64. Nifanye Nini ukomo wa muda wa madai ukipita?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala iliyopita tumeangalia juu ya ukomo wa muda katika mashauri ya kazi hasa suala la madai ya mishahara. Tumeona jinsi sheria inavyoweka muda wa kufuatilia madai. Leo tunaangalia juu nini unaweza kufanya endapo muda wa ukomo wa madai umeisha. Karibu tujifunze.

Ukomo wa Muda

Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya masharti yaliyowekwa na sheria ambayo yanampasa mdau wa sheria za kazi kuzingatia katika madai. Ukomo wa muda ni jambo la msingi sana na kuzingatia katika madai yoyote. Hakuna mtu anaruhusiwa kwenda mahakamani kwa muda anaotaka yeye, kila shauri lina muda wake, na muda ukipita basi unaweza kupoteza haki yako ya madai.

Kama tulivyonukuu katika Sheria ya Kazi kwa mujibu wa Kanuni ya 10 (1) na (2) ya Taasisi za Kazi (Usuluhishi na Uamuzi) T.S. Na.64/2007 ambayo inasema

(1) ‘Mgogoro  kuhusu uhalali wa kumwachisha kazi mfanyakazi lazima ukatiwe rufaa kwenye Tume ndani ya siku thelathini kuanzia tarehe ya kumwachisha kazi au tarehe ambayo mwajiri ametoa uamuzi wa mwisho wa kumwachisha kazi au kuthibitisha uamuzi wa kumwachisha kazi’

(2) ‘Migogoro mingine yote iwasilishwe kwenye Tume ndani ya siku sitini kuanzia tarehe ya kuanza mgogoro’

Nini kifanyike endapo ukomo wa muda umepita?

Yapo mazingira ambayo yanaweza kusababisha mwajiri au mfanyakazi kuchelewa kufungua mgogoro ndani ya muda wa siku 30 au 60 kama sheria inavyoelekeza.

Hatahivyo, ni muhimu kufahamu ya kuwa upo uwezekano wa kisheria wa kupata fursa ya madai yako kusikilizwa nje ya muda kama utafuata utaratibu wa kisheria.

Maombi ya kuwasilisha mgogoro nje ya Muda

Sheria ya kazi na ajira kwa kutambua uwepo wa mazingira yanayoweza kusababisha upande wowote kuchelewa kuwasilisha mgogoro ndani ya muda, imeweka utaratibu wa uwasilishwaji wa mgogoro nje ya muda kwa maombi maalum.

kwa mujibu wa Kanuni ya 11 (1), (2) na (3)  ya Taasisi za Kazi (Usuluhishi na Uamuzi) T.S. Na.64/2007 ambayo inasema

  1. Kanuni hii itatumika kwenye mgogoro wowote, waraka wa rufaa au maombi uliowasilishwa nje ya muda ulioanishwa kwenye Sheria au Kanuni hizi
  2. Mhusika ataomba muda wa ziada kwa kujaza na kuwasilisha fomu ya muda wa ziada kwenye Tume. Fomu hii lazima itolewe kwa wahusika wote wa mgogoro.
  3. Ombi la muda wa ziada litaeleza sababu za kutaka muda huo na litajumuisha maelezo ya mhusika anayekata rufaa juu ya yafautayo-

a. Kiwango cha kuchelewa;

b. Sababu za kuchelewa;

c. Matarajio yake ya kufanikiwa katika mgogoro na kupata nafuu anayoitafuta dhidi ya mhusika mwengine;

d. Madhara yoyote kwa upande mwengine; na

e. Sababu nyingine zozote zinazohusiana

Ni muhimu sana kuzingatia kabla ya kufungua mgogoro ujiridhishe ya kwamba upo ndani ya muda husika. Endapo utaona upo nje ya muda basi ufuate utaratibu wa kuwasilisha maombi ya kisheria nje ya muda.

Kanuni hizi pia zinaongoza kuwa maombi haya yanapaswa kuambatanishwa na Taarifa ya Maombi na Kiapo sawa na 29 (1) (a) (2), (3) (4) ya Taasisi za Kazi (Usuluhishi na Uamuzi) T.S. Na.64/2007.

Maombi ya kusikilizwa nje ya muda yanapaswa kusikilizwa kwanza kabla maombi ya msingi kusikilizwa na Tume au Mahakama. Ikiwa sababu za msingi zimetolewa na kuridhisha Tume basi uamuzi utatolewa kuruhusu mgogoro wa msingi kufunguliwa nje ya muda.

Hitimisho

Ni muhimu sana kuzingatia suala la muda katika mgogoro wa kazi kwani uwasilishwaji wa mgogoro nje ya muda kunaweza kuhatarisha haki zako na Tume au Mahakama isisikilize madai yako. Fuatilia muda wa mgogoro na chukua hatua mapema.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com