86. Ukomo wa Muda kwa madai ya Saa za Ziada

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwasumbua wafanyakazi na waajiri ni suala la malipo ya saa za ziada. Nimepata maswali mengi katika eneo hili kutoka pande zote wakitaka kujua utaratibu na hasa suala la malipo. Nimekuandalia makala hii siku ya leo kujifunza suala la saa za ziada na namna ya kudai malipo hayo ndani ya muda. Karibu tujifunze.

Saa za Ziada (Over time)

Ili kufahamu juu ya saa za ziada au ‘Over time’ ni lazima tufahamu suala la msingi juu ya saa za kazi za kawaida. Sheria ya Ajira inamtaka mwajiri kumpangia mfanyakazi saa zisizozidi 45 kwa juma. Hizi ni saa za kawaida. Saa hizi zinaweza kugawanywa kwa kila siku kwa siku 5 au 6 za juma. Mfano mfanyakazi anaweza kufanya kazi kwa saa 8 kwa siku tano kisha siku ya sita akafanya kazi kwa saa 5 kukamilisha saa 45 za juma.

Endapo mwajiri atamtaka mwajiriwa kufanya saa za ziada katika siku mojawapo au siku kadhaa ndani ya juma basi, Sheria ya Ajira imeweka utaratibu wa namna saa hizo zitakavyohesabiwa na malipo yake. Sheria ya Ajira kupitia Kifungu cha 19 kimeeleza wazi juu ya matumizi ya saa za kawaida na saa za ziada katika ajira.

Masharti ya kuzingatia kuhusu saa za kazi

  • Lazima masaa ya kawaida yawe yamekamilika ikiwa ni saa 8 au 9 kwa siku
  • Mfanyakazi haruhusiwi kufanya kazi zaidi ya saa 12 kwa siku ikijumlisha saa za kazi kawaida na saa za ziada
  • Saa za ziada hazitakiwi kuzidi saa 3 kwa siku
  • Mfanyakazi atakayefanya kazi saa za ziada anastahili kulipwa  angalau 1.5 ya mshahara wake wa saa kwa kila saa ya ziada aliyofanya kazi.
  • Saa za ziada hazipaswi kuzidi 50 katika mzunguko wa wiki 4

Ili mfanyakazi aweze kufanya kazi kwa saa za ziada ni lazima yawepo makubaliano ndani ya mkataba wa ajira au makubaliano ya ziada ya kimaandishi kuhusiana na ufanyaji kazi katika saa za ziada.

Mfano: Saa za kazi za kawaida ni saa 9 kwa siku ikiwa mwajiri anataka mfanyakazi afanye kazi na saa za ziada kwa siku zitaongezeka saa 3 tu hivyo kufanya jumla ya saa za kazi kwa siku kuwa 12.

Ukomo wa Muda wa Madai ya Saa za Ziada

Kumekuwa na changamoto ya waajiriwa wengi kujikuta wanafanya kazi katika saa za kawaida na hata za ziada kwa muda mrefu pasipo kulipwa huku wakipewa ahadi ya kulipwa na waajiri wao. Wengine hawana ufahamu hasa ni kiasi gani wanachopaswa kulipwa kwa saa za ziada.

Sheria ya Ajira imeweka wazi juu ya ukomo wa muda katika kufuatilia haki au madai ya saa za ziada. Sheria ya Ajira inamtaka mwajiriwa kupeleka malalamiko yake mbele ya Tume ndani ya siku 60 tangu pale mwajiri aliposhindwa kulipa madai juu ya saa za ziada au ‘over time’.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 10 (1) na (2) ya Taasisi za Kazi (Usuluhishi na Uamuzi) T.S. Na.64/2007  inasema

(1) ‘Mgogoro  kuhusu uhalali wa kumwachisha kazi mfanyakazi lazima ukatiwe rufaa kwenye Tume ndani ya siku thelathini kuanzia tarehe ya kumwachisha kazi au tarehe ambayo mwajiri ametoa uamuzi wa mwisho wa kumwachisha kazi au kuthibitisha uamuzi wa kumwachisha kazi’

(2) ‘Migogoro mingine yote iwasilishwe kwenye Tume ndani ya siku sitini kuanzia tarehe ya kuanza mgogoro’

Kwa mantiki ya vifungu hivi vya sheria mgogoro wa kuachishwa kazi ni lazima upingwe ndani ya siku 30 huku migogoro mingine yote ukiwamo na kushindwa kulipwa madai ya saa za ziada, inapaswa kuwasilishwa mbele ya Tume ndani ya siku 60 tangu tarehe ya kuanza mgogoro.

Huu ndio msimamo wa kisheria kuhusiana na madai ya saa za kazi za ziada ambazo mfanyakazi amezifanyia kazi.

Changamoto ya Hofu

Wafanyakazi wengi wanashindwa kudai haki zao za kiajira kutokana na hofu kubwa ya kupoteza ajira zao. Hatahivyo hofu hii haipaswi kuwepo kwani Sheria ya Ajira inamlinda mfanyakazi anayefuata sheria katika kutimiza haki zake. Si ruhusa kwa mwajiri kumwachisha mfanyakazi ajira kwa sababu anadai haki yake.

Wafanyakazi wanaogopa kufuatilia haki zao na pindi wanaposhtuka ni pale wanapoachishwa kazi na kujikuta wamepoteza muda wa kisheria kufuatilia madai yao ya msingi na halali kama ufanyaji wa kazi kwa saa za ziada. Ipo mifano ya watu wengi wana malimbikizo ya madai ya saa za ziada zaidi ya miaka 5 hawajawahi kulipwa na wala hawajachukua hatua mapema. Nikueleze tu mapema ikiwa madai yako ya kulipwa saa za ziada yanazidi muda wa siku 60 tangu mwajiri alipokiuka kukulipa basi haki hiyo umeshaipoteza. Hofu yako ndio kuangamia kwako na kujikosesha haki zako za msingi.

Hatua za kuchukua

Endapo upo kwenye mahusiano ya kiajira ambayo kwa namna yoyote yanahusisha ufanyaji kazi kwa saa za ziada basi kuna hatua za msingi za kuchukua wakati huu ili kuhakikisha haki zako na mwajiri zinalidwa;

  • Hakikisha suala la ufanyaji wa kazi kwa saa za ziada lipo katika makubaliano ya maandishi
  • Hakikisha malipo ya kila saa la ziada hayapungui 1.5 ya malipo ya mshahara wa saa. Hii ina maana mfanyakazi anapaswa kulipwa kiasi cha ziada katika kila saa la ziada 1.5 ya malipo yake ya kawaida katika saa.
  • Hakikisha malipo ya saa za ziada yanalipwa pamoja na mshahara wako ikiwa ni mwisho wa mwezi au wiki basi na malipo ya saa za ziada yawepo
  • Iwapo malipo ya saa za ziada hayajalipwa katika muda muafaka, basi mjulishe mwajiri kwa maandishi juu ya kulipwa malipo hayo katika mwezi au awamu nyingine unayofanya
  • Endapo zitaendelea kutokulipwa saa hizo za ziada kwa mfululizo kabla ya siku 60 kumalizika unaweza kufungua shauri la madai ya malipo yako.

Hizi ni hatua muhimu sana kuchukua ili kulinda haki yako ya kiajira, ukisubiri siku umesitishiwa ajira yako ili udai madai yahusuyo saa za ziada utakuwa umechelewa sana.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com

1 reply

Comments are closed.