75. Mjue vizuri Mwajiriwa wako

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulianza kujifunza Kanuni ya tatu juu ya Namna bora ya kupata mwajiriwa mwenye vigezo. Tumeangalia baadhi ya vigezo vya kisheria, vigezo vya ziada na vigezo bora zaidi. Kwa hatua tuliyofikia ni dhahiri mwajiri anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata mwajiriwa bora zaidi miongoni mwa waombaji wengi.

Leo tunakwenda kujifunza juu ya Kanuni ya nne inayomtaka mwajiri kumjua viuri mwajiriwa wake. Karibu tujifunze.

Umuhimu wa taarifa

Katika makala ya Uchambuzi wa Sheria.66 tuliangalia juu ya umuhimu wa taarifa katika kujenga mahusiano ya kiajira. Taarifa katika mahusiano yoyote ni kitu cha msingi sana kuzingatiwa na kuhakikisha kuwa una taarifa sahihi. Kadhalika kwenye mahusiano ya kiajira, ni kazi ya mwajiri kuhakikisha anazo taarifa zote muhimu kuhusiana na mfanyakazi/mwajiriwa wake. Tumeona juu ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na.6/2004 katika Kifungu cha 15 kinaeleza wazi wajibu wa mwajiri kuhakikisha anampatia mwajiriwa maelezo ya kumbukumbu ambayo yanabeba taarifa za msingi juu ya mwajiriwa.

Maendeleo ya Teknolojia

Kuna msemo usemao kuwa ‘nioneshe marafiki zako nitakueleza tabia yako’ au ‘show me your friends and I will tell your character’. Huu ni msemo wa kweli sana hasa katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Maisha ya sasa yanaenda kasi sana na taarifa juu ya watu ni rahisi zaidi kuzipata. Mwajiri anao wigo mpana wa kumjua zaidi mwajiriwa anayetaka kufanya naye kazi.

Katika zama hizi za matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii, mwajiri anaweza kunufaika na taarifa anazoweza kuzipata kumuhusu mwajiriwa wake na hasa kujua aina ya tabia zake. Tunafahamu kwa sehemu kubwa waajiriwa wa kizazi cha sasa wanajihusisha sana na mitandao ya kijamii kama facebook, twiter, instagram, watsup, telegram, na mengine mingi.

Eneo la mitandao ya kijamii ni eneo mojawapo lenye fursa kubwa ya kumjua hasa mwajiriwa juu ya tabia yake na hulka yake jinsi anavyohusiana na watu wengine nje ya kazi. Ni muhimu sana katika kuhakikisha mwajiri unapata mtu aliye bora zaidi na mwenye uwezo wa kuleta tija kazini kufahamu juu ya wafanyakazi wako na namna wanavyotumia mitandao ya kijamii. Ni rahisi wengine kuona kuwa hayo ni maisha binafsi ya mwajiriwa wako wala hupaswi kuyaingilia, shida sio kuyaingilia bali namna gani maisha ya mwajiriwa wako nje ya eneo la kazi yanavyoweza kuathiri shughuli zake au utendaji wake mahali pa kazi.

Tatizo kubwa

Kwa sasa kumejengeka aina kubwa ya uraibu au ulevi katika matumizi mabovu ya mitandao ya kijamii. Tumeshuhudia juu ya picha, au video au maneno mabaya yanayotoka miongoni mwa wananchi. Wananchi hao kwa njia moja ama nyingine ni waajiriwa wa maeneo fulani. Ni muhimu kwa mwajiri kuhakikisha anapata taarifa namna mwajiriwa anavyohusiana na watu wengine nje ya kazi na endapo mahusiano hayo yanaweza kuwa na athari gani katika kazi za kila siku.

Pia uraibu na ulevi wa matumizi ya simu yasiyodhibitiwa mahali pa kazi kwa sehemu kubwa yamechangia kushuka kwa ufanisi, tija na maendeleo na ubunifu mahali pa kazi. Pata picha unaenda katika ofisi moja kwa mara ya kwanza kuhudumiwa kisha unamkuta  mtu wa mapokezi ‘receptionist’ unamuuliza juu ya huduma anakujibu huku anaangalia simu yake muda wote, wewe utapata picha gani au unaenda kuongea na muhusika unayemtafuta ili kutatua shida yako muda wote anachat kwenye simu unapata picha gani juu ya taasisi au kampuni husika.

Hali hii ilianza taratibu lakini kwa sasa imeshika kasi sana miongoni mwa waajiriwa vijana. Kutwa kucha wapo kwenye mitandao hawana muda wa kazi.

Hitimisho

Umuhimu wa kumjua vizuri mwajiriwa wako hasa kwenye eneo la matumizi ya mitandao ya kijamii si kwa lengo la kuingilia uhuru wa mawasiliano ila ni kwa ajili ya kutunza utamaduni na viwango vya huduma vya eneo lako la kazi, na kuweka mifumo thabiti ya kuhakikisha mwajiriwa hakuibii muda wako wa kazi kwa kufanya mambo yake akitagemea mshahara kutoka kwako.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com