82. Kumwongoza mwajiriwa katika Sera za Mahusiano ya kiajira ndani ya Taasisi
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Katika makala zilizotangulia tumeangalia mambo mbalimbali yanayohusu sheria za kazi na namna zinavyoathiri mahusiano baina ya mfanyakazi na mwajiri. Tumeanza kujifunza kanuni mbalimbali ambazo mwajiri anapaswa kuzingatia pale anapokusudia kuajiri mfanyakazi. Makala zilizopita tulijifunza Kanuni ya 8 ambayo mwajiri anapaswa kuzingatia juu ya Usajili wa Mwajiriwa katika mamlaka husika.
Leo tunajifunza juu ya Kanuni ya 9 ambayo inamtaka mwajiri kuhakikisha anamjulisha mwajiriwa Sera zinazohusu ajira katika taasisi yake. Karibu tujifunze.
Kanuni ya 9
Kumwongoza mwajiriwa kwenye Sera za Ajira
Sera za ajira ndani ya taasisi ni mwongozo mpana juu ya namna mahusiano baina ya mwajiri na mwajiriwa yanapasa kuwa kwa lengo la kutimiza maono na kufanikisha malengo ya taasisi. Sheria ya Ajira inazitaka taasisi au ofisi ya mwajiri kuwa na mfumo wa sera za kiajira ambazo zitaongoza mahusiano baina ya mwajiri na mwajiriwa mbali na mkataba wa ajira.
Si kila kitu kinachohusu ajiri kinaweza kuandikwa kwenye mkataba wa ajira, bali yapo mambo mengine ya utaratibu wa kuajiri, mwongozo wa utendaji kazi na namna ya kushughulikia malalamiko au tabia ya waajiriwa vinawekwa kwenye sera maalum ambayo kwa lugha ya kiingereza zinaitwa ‘Employment Policies’.
Mwajiri anawajibika kwa mujibu wa sheria za ajira kuhakisha sera husika zinafahamika na kueleweka vizuri na mwajiriwa pindi anapoanza kufanya kazi ili ziwe mwongozo wa utendaji wake na endapo atakiuka mwongozo husika basi mwajiri anayo fursa ya kuchukua hatua dhidi ya mwajiriwa kwa mujibu wa sheria na sera mahali pa kazi.
Kifungu cha 7(1), (9) (c) cha Sheria ya Ajira ya 2004
(1)‘Kila mwajiri atahakikisha kwamba anakuza fursa sawa katika ajira na kupambana kutokomeza ubaguzi katika Sera yoyote ya ajira au katika utendaji’
(9) Kwa maudhui ya kifungu hiki;-
- ……………………
- ……………………
- ‘sera au utaratibu wa ajira’ ni pamoja na sera au utaratibu wowote unaohusiana na taratibu za kuajiri, vigezo vya utangazaji na uchaguzi, uteuzi na mchakato wa uteuzi, uainishaji wa kazi na madaraja, ujira, faida za ajira na kanuni na masharti ya ajira, upangaji wa kazi, mazingira ya kazi na vifaa, mafunzo na maendeleo, mifumo ya tathmini, upadishaji vyeo, kushusha cheo, kuachisha kazi na hatua za nidhamu
Tunaona maeneo ambayo sheria imeainisha yanayohusu sera zinazohusu uhusiano wa kiajira baina ya mwajiri na mwajiriwa ambazo mwajiriwa anapaswa kufahamishwa kikamilifu ni kama ifuatavyo;
- Sera au mwongozo kuhusu taratibu za kuajiri
- Sera au mwongozo kuhusu vigezo vya utangazaji, uchaguzi na uteuzi
- Sera au mwongozo unaoainisha madaraja ya kazi
- Sera au mwongozo unaohusu ujira
- Sera au mwongozo unaohusu faida za ajira na kanuni ya masharti ya ajira
- Sera au mwongozo unaohusu upangaji wa kazi, mazingira ya kazi na vifaa vya kazi
- Sera au mwongozo unaohusu mafunzo na maendeleo ya mwajiriwa
- Sera au mwongozo unaohusu mifumo ya tathmini, upandishaji vyeo na kushusha vyeo
- Sera au mwongozo unaohusu kuachisha kazi na hatua za nidhamu
- Sera au mwongozo wa namna ya kuhusiana na wafanyakazi wenye maambukizi ya VVU n.k
Sera hizi ni jambo la kisheria na ni kazi ya mwajiri kuhakikisha sera hizi zipo na zinafanya kazi katika mahusiano yake na mwajiriwa tangu anapoanza kazi.
Uwepo wa sera na mwongozo mahali pa kazi utahakikisha ujenzi wa mahusiano sahihi ya kiajira yanayoongozwa na sheria, kanuni, sera na mazoea ya utendaji bora pasipo kuhusisha hisia binafsi za watu au upendeleo au unyanyasaji kwa namna yoyote. Utendaji unaozingatia sera za kiajira unampa uhakika mwajiriwa na hali ya kutekeleza majukumu yake kwa kutegemea mwongozo wa kazi na kuzalisha tija na manufaa mahali pa kazi.
Mwajiri hakikisha unaendesha shughuli za kazi au taasisi yako kwa kuzingatia sheria za ajira na sera mahsusi ili waajiriwa watende kwa mujibu wa mwongozo na kile kinachotarajiwa mahali pa kazi.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.
Nakutakia siku njema ndugu yangu.
Isaack Zake, Wakili
Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com