81. Usajili wa Mwajiriwa katika Mamlaka husika

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala zilizopita tulijifunza Kanuni ya 7 ya kuzingatia pindi mwajiri anapomwajiri mfanyakazi na masharti mahsusi kuhusu kipindi cha majaribio.

Leo tunajifunza juu ya Kanuni ya 8 ambayo mwajiri anapaswa kuzingatia juu ya Usajili wa Mwajiriwa katika mamlaka husika. Karibu tujifunze.

Kanuni ya 8

Usajili wa Mwajiriwa katika Mamlaka

Suala la ajira pamoja na kuwa ni mahusiano binafsi baina ya mwajiri na mwajiriwa bado ni suala ambalo Serikali ina maslahi mapana kuhakikisha linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zote. Mahusiano ya kiajira yaliyo bora na yenye kuzingatia sheria yanahakikisha juu ya uzalishaji, tija na maendeleo katika Taifa. Mfumo wa kisheria unaotekelezeka unasaidia kuhakikisha kundi kubwa la uzalishaji linalindwa maslahi yake yote.

Hivyo wigo wa masuala ya kiajira katika sheria hauishii katika utekelezaji wa Sheria ya Ajira Na.6 ya 2004 pekee bali inahusisha baadhi ya sheria nyingine na taasisi au mamlaka za kiserikali kwa lengo la kuhakikisha maslahi mapana ya pande zote mbili yaani mwajiri na mwajiriwa yanazingatiwa.

Mamlaka za Usajili kuhusu Ajira

Masharti yanayohusiana na ajira yanamtaka mwajiri kuhakikisha anasajili au kuandikisha mahusiano ya kiajira baina yake na mwajiriwa katika mamlaka kadhaa ambazo zina maslahi kuhusiana na ajira hizo. Zifuatazo ni mamlaka ambazo mwajiri anawajibika kuandikisha uhusiano wa kiajira.

  1. Mamlaka ya Mapato – TRA

Sheria ya Kodi ya Mwaka 2004 inamtaka mwajiri kuhakikisha anatoa taarifa juu ya mahusiano ya kiajira baina yake na mwajiriwa kwa lengo la kukusanya kodi inayotokana na mapato ya mfanyakazi. Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kukata kodi na kuiwasilisha kwenye Mamlaka ya Mapato yaani TRA kwa kila wakati mwajiriwa anapopokea malipo kulingana na viwango vya kodi vya mwaka husika.

2. Mifuko ya Pensheni

Sheria ya Mifuko ya Pensheni inamtaka mwajiri awasajili wafanyakazi katika mifuko husika. Awali kulikuwa na uchaguzi wa mifuko ya pensheni mbalimbali, hatahivyo mwaka 2018 mabadiliko ya Sheria zinazohusu mifuko imeunda mifuko miwili tu yaani ule kwa ajili ya wafanyakazi wa Umma na ule unaohusu wafanyakazi kwenye sekta binafsi. Pindi mwajiriwa anapoanza kazi, taarifa zake zinapaswa kuwasilishwa kwenye mifuko hii kwa lengo la kukata makato ya kila mwezi kama akiba ya uzeeni. Sheria inaelekeza juu ya uchangiaji wa jumla ya asilimia 20 ya mshahara wa mwajiriwa unaochangiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa.

3. Mfuno wa Fidia kwa Wafanyakazi

Sheria ya Fidia ya Wanyakazi ya mwaka 2008 pamoja na Kanuni zake za 2015 zinaeleza juu ya uundaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Tunafahamu mahali pa kazi mwajiriwa anaweza kuumia au kukumbwa na ajali au ugonjwa. Mwajiri anapaswa kuhakikisha amejiandikisha katika Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi kwa ajili ya kutumika kama fidia endapo mwajiriwa atakutwa na matatizo yatakayoathiri afya yake na utendaji wa kazi.

4. Chama cha Wafanyakazi

Mwajiri ana wajibu wa kuhakikisha anamruhusu mwajiriwa kujiunga na chama cha wafanyakazi anachotaka. Hii ni muhimu kwani wapo baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwazuia wafanyakazi kujiunga na chama cha wafanyakazi, hii ni kinyume cha Sheria. Mwajiri anapaswa kuruhusu mwajiriwa kujiunga na chama na kulipa michango inayohusu mwanachama kutoka kwenye mshahara wa mwanachama.

Kumekuwa na malalamiko kwa wafanyakazi wengi wanaokatwa kodi au michango ya mifuko ya pensheni lakini hawana uhakika zinapokwenda. Wengine wanazuiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi na wanaumia kazini lakini hakuna utaratibu wa fidia. Mwajiri anawajibika kuhakikisha matakwa ya sheria yanatimizwa kikamilifu kuhusiana na usajili katika maeneo haya ili kuepusha hatua za kisheria dhidi yake.

Mwajiriwa lazima ahakikishe kuwa ana namba ya mlipa kodi, namba ya usajili wa mifuko ya pensheni, kujua namba ya usajili katika mfuko wa fidia na kwa hiyari yake usajili katika chama cha wafanyakazi. Wafanyakazi wengi hawana muda wa kufuatilia mambo haya mpaka pale matatizo yanapotokea ikiwa ni kuumia, au kuachishwa kazi ndipo huanza kulalamika na kuhangaika kuwa hakutendewa haki. Muda ni sasa kwako mwajiri kutekeleza sheria na mwajiriwa kudai haki hiyo itekelezwe kikamilifu bila hofu ya kupoteza kazi, kwani sheria inambana mwajiri kutokuchukua hatua za kinidhamu au kukuachisha kazi kwa sababu ya kudai haki yako ya kutekelezwa kwa sheria.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa mwajiri kuzingatia na kutekeleza sheria kikamilifu kwa kuhakikisha anamsajili au anasajili mahusiano ya kiajira katika mamlaka zinazohusika. Kinyume cha hapo mwajiri anaweza kuchukuliwa hatua za kijinai au madai kulingana na taratibu na sheria zinazohusu mamlaka ambazo anapaswa kusajili mahusiano ya kiajira.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com