79. Fanya Tathmini ya Utendaji wa Mfanyakazi aliye katika Kipindi cha Majaribio.
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulijifunza Kanuni ya 7 ya kuzingatia pindi mwajiri anapomwajiri mfanyakazi ni kuhakikisha anaainisha masharti ya majaribio.
Leo tunaendelea kujifunza zaidi kuhusu kanuni ya 7 kwa mwajiri kufanya tathmini juu ya mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio. Karibu tujifunze.
Kipindi cha Majaribio
Kama tulivyoainisha katika makala iliyopita juu ya uwepo wa kifungu cha muda wa majaribio katika mkataba wa ajira baina ya mwajiri na mfanyakazi. Waajiri wengi wanaweka kifungu hiki lakini hawafuati masharti ya kuhakikisha masharti ya majaribio yanawekwa wazi kwa mwajiriwa pia.
Hadhi ya mfanyakazi aliye katika kipindi cha majaribio
Kumekuwa na dhana tofauti kuhusiana na hadhi ya mfanyakazi aliye katika kipindi cha majaribio endapo ni mfanyakazi kama wengine au ana utofauti.
Je, sheria inamtazama vipi mfanyakazi aliye katika kipindi cha majaribio, je ana haki kama mfanyakazi mwengine ambaye ameshafuzu kipindi cha majaribio?
Sheria ya Ajira inamtazama mfanyakazi aliye katika kipindi cha majaribio kama mtu aliye katika usaili wa utendaji yaani ‘practical interview’. Tunafahamu kuna ngazi mbalimbali za usaili inaweza kuwepo usaili kwa njia ya kuandika, njia ya mdomo. Inapotokea mtu amefuzu katika usaili huo wa ngazi ya kwanza anapata mkataba wa ajira mahali pa kazi ambao una sharti la kuwa katika majaribio basi hiyo ni ngazi nyingine ya usaili kwa njia ya utendaji.
Kumekuwa na changamoto kubwa kwa waajiri kutokujua kuwa wafanyakazi walio katika kipindi cha majaribio si wafanyakazi wenye haki zote kama wengine na kadhalika waajiriwa walio katika kipindi cha majaribio nao wanadhani wana haki zote kama wafanyakazi wengine. Mtazamo huu ndio unaleta kutokueleweka msingi wa uwepo wa kifungu cha majaribio.
Hitaji la tathmini
Sheria ya Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora kama ilivyoanishwa katika Kanuni ya 10 (6) (a) na (b) ya Ajira na Mahusiano (Utedaji Bora) Tangazo la Serikali Na.42/2007 kinachosema
During the period of probation, the employer shall–
- Monitor and evaluate the employee’s performance and suitability from time to time;
- Meet with the employee at regular intervals in order to discuss the employee’s evaluation and to provide guidance if necessary. The guidance may entail instruction, training and counselling to the employee during probation
Kwa tafsiri nyepesi kanuni hii ina maana ya kuwa katika kipindi cha majaribio mwajiri anapaswa
- Kusimamia na kufuatilia utendaji wa mwajiriwa endapo unaendana na masharti ya majaribio mara kwa mara
- Mwajiri kukutana na mwajiriwa ili kujadili na kutathmini etendaji wake na kutoa mwongozo unaostahii. Mwongozo huo unaweza kuhusisha maelekezo, mafunzo na ushauri katika kipindi cha majaribio
Msingi wa kufanya tathmini ya mwenendo wa utendaji wa mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio ni kwa lengo la mwajiri kujiridhisha ili kufanya maamuzi sahihi ya kumwajiri au kutokumwajiri kikamilifu mfanyakazi husika.
Uzoefu unaonesha waajiri wengi pamoja na kuweka vifungu vya uwepo wa kipindi cha majaribio hawana mfumo wa kuwatathmini wafanyakazi hao walio katika kipindi cha majaribio na hivyo kusababisha migogoro isiyo na ulazima. Ili mwajiri atende haki kwa mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio ni lazima masharti ya majaribio yawe wazi na uwepo wa tathmini ya pamoja baina ya mwajiri na mwajiriwa.
Hatua za kufanya
Endapo mwajiri ameainisha kwenye mkataba wa ajira kuhusu uwepo wa kipindi cha majaribio ni lazima ifahamike ya kuwa;-
- Mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio bado yupo katika hali ya usaili katika vitendo.
- Masharti ya majaribio ni lazima yawekwe wazi kimaandishi na kusainiwa na pande zote
- Kuwe na kipindi cha tathmini kati ya mwajiri na mwajiriwa na tathmini hiyo ifanyike kwa maandishi
- Mwajiri atoe nafasi ya mwajiriwa kuboresha utendaji wake kwa kumpa ushauri, mafunzo na mwongozo katika utendaji wake.
- Masharti ya majaribio na tathmini ya utendaji vinapaswa kutunzwa katika faili la mwajiriwa vikiwa vimesainiwa na pande zote.
Hitimisho
Haitoshi tu kuweka kifungu cha uwepo wa kipindi cha majaribio au kumfahamisha mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio masharti ya majaribio, inafaa zaidi kufanya tathmini ya utendaji wa mwajiriwa huyo ambaye kisheria sio mwajiriwa halisi mpaka pale atakapofuzu kipindi cha majaribio. Ili kuondoa migogoro na pande zote kuona haki inatendeka basi ni lazima mwajiri atengeneze mfumo wa kufanya tathmini juu ya utendaji wa mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Nakutakia siku njema ndugu yangu.
Isaack Zake, Wakili
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com