71. Athari za Kisheria kwa Uamuzi wa kuingia mkataba wa Kazi maalum

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni  ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tumeangalia athari za kisheria endapo mwajiri atafanya uamuzi wa kuingia mahusiano ya kiajira na mwajiriwa katika mkataba wa muda maalum.

Leo tunakwenda kujifunza juu ya athari za kisheria kwa uamuzi wa kuingia mkataba wa kazi maalum. Karibu tujifunze.

Aina za Mkataba

Sheria ya Ajira inatambua aina kuu tatu za mikataba ya ajira kama zilivyoanishwa katika Kifungu cha 14 (1) (c) inaeleza juu ya uwepo wa mkataba wa kazi maalum.

Ufafanuzi

Mkataba wa kazi maalum – hii ni aina ya mkataba ambapo mwajiri anaingia na mwajiriwa kwa ajili ya kutekeleza kazi maalum. Mwisho wa mkataba huu ni pale kazi inapokamilika. Aina ya mkataba huu imetafsiriwa katika baadhi ya mashauri na Mahakama ya Kazi kama mkataba wa siku. Aina ya mkataba huu malipo hufanyika mara baada ya kazi kumalizika.

Athari za kisheria katika mahusiano ya mkataba wa muda maalum

  • Mkataba huu wa ajira unaendelea tangu mwajiriwa alipoanza kazi mpaka kazi husika inapomalizika.
  • Mara nyingi mkataba huu malipo yake hufanyika kwa kutwa au wiki kutegemea na ukubwa wa kazi husika.
  • Mkataba huu unasitishwa pale mwajiri anapoona hakuna kazi ya ziada au inayoendelea kwa kutoa taarifa au malipo ya siku 4 badala ya taarifa.
  • Mkataba huu hauna mlolongo wa utaratibu wa usitishwaji wake kama ile ya muda maalum au wa kudumu.
  • Endapo mwajiri atashindwa kufuata utaratibu, basi mwajiriwa ana haki ya kukata rufaa mbele ya Tume  kupinga uamuzi wa mwajiri.
  • Endapo Tume itaona hapakuwa na utaratibu wa kuachishwa kazi katika mkataba wa kazi maalum inaweza kuamuru mwajiriwa husika kumlipa mfanyakazi kiasi cha notisi ya siku 4 au siku 7 na madai mengine kama yakithibitika. Mfano kiasi cha fedha walichokuwa wamekubaliana kulipwa kutokana na kazi au ukamilishwaji wa sehemu ya kazi. Mwajiriwa katika mkataba wa kazi maalum hawezi kulipwa fidia ya miezi 12 kwani si mkataba wa kudumu, wala hawezi kulipwa kiasi cha muda wa mkataba uliobaki kwani si mkataba wa kipindi maalum.

Kwa upande mwengine, endapo mwajiriwa anakusudia kusitisha ajira yake na mwajiri wake ambapo ana mkataba wa kazi maalum anaweza kufanya hivyo endapo

  • Muda wa mkataba wa kazi maalum utakuwa umekwisha
  • Ataamua kujiuzulu kazi kwa kutoa taarifa ya maandishi.

Ndugu msomaji, masharti ya mkataba wa kazi maalum ni tofauti kabisa na masharti kwenye mikataba mingine. Hatahivyo ni muhimu kufahamu mwajiri hapaswi kutoa mkataba wa kazi maalum kwa shughuli ambazo ni sehemu ya uendeshaji wa kazi zake. Mfano mwajiri ni taasisi inayotoa elimu, hawezi kutoa mkataba wa kazi maalum kwa walimu, ila anaweza kufanya hivyo kwa mafundi au watu wanaofanya usafi n.k

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com