Sheria Jinai.2. Wajibu wa Kutoa Taarifa za Makosa ya Jinai

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wetu na mfuatiliaji wa makala mbali mbali za mtandao wa uliza sheria. Katika makala iliyopita tulipata utangulizi juu ya sheria hii ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Leo tunaangazia juu ya Wajibu wa Kutoa Taarifa za Makosa ya Jinai. Karibu ndugu msomaji tujufunze.

Taarifa Msingi wa Mwenendo wa Makosa

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 kwa sehemu kubwa msingi wake umejengwa juu ya taarifa. Ili sheria hii iweze kufanya kazi inapaswa kuwepo na taarifa juu ya kosa au kusudio la kosa la kijinai.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Kifungu cha 7 kinaeleza wazi juu ya jukumu la kila mmoja wetu kutoa taarifa endapo utakuwa na ufahamu juu ya kosa lililotendeka au linalokusudiwa kutendeka.

  1. Mtu yoyote anayejua au atakayejua:-
  • kutendeka au kusudio la mtu yoyote kutenda kosa linaloadhibiwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu; au
  • tukio lolote la kifo cha ghafla au kisicho cha asili au kifo kitokanacho na ukatili au kifo chochote kilicho katika mazingira yenye kutia shaka au mwili wa mtu yeyote aliyekutwa amekufa bila kujua jinsi mtu huyo alivyokufa,

atatakiwa wakati huohuo kutoa taarifa kwa afisa polisi au kwa mtu mwenye madaraka katika sehemu hiyo ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwa afisa polisi msimamizi wa kituo cha polisi kilicho karibu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 7 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, inamtaka kila mtu pasipo kujali cheo, umri, jinsia, rangi au nasaba yake, endapo atakuwa na taarifa kuhusiana na vitendo vinavyoashiria kosa la kijinai basi atoe taarifa wakati huo huo.

Sheria hii ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 inafanya kazi pamoja na Sheria ya Kanuni za Adhabu  Sura ya 16. Sheria ya Kanuni za Adhabu inabainisha aina mbali mbali ya makosa ya jinai na adhabu zake. Hivyo upo umuhimu mkubwa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kuifahamu sheria ya Kanuni za Adhabu ili kujua ni vitendo gani vinaonesha kuwa ipo jinai au haipo au ni aina ya makusudio gani yanaweza kuwa mipango ya utendaji wa makosa ya jinai au la.

Kama tulivyoeleza katika makala ya utangulizi ya kwamba changamoto kubwa katika utendaji kazi wa sheria hii ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ni uelewa mdogo wa wananchi ambao ndio wadau wa msingi katika utekelezaji wa sheria hii. Wananchi wengi hawajui au hawana maarifa sahihi juu ya uwepo wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, sheria inayoanisha aina mbalimbali za makosa.

Watu wengi wana uelewa wa maeneo machache sana ya utendaji wa makosa ikiwa ni makosa ya uhalifu, ukatili au mauaji n.k lakini ndani ya sheria ya Kanuni za Adhabu yapo makosa mengi sana achilia mbali sheria nyingine.

Itoshe tu kusema katika makala hii ya awali, kwamba kila mmoja wetu anao wajibu wa kutoa taarifa zitakazoweza kusaidia kuzuia utendaji au utekelezwaji wa makosa ya kijinai, na endapo tayari kosa limefanyika basi vyombo vinavyohusika vianze kuchukua hatua mapema.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com