80. Fanya Uamuzi ndani ya muda

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala iliyopita tulijifunza Kanuni ya 7 ya kuzingatia pindi mwajiri anapomwajiri mfanyakazi ni kuhakikisha anaainisha masharti ya majaribio na  mwajiri kufanya tathmini juu ya mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio.

Leo tunaendelea kujifunza kuhusu kufanya maamuzi ndani ya muda  kuhusu mfanyakazi aliye katika kipindi cha majaribio. Karibu tujifunze.

Kipindi cha Majaribio

Kama tulivyoainisha katika makala iliyopita juu ya uwepo wa kifungu cha muda wa majaribio katika mkataba wa ajira baina ya mwajiri na mfanyakazi. Kipindi cha majaribio kinaweza kuwa ni miezi 3 au 6 au 12 kutokana na mahitaji ya mwajiri kulingana na majukumu ya mwajiriwa.

Halikadhalika tumeeleza juu ya msimamo wa Sheria ya Ajira kuhusu mfanyakazi aliye katika kipindi cha majaribio kama mtu aliye katika usaili wa utendaji yaani ‘practical interview’. Katika kipindi hiki cha majaribio mfanyakazi anakuwa bado hajathibitishwa kama mfanyakazi kamili mpaka pale kipindi cha majaribio kitakapomalizika na kufanyiwa tathmini itakayoweza kuamua hatma yake.

Umuhimu wa kufanya tathimini kama tulivyoona katika makala iliyopita ni kwa lengo kuu la kumsaidia mwajiri kufanya maamuzi sahihi wakati sahihi. Kukosekana kwa tathmini ya mwajiriwa aliye katika kipindi cha majaribio kunampatia mwajiri wakati mgumu pindi atakapotaka kumwachisha mwajiriwa aliye katika kipindi hiki kwani anakosa msingi wa haki wa kufanya hatua hiyo.

Nini kinatokea endapo muda wa majaribio unaisha bila mwajiri kufanya uamuzi wa kumthibitisha mwajiriwa au kutokumthibitisha?

Pia kumekuwa na kutokuelewa kwa baadhi ya waajiri na waajiriwa pindi muda wa majaribio unapokamilika bila mwajiri kuchukua hatua za uamuzi wa kuthibitisha ajira au la. Mtazamo wa waajiri na waajiriwa wengi ni kuwa mwajiriwa huyo atakuwa mfanyakazi kamili. Mtazamo huu si sahihi kabisa kwani kitendo cha mwajiri kutochukua hatua ya kuthibitisha ajira ya mwajiriwa hakubadilishi hadhi ya mwajiriwa kutoka katika hali ya mwajiriwa chini ya majaribio na kuwa mwajiriwa kamili. Yapo mashauri kadhaa yaliyoamuliwa na Mahakama Kuu ya Kazi katika kuthibitisha msimamo huu wa kisheria.

Athari za kutokufanya uamuzi

  • Kutokurasimisha mahusiano ya kiajira baina ya mwajiri na mwajiriwa
  • Mwajiri kukosa nafasi nzuri ya kuweza kumpatia mwajiriwa majukumu sahihi kutokana na nafasi anayotakiwa kuifanyia kazi
  • Uwezekano wa mwajiriwa kufungua shauri la madai endapo atasitishiwa ajira yake katika kipindi cha majaribio pasipo kufuata taratibu za masuala ya kazi.
  • Mwajiriwa kukoseshwa haki zake na fursa ya ajira

Hitimisho

Ni muhimu ifahamike kipengele cha uwepo wa muda wa majaribio katika makubaliano ya kiajira si suala la kupendezesha tu mkataba wa ajira bali ni suala la kisheria lenye utaratibu wake unaopaswa kufuatwa kama tulivyoona katika mfululizo wa makala katika kanuni ya 7 ya mwajiri kuzingatia katika hatua za kuajiri mwajiriwa. Endapo mwajiri ana nia ya kutaka kumweka mwajiriwa katika kipindi cha majaribio basi ni lazima azingatie masharti ya kisheria yanayoambatana na kipindi cha majaribio.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com