Sheria Jinai.1. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Kijinai

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wetu na mfuatiliaji wa makala mbali mbali za mtandao wa uliza sheria. Kutokana na mahitaji ya wasomaji na maswali kadhaa ambayo tumekuwa tukiyapokea na kuyajibu mara kwa mara kumejitokeza uhitaji wa ufafanuzi hasa katika masuala ya makosa ya Kijinai. Watu wengi wamekuwa wakiguswa kwa namna moja ama nyingine na maswala ya kisheria yanayohusu makosa  ya kijinai, hivyo ufafanuzi na elimu ya kutosha kuhusiana na mwenendo wa makosa ya kijinai unahitajika sana.

Katika makala hii ya utangulizi tunaenda kujifunza kwa ufupi juu ya Sheria maalum inayoongoza mwenendo wa makosa ya Kijinai inayoitwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 ya sheria za Tanzania. Karibu tujifunze.

Changamoto za Mfumo wa Mwenendo wa Makosa ya Jinai

Moja ya maeneo yenye changamoto kubwa sana katika mfumo wa kisheria ni masuala ya makosa ya kijinai. kuna mashauri mengi sana mpaka sasa yapo mahakamani na yanachukua muda mrefu kufikia hatma yake. Wananchi wamekuwa na malalamiko mengi hususani mashauri ya kijinai kuchukua muda mrefu sana kuanzishwa na hata kukamilika kwake.

Mfumo wa mwenendo wa makosa ya kijinai unakabiliwa na changamoto kadhaa;

  • Muda; muda umekuwa kikwazo kikubwa sana kwa mashauri ya jinai kuchukua muda mrefu sana mahakamani. Kwa wastani shauri moja linaweza kuchukua angalau muda wa chini usiopungua miaka 2 hata 3. Mashauri mengi yanafika miaka 5 hata 10 bado yakiwa mahakamani. Hali ya kushindwa kumalizika mashauri ya kijinai mapema hukatisha tamaa wananchi na hata kwa sehemu huaribu ushahidi pale mashahidi wanapokosekana kwa sababu moja au nyingine.
  • Ufahamu wa sheria; watu wengi ambao wapo kwenye mchakato wa mashauri ya kijinai hawana ufahamu wa kutosha kuhusiana na namna sheria na mifumo yake inavyofanya kazi. Hii ni changamoto kubwa kwani hali ya kutokujua namna sheria hizi zinavyofanya kazi zinaweza kuchangia kwa sehemu kubwa ucheleweshwaji wa mashauri mahakamani au katika ngazi nyingine.
  • Rasilimali watu; ni dhahiri mfumo wa mwenendo wa mashauri ya kijinai unahusisha taasisi nyingi. Mfumo huu unahusisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na taasisi nyingine ambazo kwa shughuli zake ni lazima zihusike katika ukamilishaji wa michakato ya mashauri ya kijinai. Rasilimali watu wanaopaswa kufanya kazi katika kusaidia mfumo huu ni wachache kulinganisha na idadi ya mashauri yanayopaswa kushughulikiwa. Mathalani katika idara ya upelelezi watendaji ni wachache sana kulinganisha na idadi ya makosa yanayopaswa kuchunguzwa. Sababu ya upelelezi kutokamilia imekuwa ni sababu kubwa sana ya kucheleweshwa kwa mashauri ya jinai, tofauti sana na mfumo wa mashataka ya madai ambayo hayahusiani na masuala ya upelelezi.
  • Rasilimali vifaa; kulingana na maendeleo ya kisayansi na teknolojia, matukio ya kiuhalifu yamechukua sura mpya na yana mtandao mpana sana katika kuyatekeleza. Hali hii inapaswa kukabiliwa na zana za kisasa pamoja na weledi wa hali ya juu. Ufinyu wa rasilimali vifaa katika kukabiliana na wimbi kubwa la uhalifu unatatiza kwa kiwango kikubwa katika ukamilishaji wa mashauri ya kijinai ndani ya muda mfupi.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 imetungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1985 na kuendelea kufanyiwa marekebisho mara kwa mara.

Madhumuni makuu ya sheria hii ni kutoa utaratibu unaopaswa kufuatwa kwenye upelelezi wa makosa ya kijinai, uendeshaji wa mashtaka ya kijinai na mambo mengine yanayohusiana na makosa ya kijinai.

Katika mfululizo wa makala za uchambuzi wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, tunajifunza mambo mbali mbali ambayo kwa sehemu itasidia kwa wadau hasa wananchi kufahamu hatua wanazopaswa kuchukua ili mfumo huu wa sheria ufanye kazi kwa ufanisi na muda mfupi.

Lengo kuu la kuanzisha ukurasa huu ni kusaidia elimu ya msingi kwa wadau wa sheria hii, hususani wananchi ambao wanajikuta katika mchakato wa utendaji wa sheria hii.

Hivyo nakukaribisha sana ndugu yangu msomaji wa makala hizi tuendelee kujifunza na kuuliza maswali ili kupata ufafanuzi unaohitajika.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com