Biashara Sheria.13. Sifa za Mkataba Halali Kisheria – Nia ya kuwajibika kisheria

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa ukurasa wetu wa Biashara Sheria. Ukurasa huu umekuwa mahsusi kwa ajili ya uchambuzi wa mambo mbalilmbali yanayomwezesha mtu au kikundi kuwa na namna bora ya kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa mujibu wa sheria. Katika makala iliyopita tuliangalia kwa utagulizi juu ya sifa za mkataba kuwa halali ambapo tumeona ni lazima kuwepo na ‘Pendekezo na kukubaliwa kwa pendekezo’ yaani ‘Offer and Acceptance’. Leo tunaendelea  kujifunza juu ya sifa zinazosababisha mkataba kuwa halali kisheria. Karibu tujifunze.

Maana ya mkataba

Kama tulivyoona katika makala iliyopita tafsiri ya kawaida kabisa juu ya mkataba ni makubaliano baina ya pande mbili au zaidi.

sheria kuu ya Mikataba Sura ya 345 inaeleza zaidi kupitia kifungu cha 10 cha sheria kinachosema

Makubaliano yote ni mikataba kama yatakuwa yamefanywa kwa hiari na watu wanaostahili kufanya makubaliano, kwa malipo ya kitu halali na ambayo hayajatajwa waziwazi hapa kuwa ni batili: Isipokuwa kwamba maelezo yoyote yaliyomo hayatadhuru sheria yoyote inayotumika, na ambayo imefutwa ama kuacha kutumika, inayoelekeza mikataba yote inatakiwa iwe kwenye maandishi au ifanywe mbele ya mashahidi, au sheria yoyote ihusuyo usajili wa nyaraka.

Kupitia tafsiri hii ya kisheria, tunaweza kuona vipengele muhimu ambavyo vinafanya mikataba au makubaliano yawe na nguvu ya kisheria yaani kuwabana pande zote.

Katika makala ya leo tunaangalia kipengele muhimu sana ambacho kinapaswa kudhihirishwa katika mkataba nacho ni ‘Nia ya Kuwajibika Kisheria’

Maana ya Kuwajibika Kisheria

Kuwajibika kisheria ni kipengele muhimu sana cha kuwa na mkataba halali. Haitoshi tu kuwa na pendekezo ambalo limekubaliwa yaani ‘offer and acceptance’ bali ni muhimu zaidi kuwe na nia ya pande zote kuwajibika kisheria. Ili mkataba au makubaliano yoyote yawe na nguvu ya kisheria, ni lazima pande zote ziwe zimekusudia au zina nia ya kuwajibika au kufungwa kisheria. Katika makubaliano yoyote ambayo yana kusudiwa kuwa na nguvu ya kisheria, ni lazima pande zote zihakikishe kuwa wanajua na wanayo nia ya kuhusiana kisheria katika makubaliano hayo. Yaani makubaliano yao yalindwe au kutafsiriwa kisheria.

Nia ya kuwajibika au kufungwa kisheria ina maana kuwa endapo upande mmoja ukaenda kinyume au ukashindwa kutimiza masharti au makubaliano basi unapaswa kuadhibiwa kisheria.

Ni lazima ifahamike kwamba si kila makubalino yana nguvu ya kisheria au yana nia ya pande zote kuwajibika kisheria yapo makubaliano ya kijamii ambayo watu hufanya kila siku pasipo na nia ya kuwajibika au kufungwa kisheria.

Athari za kutoonesha nia ya uwajibikaji wa kisheria katika mkataba

Kama tulivyoona kuwa si kila makubaliano yanakuwa mkataba wenye nguvu ya kuzibana pande zote kisheria. Hivyo endapo mkataba hautaonesha nia ya pande zote kubanwa au kuwajibika kisheria basi makubaliano hayo yanakosa nguvu ya kisheria. Zipo athari za makubaliano kukosa nia ya uwajibikaji au kufungwa kisheria;-

  • Makubaliano yaliyokosa nia ya uwaibikaji wa kisheria hayawezi kuwa na nguvu ya kisheria au kumbana mtu pale anaposhindwa kutekeleza
  • Pande zote haziwezi kushtakiana mahakamani endapo upande wowote utashindwa kutimiza ahadi au makubaliano
  • Makubaliano yasiyo na uwajibikaji hubaki tu kuwa ahadi ambayo haina ulazima wa kuitimiza

Kwa kawaida huchukuliwa makubaliano ya kifamilia hayawezi kuwa mkataba mpaka pale itakapothibitishwa vinginevyo. Ikiwa baba anampa ahadi mtoto kisha akashidwa kuitekeleza, mtoto hawezi kuidai ahadi hiyo katika mahakama mpaka pale itakapothibitishwa kuwa kulikuwa na nia ya kisheria.

Katika kesi maarufu ya Bafour v Bafour, 1919, ambapo mume alimuhaidi mkewe kuwa atakuwa akimtumia kiasi cha pauni 30 kila mwezi za matunzo mpaka pale atakaporudi. Aliweza kwa muda kutimiza ahadi hiyo, lakini kwa kipindi fulani alishindwa. Mke akamshtaki mume kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake. Mahakama iliamua kuwa ahadi ya mume haikuwa na nia ya kuwajibika kisheria endapo angeshidwa kutimiza na hivyo kutupilia mbali madai ya mke kwamba ulikuwa mkataba.

Hitimisho

Ni muhimu sana katika masuala ya kibiashara ya kila siku kuhakikisha kuwa makubaliano unayoingia yana nia au msukumo wa kuwajibika kisheria ili kuepuka hasara zinazoweza kujitokeza kama kipengele hiki muhimu kitakosekana katika makubaliano husika.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com