78. Ainisha Masharti ya Majaribio

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulianza kujifunza ya Kanuni ya 6  ya kuhakikisha unatoa mkataba wa maandishi.

Leo tunakwenda kutazama Kanuni ya 7 ya kuzingatia pindi mwajiri anapomwajiri mfanyakazi ni kuhakikisha anaainisha masharti ya majaribio. Karibu tujifunze.

Kipindi cha Majaribio

Imezoeleka katika mikataba mingi ya ajira mwajiri huweka kifungu kinachohusu kipindi cha majaribio au ‘probation period’. Kifungu hiki kwa sehemu kubwa kinaeleza juu ya mwajiriwa kuwa chini ya uangalizi kabla ya kuthibitishwa kama mwajiriwa halali kwa kipindi cha muda Fulani. Muda huo unaweza kuwa mwezi 1 au 3 au 6 au 12 kutegemeana na mahitaji ya uangalizi anayotaka mwajiri.

Sheria ya Ajira na Kanuni zake zinaelekeza ya kuwa endapo mkataba wa ajira utahusisha suala la uwepo wa kipindi cha majaribio, basi ni muhimu kwa masharti hayo ya majaribio kuwekwa wazi kwa mfanyakazi ili aweze kujua ni kiwango gani cha utendaji kinachotarajiwa kwake na kuzingatia masharti husika.

Kanuni ya 7

Ainisha masharti ya majaribio

Waajiri wengi wanaishia tu kuweka kifungu ndani ya mkataba wa ajira ya kuwa mfanyakazi atakuwa kwenye majaribio kwa kipindi cha meizi kadhaa. Kifungu cha mkataba kuonesha juu ya uwepo wa kipndi cha majaribio hakitoshi kuhalalisha kipindi hicho bila masharti ya majaribio kuwekwa bayana kati ya pande zote.

Napenda kunukuu kanuni ya 10 (2) ya Ajira na Mahusiano (Utedaji Bora) Tangazo la Serikali Na.42/2007 kinachosema

Terms of probation shall be made known to the employee before the employee commences employment’ 

Kwa tafsiri nyepesi kanuni hii ina maana ya kuwa ‘masharti ya majaribo ni lazima yajulikane kwa mfanyakazi kabla hajaanza kazi’

Maswala ya msingi ambayo mwajiri anapaswa kujadili na kuweka wazi kwa mwajiriwa aliye chini ya kipindi cha majaribio yanahusu;

  • Muda wa majaribio
  • Majukumu ambayo mfanyakazi anapaswa kuyatekeleza katika kipindi cha majaribio
  • Vigezo vitakavyotumika kupima utendaji wa kazi wa mfanyakazi aliye chini ya kipindi cha majaribio
  • Muda wa kupimwa endapo mwajiriwa anakidhi vigezo na masharti ya kipindi cha majaribio

Athari za kutotoa mkataba wa maandishi kwa mwajiri

Waajiri wengi kwa kutokujua suala la kipindi cha majaribio huishia tu kuandika kwenye mkataba kuhusu uwepo wa kipindi cha majaribio bila kuainisha masharti yanayoambatana na kipindi husika.

Athari za kutoainisha masharti ya majaribio;

  • Kushindwa kujua endapo mwajiriwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo
  • Mwajiri kukosa vigezo vya kisheria vya kuchukua uamuzi dhidi ya mwajiriwa aliye chini ya kipindi cha majaribio
  • Uamuzi wa mwajiri kutokudhibitisha mfanyakazi aliye chini ya majaribio unaweza kubatilishwa endapo mfanyakazi atalalamika mbele ya Tume

Hatua za kufanya

Endapo mwajiri anakusudia kuweka kipindi cha majaribio basi anapaswa kufuata hatua zifuatazo;

  • Kuainisha kifungu kinachohusiana kipindi cha majaribio
  • Kuhakikisha masharti ya majaribio yanaainishwa katika barua ambayo mwajiriwa na mwajiri wataisaini kwa pamoja
  • Kuainisha muda ambao mwajiri atakuwa anampima mwajiriwa kama anakidhi vigezo vya ajira alivyowekewa.

Hitimisho

Suala la kuweka kipindi au kifungu kinachohusu majaribio si suala la lazima katika mkataba wa ajira baina ya mwajiri na mwajiriwa ni hiyari ya mwajiri. Hatahivyo endapo mwajiri anakusudia kuweka kifungu cha majaribio basi ni lazima afuate masharti ya kisheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Isaack Zake, WakiliMwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com