57. Athari za Kujiuzulu kwa Hila

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeangalia juu ya Kujiuzulu kwa Hila ambapo waajiri wengu wamekuwa wakiwashawishi wafanyakazi kuchukua maamuzi hayo. Leo tunaangalia juu ya ‘Athari Kujiuzulu kwa Hila’ Karibu tujifunze.

Kujiuzulu kwa Hila

Katika makala iliyopita tumeweza kuona kuwa mfanyakazi anaweza kushawishiwa kujiuzulu kwa hila na mwajiri wake. Tumeona sababu kadhaa ambazo zinaweza kusababisha mfanyakazi kujiuzulu kwa hila ambazo kwa hakika ni hofu tu ya wafanyakazi inayosababisha kuchukua hatua hizo.

Zipo athari zinazoweza kujitokeza kwa mfanyakazi kuchukua hatua ya kujiuzulu kutokana na ushawishi wa mwajiri au washauri wengine wasio wataalam wa sheria za kazi. Katika makala hii tunaona baadhi ya athari hizo;

  1. Mfanyakazi kupoteza fursa ya utetezi katika mchakato wa kinidhamu

Mfanyakazi anapoamua kujiuzulu kutokana na kushawishiwa na mwajiri, inampotezea fursa ya utetezi ambao angeweza kuwa nao katika kikao cha kinidhamu. Wapo waajiri wanaowashawishi wafanyakazi kujiuzulu ili wasiandikiwe barua ya kuachishwa kazi. Wakati mwengine huu ni mtego ambao wafanyakazi pasipo kujua wanaingia na hatimaye kurahisisha zoezi la kuondoka kwao katika kazi. Maana itaonekana umeacha kazi mwenyewe pasipo shindikizo.

  1. Mfanyakazi kukosa dai la haki kisheria dhidi ya mwajiri

Endapo mfanyakazi ataamua kujiuzulu kwa hiyari yake iwe kwa kushawishiwa au pasipo kushawishiwa, anakosa sifa ya kisheria kudai haki zozote kwa mwajiri wake. Ili mfanyakazi aweze kuwa na haki ya madai dhidi ya mwajiri kuhusiana na haki za kiajira ni lazima pawe na mgogoro baina yake na mwajiri ndipo mgogoro husika uwasilishwe katika vyombo maalum vya utatuzi. Kujiuzulu kwa mfanyakazi kunamwondolea sifa ya kuweza kufungua madai endapo atakuwa amedhulumiwa haki zake za kiajira.

  1. Uwezekano wa mfanyakazi kuchukuliwa hatua za kijinai

Waajiri nyakati nyingine wanawaahidi wafanyakazi endapo watajiuzulu basi hawatawachukulia hatua za kijinai. hata hivyo nyakati nyingine ahadi hizi hazitimii, mara baada ya mfanyakazi kujiuzulu katika nafasi yake, waajiri wanatoa taarifa kwa vyombo vya uchunguzi wa kijinai huku wakitumia na barua ya kujiuzulu kwako mfanyakazi kama kigezo cha kutilia mashaka uadilifu wako.

 

  1. Uwezekano wa kuharibiwa kwa sifa ya mfanyakazi

Kama tulivyoona moja ya sababu ya wafanyakazi kujiuzulu ni kujaribu kulinda sifa yao ya kiajira ili wanapopata kazi sehemu nyingine waweze kukubaliwa. Lakini tumeshuhudia baadhi ya waajiri wakianika sifa mbaya kwa wafanyakazi wao hata waliojuzulu kwa kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusiana na tabia au sifa mbaya za mfanyakazi huyo. Hali hii bado kwa sehemu kubwa inachafua sifa ya wafanyakazi.

Hizi ni baadhi ya athari zinazojitokeza pale mfanyakazi anapochukua uamuzi wa kujiuzulu kazi kutokana na ushawishi wa mwajiri kufuatia mazingira ya kazi yaliyopo.

Napenda ieleweke katika makala hii ya kwamba haina lengo la kuwatetea wafanyakazi wasio waadilifu au wabadhilifu wa mali ya mwajiri, bali kuzingatia kwa hakika sababu na utaratibu wa haki katika kushughulikia nidhamu ya wafanyakazi. Endapo mfanyakazi atakuwa na makosa ya nidhamu basi, mwajiri anapaswa kuchukua hatua zote za kinidhamu kama inavyostahili kwa kuendesha vikao vya kinidhamu na kuchukua hatua zinazostahili kwa mfanyakazi husika.

Hata hivyo baadhi ya waajiri kwa kukosa ushahidi au weledi wa utaratibu wa kuchukua kwenye matukio yanayohusu tabia na mwenendo wa wafanyakazi hutafuta njia ya mkato ya kuwezesha mfanyakazi husika kuondoka kazini, na njia moja wapo ni kumshawishi kwa vitisho au kwa ahadi ambazo haziwezi kutekelezeka na hatimaye mfanyakazi anapoteza haki yake akiwa kazini na hata anapokuwa nje ya kazi.

Hivyobasi, ni muhimu sana mfanyakazi kutafakari kwa kina na kutafuta ushauri kwa wataalam wa sheria za kazi na ajira ili kujua ni mazingira yapi yanaweza kumfaa katika kuchukua uamuzi wa kujiuzulu kazi au la.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

2 replies

Comments are closed.