77. Toa Mkataba wa Maandishi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulianza kujifunza Kanuni ya 5 juu ya namna bora ya kukusanya taarifa kuhusu mwajiriwa wako kupitia watu wengine muhimu.

Leo tunaangalia juu ya Kanuni ya 6  ya kuhakikisha unatoa mkataba wa maandishi. Karibu tujifunze.

Umuhimu wa Mkataba wa Maandishi

Kwa kupitia makala mbalimbali ambazo tumetangulia kuzichambua tumeeleza wazi ya kuwa ni jukumu la mwajiri kuhakikisha mwajiriwa anapata mkataba wa maanidishi. Mkataba wa maandishi una umuhimu mkubwa kwa pande zote kwa kusaidia kufahamu haki zao na wajibu wao katika kutekeleza masharti ya mkataba.

Kanuni ya 6

Kifungu cha 14 (2) cha Sheria ya Ajira ya 2004 kinaeleza wazi sharti la mwajiri kutoa mkataba wa maandishi kwa mwajiriwa bila kujali endapo anafanya kazi ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama tulivyoona ufafanuzi wa Kanuni ya 2 ya kufanya uamuzi juu ya aina ya mkataba ambao mwajiri anapaswa kuutoa na mfululizo wa ufafanuzi juu ya kila aina ya mkataba, hivyo katika kanuni hii ya 6 mara baada ya kufanya maamuzi na kupata mtu anayehitajika na taasisi basi ni jukumu la mwajiri kuhakikisha anatoa mkataba husika. Mkataba huo unaweza kuwa usio wa muda maalum, wa kipindi maalum au kazi maalum.

Kumbuka aina ya mkataba itaamua aina ya haki na wajibu unaostahili kila upande endapo ajira itakoma kwa sababu yoyote ile. Hivyo mwajiri ni lazima awe makini katika kuchagua na kuandaa mkataba husika.

Kutokutoa mkataba wa maandishi kunaweza kuhatarisha haki za mwajiri endapo ajira itakoma kwani mwajiriwa anaweza kufungua madai dhidi ya mwajiri kwamba alikuwa na mkataba wa kudumu au usio wa muda maalum wakati kwa uhalisia mwajiriwa na mwajiri walikuwa katika makubaliano ya muda au kazi maalum.

Sheria ya ajira imeweka wazi kabisa juu ya jukumu la mwajiri kuthibitisha mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi juu ya aina ya makubaliano baina yake na mwajiriwa. Namna bora na rahisi itakayomsaidia mwajiri kuthibitisha makubaliano hayo ni kuhakikisha yameandikwa.

Athari za kutotoa mkataba wa maandishi kwa mwajiri

  • Uwezekano wa kufunguliwa mashtaka na kulipa faini kwa kukiuka Sheria ya Ajira
  • Uwezekano wa mwajiriwa kudai madai ambayo hakustahili kisheria na kulipwa kwa mwajiri kukosa uthibitisho wa kimkataba
  • Uwezekano wa mwajiriwa kudai kuwa amekuwako kazini muda mrefu zaidi wakati kiuhalisia ameanza kazi muda si mrefu hivyo kusababisha mwajiri kuwajibishwa.

Hatua za kufanya

Mara mwajiri anapoamua kumwajiri mfanyakazi ahakikishe makubaliano yanaandaliwa;

  • Mkataba wa maandishi uandaliwe kwa lugha ambayo inaeleweka na pande zote
  • Kuwe na nakala mbili halisi (original) yaani nakala moja kwa ajili ya mwajiri na nyingine kwa ajili ya mwajiriwa
  • Nakala zote zitiwe sahihi na pande zote na ziwekwe tarehe zinazoanisha mwanzo wa mkataba huo na ukomo wake

Masharti mengine ya mkataba wa ajira kwa kadri mwajiri na mwajiriwa watakavyokubaliana.

Hitimisho

Waajiri wengi wanafikiri kutokutoa mkataba wa maandishi kunawanufaisha wao na kuwakomoa waajiriwa, hii ni kinyume chake, hata pasipo mkataba wa maandishi bado mwajiriwa anaweza kudai madai ya kiajira na kushinda kirahisi sana. Mwajiri anapoteza fursa ya masharti yaliyoanishwa kwenye mkataba wa ajira kuwa kigezo kikuu cha kuamua haki na wajibu wake.

Kutoa mkataba wa ajira ni suala la kisheria na amri ya Sheria ya Ajira na sio ombi au hiyari ya mwajiri kufanya au kutokufanya. Waajiri wengi hawatoi mikataba na pale wanapoulizwa na wafanyakazi huwatishia kuwafukuza au kuwafukuza kabisa, hii sio sawa. Sheria ya Ajira imeweka hatua kali za kuchukua endapo mwajiri atakaidi kutokutoa mkataba wa ajira kwa wafanyakazi. Chukua hatua sasa ya kutoa mkataba ili kulinda haki zako kama mwajiri na maslahi yako katika kazi.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com