58. Utaratibu wa Kushughulikia Nidhamu Kazini

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeona juu ya kujiuzulu kwa hila. Leo tunaangalia juu ya Utaratibu wa Kushughulikia Nidhamu Kazini. Karibu tujifunze.

Nidhamu Kazini

Ni matarajio baina ya mwajiri na mfanyakazi kuwa mahali pa kazi ni kwa ajili ya kuzalisha. Hata hivyo inatarajiwa mfanyakazi afuate taratibu na maelekezo ya mwajiri.

Waajiri wengi hawana utaratibu au hawafuati utaratibu wa kisheria katika kushughulikia masuala ya kinidhamu dhidi ya wafanyakazi. Waajiri wanatumia vitisho, ubabe na hila katika kushughulikia masuala hayo. Sheria ya ajira inawataka waajiri kuwa na mfumo wa kanuni na mwongozo wa utendaji kazi mahali pa kazi ili kusaidia upatikanaji wa haki na kuepusha upendeleo.

Katika kushughulikia masuala ya kinidhamu mahali pa kazi, Mwajiri atazingatia utaratibu wa kutoa ushauri kwa mfanyakazi na endapo hali haitabadilika basi, mwajiri atatoa onyo la mdomo na kisha onyo la maandishi kama hatua za awali.

Utaratibu wa kushughulikia nidhamu mahala pa kazi unapaswa kuwa kama ifuatavyo;

  1. Kutoa Ushauri

Madhumuni ya msingi ya hatua za kushughulikia nidhamu ni kurekebisha tabia za wafanyakazi ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na tabia zinazokubalika. Njia ya msingi ya kufanikisha lengo hili ni kuwapatia ushauri wafanyakazi utakaotolewa na mwajiri, ambao atawafafanulia wafanyakazi wanatarajiwa kufanya nini. Kama hili halikufanikisha malengo yaliyokusudiwa, itabidi kuchukua hatua kali zaidi.

  1. Onyo la Mdomo

Pale ambapo mwajiriwa atafanya kosa dogo au kufanya kazi kwa ubora wa chini, hatua za kuchukua itakuwa onyo kwa mdomo ikifuatiwa na maelekezo kutoka kwa meneja wa mwajiriwa arekebishe tabia. Maonyo haya ni pamoja na hatua za kurekebisha zisizo rasmi na hazitaingizwa kwenye faili binafsi la mwajiriwa.

  1. Onyo kwa Maandishi

Onyo kwa maandishi linaweza kutolewa na msimamizi au meneja, kama utendaji kazi au tabia ya mwajiriwa haijabadilika kufuatia ushauri na onyo kwa mdomo au kama tabia mbaya au utendaji wa kazi unahitaji kuchukuliwa hatua badala ya onyo kwa mdomo.

Meneja amtaarifu mwajiriwa sababu za hatua iliyochukuliwa, na kumpatia mwajiriwa fursa ya kujieleza. Wakati wa mchakato huu, mwajiriwa anaweza kuwa na mwakilishi aliyeteuliwa kuhudhuria. Mchakato huu usichukuliwe kama usikilizaji wa shauri rasmi.

Baada ya kufikiria maelezo yaliyotolewa, Meneja aamue kama atampatia au hatampatia mwajiriwa onyo kwa maandishi. Onyo lolote litolewe kwa mwajiriwa binafsi.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa waajiri kuzingatia utaratibu wa haki katika kushughulikia nidhamu mahali pa kazi, hii itasaidia uzalishaji mahali pa kazi na kuepusha uonevu mahali pa kazi. Utaratibu huu unasaidia katika kujenga mahusiano bora mahali pa kazi.

Hata hivyo ieleweke kuwa yapo makosa makubwa ambayo akiyafanya mfanyakazi hayatahitaji kufuata mchakato huu, makosa hayo yatapelekea kuchukuliwa hatua za nidhamu moja kwa moja za kuitisha kikao cha kinidhamu na kuweza kusitishiwa ajira.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com