail.com namba ya simu watsup 0713 888 040 na kwa sms .

‘Usikwame kwenye tatizo lolote la kisheria wakati unayo nafasi ya kuuliza, uliza sheria uoneshwe njia’

Nakutakia siku njema sana ndugu yangu.

Wako

Isaack Zake, Wakili.