88. Ufanye nini endapo mfanyakazi haonekani kazini pasipo ruhusa?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ambapo tumekuwa tukiichambua Sheria ya Kazi. Moja ya changamoto ambayo imekuwa ikiwakuta waajiri ni suala la wafanyakazi kuondoka kazini na kutoonekana kwa siku au miezi kadhaa pasipo taarifa au mawasiliano yoyote. Hali hii imeibua maswali mengi na hatma ya wafanyakazi kama hawa. Nimekuandalia makala hii kujibu hoja hii na hatua ambazo mwajiri anaweza kuchukua. Karibu tujifunze.

Matakwa ya mkataba wa Ajira

Kama tunavyofahamu juu ya uhusiano wa kiajira ni mahusiano yanayojengwa kwa mujibu wa mkataba yaani makubaliano ya kisheria baina ya mwajiri na mwajiriwa. Pande zote mbili kuna masharti na wajibu ambao wanapaswa kuzingatia ili kufanikisha lengo la makubaliano. Upo wajibu anaopaswa kutimiza mwajiri na upo wajibu ambao anapaswa kutimiza mwajiriwa.

Ni matakwa ya mkataba na sheria ya Ajira kuwa mwajiriwa anapaswa kuudhuria eneo la kazi pasipo kukosa kulingana na maelekezo ya mkataba au makubaliano. Kitendo cha mwajiriwa kutokuonekana kazini bila ruhusa au taarifa zilizodhibitishwa na mwajiri ni kitendo kinachoashiria ukosefu wa utovu wa nidhamu.

Utovu wa Nidhamu

Utovu wa nidhamu maana yake ni kufanya mambo kinyume na mwongozo au tararibu za ajira sehemu ya kazi. Katika mahusiano ya kiajira baina ya mfanyakazi na mwajiri kuna mfumo wa mwenendo ambao unatarajiwa mfanyakazi auishi katika kutekeleza majukumu yake. Kutoka nje ya mfumo huo wa kimatendo kunasababisha makosa ambayo yanaonekana ni utovu wa nidhamu ‘misconduct’. Utovu wa nidhamu ni sababu mojawapo ambayo inakubalika kwa mujibu wa Sheria ya Kazi na Ajira kupelekea usitishwaji wa ajira endapo itathibitishwa na kufuata utaratibu wa haki.

Utoro kazini

Kumekuwa na tabia ya utoro kazini kwa wafanyakazi wengi sana. Wafanyakazi hawaji kazini pasipo na sababu au kutoa sababu za uongo za kuwafanya wasije kazini. Sheria ya Kazi na Ajira kupitia Kanuni za Utendaji Bora ‘Employment and Labour Relations (Code of Good Prictice)’ inaeleza kuwa

‘kutokuwepo kazini pasipo ruhusa au sababu ya msingi kwa zaidi ya siku 5 za kazi ni kosa linaloweza kusababisha kusitishwa ajira kwa utovu wa nidhamu’

Endapo mfanyakazi atashindwa kufika kazini kwa siku 5 basi mwajiri anayo haki ya kuanzisha mashtaka ya kinidhamu na ikithibitika kuwa mfanyakazi ametenda kosa hilo, mwajiri anaweza kusitisha ajira ya mfanyakazi husika.

Changamoto

Tatizo kubwa linalojitokeza katika mahusiano ya kiajira wakati huu mwajiriwa anatoweka kazini na hakuna namna ya kupata mawasiliano yake hivyo kumtatiza mwajiri hatua za kuchukua. Waajiri wengi nao kwa kuona mwajiriwa haonekani hawachukui hatua yoyote. Hali hii imegeuka kuwa tatizo kwa waajiri kwani baadhi ya wafanyakazi baada ya kutoweka muda mrefu wanakuja kutokea Tume na kuleta madai dhidi ya mwajiri ya kuwa waliachishwa kazi pasipo sababu au kufuata utaratibu na kusababisha hasara kwa waajiri.

Katika makala hii nimekuandalia hatua ambazo kama mwajiri unapaswa kuzichukua endapo, mwajiriwa atatoweka kazini kwa muda mrefu yaani zaidi ya siku 5 na huna namna ya kumpata kwa mawasiliano yake au eneo analoishi.

Hatua za kuchukua

  1. Hakikisha wakati unaingia makubaliano na waajiriwa una taarifa zote muhimu za mwajiriwa. Hii ina maana uwe na fomu maalum ambayo mwajiriwa ataijaza kueleza mawasiliano yake yote na eneo lake la kuishi na endapo hapatikani ni nani wa kuwasiliana naye.
  2. Mara baada ya kutoonekana kwa siku 5 mfululizo, mwajiri unapaswa kumwandikia barua mfanyakazi na kuituma kwenye anauani aliyokupatia kwenye fomu au kuipeleka kwenye ofisi ya mtaa aliyosema anaishi katika fomu husika. Barua hiyo imtake kutoa maelezo kwa nini asichukuliwe hatua kwa sababu ya utoro.
  3. Endapo barua hiyo haitapata majibu katika kipindi cha siku 2 mpaka 7 basi unaweza kuandika barua nyingine ya kumtaka kufika katika kikao cha kinidhamu kwa tuhuma za utoro. Barua ieleze kikao kitakapofanyika na muda na haki zake katika kikao. Pia ifafanue endapo hatofika kikao kitaendelea bila ya uwepo wake na kufikia maamuzi.
  4. Endapo mwajiriwa husika hatofika siku ya kikao, basi mwajiri anaruhusiwa kuendesha kikao hicho na kufikia maamuzi ya kumwachisha kazi kwa utoro. Kikao kiandae muhtasari wa kusikilizwa shauri na maamuzi yaliyofikiwa.
  5. Mwajiri aandike barua ya kusitisha ajira ya mwajiriwa na sababu husika na kuituma kwenye anuani au ofisi ya mtaa ambayo alijaza kwenye fomu wakati wa kuajiriwa.

Mara baada ya kuzingatia hatua hizi mwajiri anakuwa amekamilisha mchakato mzima wa kisheria wa kumwachisha kazi mwajiriwa ambaye ametoroka kazini na kwa njia zozote ameshindwa kumpata. Hatua hizi zitamlinda mwajiri dhidi ya wafanyakazi wasio waaminifu ambao huku wakijua wametoroka wanarudi kufungua mashauri ya uongo dhidi ya mwajiri.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku.

Nakutakia siku njema ndugu yangu.

Isaack Zake, Wakili

Mwandishi Isaack Zake ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kujitegemea anayefanya katika ofisi za Uwakili Zake Advocates zilizopo Dar es Salaam, Mtaa wa Bibi Titi Mohamed. Isaack Zake anatoa elimu ya kisheria, ushauri wa kisheria na usimamizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali kama Sheria za Kazi, Mirathi, Ndoa, Mikataba na Biashara. Kwa ushauri usisite kuwasiliana naye kwa 0713 888 040 na email zakejr@gmail.com