Sheria Jinai.3. Kwa nini watu hawatoi taarifa za Kijinai?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wetu na mfuatiliaji wa makala mbali mbali za mtandao wa uliza sheria. Katika makala iliyopita tuliangalia wajibu wa kutoa taarifa juu ya makosa ya jinai. Leo tunakwenda kujibu swali kwa nini watu hawatoi taarifa za Kijinai. Karibu ndugu msomaji tujufunze.

Wajibu wa Kutoa taarifa

Katika makala iliyotangulia tuliweza kuona ya kwamba kila mmoja wetu anao wajibu wa kutoa taarifa juu ya makosa ya kijinai yaliyofanyika au yanayopangwa kufanyika. Wajibu huu ni wa kila mmoja wetu ambaye anajua au amesikia kuhusiana na tukio lolote la kijinai.

Changamoto za utoaji wa taarifa za Kijinai

Hatahivyo, zinajitokeza changamoto za utoaji wa taarifa za kijinai ambazo kwa sehemu kubwa hizo changamoto zinasababisha vyombo vya kiuchunguzi kushindwa kupata taarifa sahihi, kwa wakati na za hakika.

Kwa hakika vitendo vya kijinai vinafanyika ndani ya jamii na kwa namna yoyote ile wana jamii wanayo au wanakuwa na taarifa ya kile kilichofanyika au kinachopangwa kufanyika. Hatahivyo, kwa sababu mbalimbali wanajamii wanashindwa kutoa ushirikiano au kutoa taarifa kwa vyombo husika kwa wakati ili kuweza kuepusha jinai au kupelekea wahalifu kukamatwa.

Baadhi ya changamoto zinazozuia wananchi au watu wenye taarifa za matukio ya kijinai ni kama ifuatavyo;

  1. Mfumo wa utoaji wa taarifa

Watu wengi hawaamini juu ya mfumo wa utoaji wa taarifa za kihalifu. Sheria inaelekeza kuwa mwenye taarifa anapaswa kuwasilisha taarifa husika kwa afisa wa Polisi kwenye kituo cha karibu. Mfumo huu unamtaka mtoa taarifa mwenyewe kufika na kutoa taarifa kwenye kituo au kutoa taarifa kwa mtu mwenye mamlaka ikiwa ni serikali ya mtaa au kijiji naye aiwasilishe kwenye kituo. Mfumo huu unawapa mashaka watu wengi kuhusiana na usiri juu ya kile ambacho wanasema endapo watakuwa salama.

  1. Kutochukuliwa hatua wahalifu

Pamekuwa na malalamiko kwa wananchi juu ya taarifa wanazotoa kutokuchukuliwa hatua kwa wahalifu. Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa wanatoa taarifa juu ya uhalifu na wahalifu lakini hawaoni taarifa zao zikifanyiwa kazi ipasavyo. Watu hawaoni hatua zikichukuliwa na baadhi ya wahalifu wanaendelea na maisha yao kama kawaida.

  1. Kusumbuliwa kwa watoa taarifa

Wananchi pia wanahofu ya kupata usumbufu pale ambapo wanatoa taarifa. Ipo dhana ya kuwa endapo unatoa taarifa juu ya uhalifu basi vyombo vya uchunguzi vinaanza na wewe mtoa taarifa. Wapo baadhi ya watu wanaotoa ushuhuda juu ya kusumbuliwa kutokana na taarifa wanazotoa. Kutokana na hofu ya kusumbuliwa kwa taarifa ambazo mtu ametoa basi wanaona ni afadhali kukaa kimya na hivyo uhalifu kuendelea.

  1. Usiri

Suala la usiri juu ya utambulisho wa mtoa taarifa na taarifa husika limekuwa ni sehemu mojawapo ya changamoto za watoa taarifa. Watoa taarifa wamekuwa na hofu ya taarifa zao kujulikana na watu wengine au wale ambao taarifa zimetolewa dhidi yao. Watu wana hofu kuwa taarifa walizotoa au wanazotaka kutoa zinaweza kuwafikia wale ambao zimetolewa dhidi yao na hatimaye wakapata madhara wao binafsi au familia zao.

  1. Hofu ya kuwa shahidi

Ipo dhana kuwa ukitoa taarifa za uhalifu basi wewe mtoa taarifa utakuwa shahidi wa kwanza katika suala hilo. Wengi wana hofu ya kwamba endapo watatoa taarifa basi watawajibika kushughulikia suala hilo mpaka mwisho wake yaani mahakamani. Hii ni sababu mojawapo kubwa ambayo inawarudisha wengi wasitoe taarifa za kihalifu.

Hizi ni baadhi tu ya sababu ambazo zinawafanya watu wasiwe wepesi kutoa taarifa kuhusiana na taarifa za kihalifu.

Katika makala inayofuata tutaangalia juu ya mambo yanayoweza kufanyika ili watu au wananchi waweze kuwa huru kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com