Nini Maana ya Sheria?

Ndugu msomaji wa blog ya uliza sheria karibu sana katika makala ya kwanza katika ukurasa huu ambapo tutajibu swali juu ya ‘Nini Maana ya Sheria?’.
Wengi wetu tumekuwa tukisikia maneno yanayozungumzia ‘kwa mujibu wa sheria’ au ‘sheria ni msumeno’ au ‘tii sheria bila shuruti’n.k. Swali linakuja je, tunafahamu nini juu ya maana ya neno Sheria?. Fuatana nami katika makala hii na tuweze kujifunza maana ya sheria.

Maana ya Sheria
Sheria ni mfumo wa kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza matendo yao na mahusiano yao. Sheria pia ina maana ya utaratibu unaotengeneza mfumo na mwelekeo wa maisha chini ya mamlaka husika. Mifano ya kanuni hizo ni katika nchi, familia, ukoo, shule, ofisi n.k.

Jamii ni kundi la watu ambao wanaishi pamoja na kuendesha shughuli zao za maendeleo kitamaduni,kisiasa,kiuchumi na hata kidini katika makubaliano ambayo yanawekewa kanuni au utaratibu (sheria). Hivyo jamii yoyote haiwezi kuenenda au kukaa pamoja pasipo kuwa na sheria ya kuwaongoza.

Tafsiri ya neno sheria kama ilivyoainishwa katika makala hii inatusaidia kuona vipengele kadhaa vya muhimu ambavyo vitatusaidia kuelewa zaidi maana ya sheria.

1. Mfumo wa kanuni: hizi ni kanuni au taratibu zinazotumika au kufuatwa na watu walio chini ya mamlaka husika.

2. Mamlaka: inaashiria chombo katika jamii kilicho na wajibu wa kutunga au kupitisha sheria/kanuni zinazopaswa kutumika katika jamii.

3. Kuongoza matendo: kazi ya sheria ni kusaidia watu kuongozwa kwa matendo yao na mahusiano yao na wana jamii wengine.

4. Jamii: mkusanyiko wa watu wanaoishi kwa pamoja au wenye maslahi ya pamoja. Jamii inaweza kumaanisha wananchi,wafanyakazi,wanafunzi,wakulima,wafanyabiashara n.k.

umuhimu mkubwa wa sheria kwa jamii ni kuwasaidia kuishi kwa amani na kujiletea maendeleo na ustaei katika nyanja mbalimbali kama kitamaduni, kisiasa, kiuchumi na hata kiroho.

Hitimisho
Sheria ni msingi wa uhai wa jamii yoyote ile iwe kubwa au ndogo, zote zinahitaji uwepo wa sheria maana pasipo sheria kila mmoja atafanya atakayo kufanya na kutakosekana amani na uthabiti kwa maisha ya watu.

Ndugu msomaji wa makala za uliza sheria nakutakia usomaji mwema wa makala za kujifunza juu ya sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote‘ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nasi kupitia mtandao wako wa www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili.

12 replies
  1. Dany
    Dany says:

    Yah Isaac naamini hii website itatusaidia kuelewa kirahisi mambo ya kisheria na hasa tabaka la chini.Asante sana.

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Nashukuru sana kaka kwa hatua hii tutaendelea kushirikishana taaluma hii kwa manufaa ya watu wote.

  2. Elisonguo
    Elisonguo says:

    Asante kwa ukurasa huu na tovuti hii kwa ujumla. Nasubiria kwa hamu makala ya elimu juu ya makosa mbalimbali yanayohusiana na ununuzi/uuzaji na umilikaji wa ardhi na majengo.

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Karibu sana ndugu yetu Elisonguo tutaendelea kuweka makala za kutoa elimu katika maeneo mbali mbali ya sheria ikiwa ni pamoja na Sheria ya Ardhi.

  3. Pastor Emmanuel Dominic
    Pastor Emmanuel Dominic says:

    Wakili…neno sheria na neno kanuni…hutumika pamoja yaani yana maana moja? Naomba tofauti yake kama ipo. Maana utasikia kwa “kanuni na sheria” nisaidie kitaalamu tafadhali…

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Karibu sana Pastor Emmanuel

      Kwanza niombe radhi kwa kuchelewa kujibu swali lako, mtandao wetu kwa kipindi fulani ulikiwa kwenye marekebisho. Nikushukuru pia kwa ufuatiliaji na usomaji wako.
      Hakuna tofauti kubwa sana kuhusu sheria na kanuni. Kwa mantiki ya kuelewa sheria ni zile zinazotungwa na Bunge kwani ndio chombo cha kutunga sheria. Kanuni ni zile sheria ndogo ndogo zinazotugwa hata na Waziri/Mamlaka kwa nia ya kusaidia utekelezaji wa sheria kuu iliyotungwa na Bunge.

      Ni muhimu kuelewa hasa kuwa katika matumizi yake sheria haina tofauti na kanuni

      Karibu sana ndugu yetu

  4. parmena peter mpande
    parmena peter mpande says:

    nashukuru kwa ufafanuzi wako naombta kuuliza kwenye asasi za kiraia mathalani hutakiwa kuwa na katiba ya asasi,sheria ,kanuni na taratibu za asasi swali hapo inamaanisha nini kuhusu vipengere hivyo na je sheria ndani ya asasi hiyo itaitwa kwa jina gani nitashukuru kuelimishwa

Comments are closed.