56. Kujiuzulu kwa Hila

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Mfululizo wa makala zilizopita ulielezea juu ya makosa mbalimbali ambayo yanaweza kupelekea usitishwaji wa ajira ya mfanyakazi. Leo tunaangalia juu ya ‘Kujiuzulu kwa Hila’ Karibu tujifunze.

Maana ya Kujiuzulu

Sheria ya Kazi na Ajira inatambua kuwa mfanyakazi anaweza kusitisha ajira yake kwa kitendo cha kujiuzulu. Kujiuzulu kazi ni kitendo cha hiyari kuacha kazi kwa mfanyakazi kutokana na sababu mbalimbali.

Kanuni za Utendaji Bora zinazotokana na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini zinaeleza wazi kuwa aina mojawapo ya usitishwaji wa ajira halali ni ule usistishwaji unaofanywa na mfanyakazi. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 3 (2) (d) ya Kanuni za Utendaji Bora.

Usitishwaji huu wa mfanyakazi unaweza kufanywa kwa njia ya kujiuzulu kwa kuandika barua au hata kwa mdomo. Pia mfanyakazi anaweza kusitisha ajira yake kwa kutoonekana kazini kwa muda mrefu pasipo kutoa taarifa kwa mwajiri wake.

Kujiuzulu kwa Hila

Kama inavyoonekana kuwa kujiuzulu kwa mfanyakazi ni aina mojawapo ya usitishwaji wa ajira unaotambulika kisheria. Hata hivyo mazingira ya kazi yanaweza kusababisha mfanyakazi kujikuta analazimika kujiuzulu kwa kushawishiwa na mwajiri wake. Huku ndiko kujiuzulu kwa hila.

Mathalani pametokea matatizo ya kiajira mahali pa kazi na mwajiri anakosa namna bora ya kushughulikia matatizo hayo na mfanyakazi wake, njia pekee anayoitumia ni kumshawishi mfanyakazi husika kujiuzulu.

Uzoefu unaonesha kuwa wafanyakazi wengi wanaojiuzulu nafasi zao za kazi si kwamba wametenda kwa hiyari yao, bali kuna mazingira na msukumo fulani ulitengenezwa na mwajiri ili mfanyakazi husika ajiuzulu na ionekane amejiuzulu mwenyewe kwa hiyari.

Zipo sababu kadhaa ambazo zinasababisha wafanyakazi wengi kuingia katika mtego wa kujiuzulu kwa ushawishi wa mwajiri. Hata hivyo katika makala hii tutaangazia sababu kadhaa.

  1. Hofu ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu

Katika shuguli za kila siku za mahusiano ya ajira kati ya mwajiri na mfanyakazi yapo mazingira ambayo ni lazima kuna kupishana kiutendaji au kwa kauli. Hali hii inapojitokeza ikiwa mwajiri hana mfumo mzuri wa kushughulikia tabia na mwenendo wa waajiriwa, hukumbilia kutishia kufukuza kazi au kuchukua hatua kali zitakazomnyima haki mfanyakazi. Mfanyakazi hupata hofu, ili kuepuka adhabu ambayo inaweza kuhatarisha maslahi yake ya kipato basi ajiuzulu.

  1. Hofu ya kuchukuliwa hatua za kijinai

Utendaji wa kazi mahali pa kazi pia unaweza kuhusisha matukio ambayo yana viashiria vya makosa ya kijinai. Waajiri wasio waaminifu hutumia mwanya huu kuwatisha wafanyakazi na hata kuwapeleka katika mchakato wa kijinai kwenye taasisi za Polisi au uchunguzi wowote. Ikifika hatua hii wafanyakazi wengi huingia hofu na kwa ushauri au ushawishi wa mwajiri, huamua kujiuzulu ili kuepuka mchakato wa kijinai wa maswala yanayohusishwa na kazi zao.

  1. Hofu ya kuchafuliwa CV na mwajiri

Panapojitokeza makosa ambayo mfanyakazi anahusika moja kwa moja au anahisiwa kuhusika, baadhi ya waajiri huwashawishi wajiuzulu ili wasiwachafulie sifa yao kwa mashirika mengine wanayoweza kwenda kuomba kazi. Wafanyakazi kwa kutokujua nafasi yao na haki zao wanakubali kuacha kazi kwa lengo la kulinda sifa yao kwa ajili ya mahali wanapotaka kwenda kufanya kazi.

 

  1. Hofu ya kukosa maslahi ya kipato

Wapo waajiri wanaowashawishi wafanyakazi kujiuzulu ili angalau waweze kupata kipato fulani. Hali hii inaweza kujitokeza pale ambapo mwajiri anataka kukwepa mchakato wa kupunguza wafanyakazi. Hivyo hutumia njia hii ya kushawishi wafanyakazi waache kazi wenyewe ili angalau awape kiasi kidogo cha kuanzia maisha. Wafanyakazi wengi wanaogopa kupinga kile wanachoelezwa na waajiri kwani wanaona wakikataa kujiuzulu basi itatafutwa sababu yoyote ya kuwaondosha kazini.

  1. Kutokujua haki za mfanyakazi

Hii ndiyo sababu kuu kabisa ambayo inapelekea wafanyakazi kuchukua hatua ya kujiuzulu kutokana na ushawishi wa mwajiri. Wafanyakazi wengi hawajishughulishi kutafuta maarifa yanayolinda haki zao za kiajira, wala kutafuta ushauri kwa wataalam wa sheria za kazi na ajira. Wafanyakazi wengi hutafuta ushauri kwa wenzao ambao wapo nao mahali pa kazi pasipo kujua hata hao wenzao hawana ufahamu au pengine wanatumiwa na mwajiri kuwarubuni waache kazi kwa kujiuzulu.

Hizi ni baadhi ya sababu ambazo zinapelekea wafanyazi kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kutokana na kushawishiwa na mwajiri au mawakala wa mwajiri pasipo kuwa na sababu za msingi au hiyari yao wenyewe.

Katika makala inayofuata tutaangalia kwa sehemu athari za maamuzi haya kwa mfanyakazi husika.

‘Mfanyakazi kabla ya kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kazi tafakari kwa makini iwapo uamuzi wako ni wa hiyari au la’

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com