87. Ukomo wa Muda kwa madai ya Likizo

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Kama tulivyoona katika makala iliyopita juu ya ukomo wa muda kwa madai ya saa za ziada, kadhalika changamoto hiyo inaonekana katika madai ya likizo. Eneo la likizo pia limekuwa na changamoto hasa katika madai yake. Nimekuandalia makala hii siku ya leo kujifunza suala la madai ya likizo na ukomo wake. Karibu tujifunze.

Haki ya Likizo

Suala la likizo ni suala la haki ya kiajira kwa kila mfanyakazi aliyefanya kazi kwa mwajiri mmoja kwa kipindi kisichopungua miezi 12 mfululizo. Hii ni likizo ya mwaka ambayo kila mfanyakazi anapata haki ya kupumzika kwa siku 28 kwa kila mwaka wa kazi.

Makundi ya wafanyakazi wanaostahili kupata likizo ya malipo ni;

 • Waliofanya kazi kwa zaidi ya miezi 6 mfululizo
 • Wafanyakazi wa msimu
 • Wafanyakazi waliofanya kazi kwa kipindi tofauti kwa mwajiri mmoja katika mwaka iwapo vipindi husika vikijumlishwa vitazidi miezi sita

 Likizo ya Mwaka

Kwa mujibu wa Kifungu cha 31 cha Sheria ya Ajira, mwajiri anawajibika kumpatia mwajiriwa likizo ya mwaka kwa utaratibu ufuatao.

 • Mfanyakazi anastahili kupewa likizo ya siku 28 mfululizo katika mzunguko wa miezi 12
 • Siku za likizo zinaweza kukatwa endapo mfanyakazi alipewa ruhusa mbalimbali
 • Mwajiri ana haki ya kuamua siku ya kuanza likizo kwa mfanyakazi ndani ya miezi 6 kuanzia siku ambayo mfanyakazi alistahili kuanza likizo
 • Muda wa kuanza likizo baada ya miezi 6 unaweza kuongezwa kwa makubaliano iwapo yapo mahitaji ya uendeshaji na nyongeza ya muda wa kuanza likizo isizidi miezi 12
 • Mfanyakazi hapaswi kufanya kazi wakati wa likizo
 • Likizo ya mwaka haitakiwi kuchukuliwa wakati wa likizo nyingine au wakati wa kipindi cha notisi ya kusitisha ajira.
 • Mwajiri ni lazima amlipe mfanyakazi mshahara wake wakati wa likizo

Ukomo wa Muda wa Madai ya Likizo

Suala la likizo kama masuala mengine ya haki za kiajira lina ukomo wake katika kudai. Sheria ya Ajira imeweka wazi utaratibu wa mtu kudai likizo ambao unapaswa kufuatwa. Hatahivyo tumeshuhudia waajiriwa wengi wamekuwa wakidai malimbikizo ya likizo zaidi ya miaka 2 hadi 10 kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Kuna mifano ya watu ambao hawajawahi kwenda likizo kwa kipindi cha miaka 5 wala kulipwa madai ya likizo kwa mujibu wa sheria.

Sheria ya Ajira imeweka wazi juu ya ukomo wa muda katika kufuatilia haki ya likizo.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 31 (3) cha Sheria ya Ajira inaelekeza mwajiri kuamua suala la likizo ya mwaka kuchukuliwa lini

 • Likizo ya mwaka inaweza kuchukuliwa pindi tu mzunguko wa miezi 12 unapokamilika
 • Miezi sita baada ya kupita mzunguko wa likizo
 • Miezi kumi na mbili baada ya kupita mzunguko wa likizo endapo mwajiriwa ameridhia na sababu za kusogeza muda zinatokana na mahitaji ya uendeshaji wa mwajiri

Hii ina maana mwajiri hawezi wala hana mamlaka ya kupitisha mwaka 1 wa likizo ya mwajiriwa yaani haiwezekani mwajiriwa kulimbikiza likizo 2 kwa wakati mmoja. Sheria imeweka wazi mazingira ya mwajiri kuamua lini kutoa likizo kutozidi miezi 6 au miezi 12 baada ya mzunguko wa likizo kwa sababu maalum.

Hii ina maana endapo mwajiriwa hatoenda likizo au kulipwa madai ya likizo ya mwaka kwa zaidi ya miezi 12 tangu kuwa na haki ya likizo basi kisheria ameipoteza likizo yake.

Kwa nini waajiriwa wanalimbikiza likizo?

Zipo sababu kadhaa za waajiriwa kujikuta wanalimbikiza likizo zaidi ya moja mfano

 • Kutokujua haki ya likizo ya mwaka na namna ya kuidai
 • Waajiri kutokujua suala la likizo ni haki ya msingi
 • Hofu ya kudai likizo na kudhani inaweza kusababisha kupoteza kazi

Hatua za kuchukua

Endapo upo kwenye mahusiano ya kiajira ambayo kwa namna yoyote yanahusisha ufanyaji kazi kwa miezi 12 basi una haki ya likizo ya mwaka ambapo unahitaji kuchukua hatua zifuatazo;

 • Mwajiri na mwajiriwa fahamu ya kuwa suala la likizo ni haki ya kiajira kwa mfanyakazi aliyefanya kazi miezi 12 mfululizo
 • Pindi muda wa likizo ukifika ni vyema mwajiriwa kumtaarifu mwajiri kwa maandishi hitaji lake la kwenda likizo
 • Mwajiri atoe sababu endapo likizo ya mwajiriwa itasogezwa mbele kuzidi miezi sita tangu mzunguko wa likizo kufika
 • Endapo mwajiriwa atanyimwa kwenda likizo katika kipindi cha miezi 12 mwajiriwa anaweza kufungua mgogoro mbele ya Tume kudai haki ya likizo

Hizi ni hatua muhimu sana kuchukua ili kulinda haki yako ya kiajira, ukisubiri siku umesitishiwa ajira yako ili udai madai yahusuyo malimbikizo ya likizo utakuwa umechelewa sana.

Kwa ushauri zaidi usisite kuwasiliana nasi kama inavyoelekezwa hapo chini katika makala hii.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com