76. Wasiliana na watu muhimu kuhusu mwajiriwa wako

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulianza kujifunza Kanuni ya nne inayomtaka mwajiri kumjua vizuri mwajiriwa wake. Tumeona umuhimu wa kuwa na taarifa binafsi zinazohusiana na mwajiriwa wako.

Leo tunendelea kuangalia Kanuni ya 5 juu ya namna bora ya kukusanya taarifa kuhusu mwajiriwa wako kupitia watu wengine muhimu. Karibu tujifunze.

Umuhimu wa taarifa

Katika kuhakikisha mwajiri unapata mwajiriwa bora zaidi miongoni mwa waombaji wengi wenye vigezo hakuna mbadala zaidi ya kupata taarifa sahihi na za wakati kuhusiana na mwajiriwa wako. Ikiwa mwajiri unataka kupata watu bora lazima utengeneze mfumo wa kupata taarifa muhimu zinazohusu mwajiriwa.

Kanuni ya 5

Waajiriwa wengi wanapoomba kazi au kuajiriwa katika taasisi huambatanisha na CV zao zikielezea wao ni nani na wana vigezo gani. pamoja na CV hizo huambatanisha na mawasiliano ya wadhamini au ‘referees’ ambao wana taarifa kuhusiana na waajiriwa hao. Hata hivyo suala la ‘referees’ limekuwa likichukuliwa kwa mazoea tu wala waajiri hawachuku taarifa hizi kwa umakini na hivyo kukosa fursa ya kupata taatifa zaidi kuhusu mwajiriwa huyo, juu ya utendaji kazi wake, bidii yake na tabia yake mahali pa kazi au nje ya kazi.

Mwajiri ana wigo mkubwa wa kupata taarifa kwa kuwatumia ‘referees’ ambao majina yao na mawasiliano yao yamewasilishwa kwenye CV za waombaji. Mwajiriwa anaweza kuwasiliana na nao kwa njia ambayo si lazima mwajiriwa afahamu inaweza kuwa kwa fomu maalum ambayo inauliza maswali muhimu kuhusiana na tabia za mwajiriwa husika.

Pia mwajiri anaweza kupata taarifa zaidi kwa kutaka majina au taasisi zaidi za kuwasiliana nazo kuhusiana na mwenendo wa mwajiriwa. Taarifa hizi ni muhimu zipatikane mapema zaidi wakati mwajiriwa akiwa katika kipindi cha majaribio endapo mkataba wake unaruhusu kuwa na kipindi cha majaribio.

Waajiriwa wanapaswa kujenga tabia ya nidhamu katika kazi na mwenendo mzuri katika jamii kwani waajiri wana wigo mpana wa kuweza kutafuta taarifa zinazohusu wao na mwenendo wao. Maisha ya nidhamu mahali pa kazi yanamsaidia mwajiriwa pindi anapoondoka mahali fulani katika ajira na kwenda kwengine aondoke vizuri. Kumekuwa na changamoto ya waajirwa kutokuwa waaminifua au kuondoka kwa matatizo ya kinidhamu, tabia mbovu au ubadhilifu. Waajiriwa wakijua mwajiri anafuatilia taarifa mahali walipotoka watachukua taadhari.

Hitimisho

Kuna umuhimu mkubwa wa kupata taarifa za mwajiriwa wako kuhusiana na namna ya mwenendo wake katika kazi au mahali alipotoka kwa watu muhimu wanaofahamu mwenendo wake kabla ya kuajiriwa katika taasisi yako. Hali hii itakusaidia sana kufanya maamuzi ambayo tayari una taarifa za kutosha.

Hatahivyo, mwajiri ni lazima awe makini na taarifa hizo anazopata kwani wengine watoa taarifa wanaweza wasiwe waaminifu katika kutoa taarifa za uongo juu ya mwajiriwa kwa lengo la kumpendelea apate ajira au kumwaribia sifa ili akose ajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com