Sheria Leo. Yajue makundi ya Sheria

Ndugu msomaji wa mtandao wetu wa ulizasheria karibu tena kwenye mfululizo wa mafunzo ya sheria, katika ukurasa wa Sheria Leo.  Asante kwa kuendelea kutufuatilia tunapotoa maarifa ya elimu ya kisheria. Lengo letu bado ni lile la kuhakikisha tunakujengea uwezo wa maarifa ya kisheria yatakayokusaidia kukabiliana na changamoto kadhaa kwenye eneo la sheria kila siku.

Leo ninakwenda kukushirikisha baadhi ya makundi ya sheria ili kukusaidia kitu cha kufanya na unapokabiliana na matatizo ya kisheria kwenye eneo lolote, karibu tufuatane pamoja kwenye shule hii.

Utangulizi

Watu wengi wamekuwa wanakumbwa na changamota nyingi linapokuja kutokea tatizo la kisheria linalomuhusu yeye au mtu wake wa karibu, mara nyingi wanashikwa na hamaki, wanashindwa kujua ni aina gani ya tatizo linalowakabili. Wanashindwa kutambua ikiwa changamoto hiyo itakuwa na matokeo gani isipotatuliwa, je inaweza kusababisha adhabu au kufungwa au inaweza kumalizika kwa mazungumzo tu. Katika shule hii ya leo tutakwenda kuangalia kwa ufupi makundi ya aina za sheria ili kumsaidia mtu kujua ni sheria gani anakabiliana nayo na hatua gani anapaswa kuchukua.

Pia katika makala zitakazofuata tutakwenda kuziangalia sheria kadhaa katika makundi haya ili kumsaidia mwananchi kujua aina ya sheria ambayo anahusika nayo kwa wakati huo. Karibu sana.

Makundi ya Sheria

Wasomi wa sheria kupitia tafiti na tafakari waliweza kugawanya sheria katika makundi mbali mbali kulingana na matumizi yake, mamlaka iliyozitunga, watu wanaobanwa nazo na athari au matokeo ya sheria hizo. Yafuatayo ni baadi ya makundi ya sheria.

  1. Sheria za Kimataifa na sheria za Kitaifa (International and Municipal laws)

 Sheria za kimataifa ni sheria ambazo zinatungwa na vyombo vya kimataifa na sheria hizo kuzingatiwa na zinawabana mataifa mbali mbali. Mfano wa sheria za kimataifa ni zile ambazo zinatungwa na Umoja wa Mataifa (United Nations).

Sheria za Kitaifa ni sheria zile zinazotungwa na kutumika kwenye taifa moja yaani sheria zinazotungwa na kutekelezwa ndani ya nchi moja. Mfano taifa la Tanzania lina chombo kinachohusika na utungaji wa sheria nacho ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

2. Sheria za Umma na Binafsi (Public and Private laws) 

 Sheria za umma ni zile ambazo zinatungwa kwa ajili ya kutumika kuratibu mahusiano baina ya serikali na jamii nzima ya eneo husika. Sheria hizi mara nyingi zinasimamiwa utekelezaji wake na Serikali. Mfano wa sheria za umma kama sheria ya Makosa ya Jinai.

Sheria binafsi ni aina ya sheria ambazo zinatungwa kwa nia ya kuratibu mahusiano baina ya watu wenyewe. Mfano sheria za mikataba, sheria za urithi, sheria ya ndoa n.k

Tofauti kati ya sheria za umma na binafsi ni endapo sheria inapovunjwa ikiwa ni ya umma Serikali inachukua hatua kuhakikisha sheria inaheshimiwa na kushitaki ili adhabu itolewe wakati kwenye sheria zinazoratibu mambo binafsi ikitokea imevunjwa, mhathirika wa uvunjifu ule wa sheria anachukua wajibu wa kutafuta haki yake ikiwa ni pamoja na kushitaki mahakamani.

3. Sheria za Madai na Jinai (Civil and Criminal laws)

 Sheria za madai ni aina ya kundi la sheria ambazo zikivunjwa aliyeathirika anaweza kufungua madai mahakamani na kupewa haki husika mara nyingi nafuu anayopata ni fidia au kurudishiwa haki aliyopoteza.

Sheria za jinai ni aina ya kundi la sheria ambazo zikivunjwa Serikali inachukua jukumu la kushitaki na mara nyingi nafuu yake ni faini na kifungo baada ya mtuhumiwa kutiwa hatiani.

Tofauti ya makundi haya ya sheria ni matokeo na mfumo wa mashitaka endapo sheria itavunjwa. Ikiwa ni sheria ya madai basi matokeo yake ni kupata fidia au kurudishiwa haki iliyopotea mfano kiwanja au mali fulani wakati  ikiwa sheria iliyovujwa ni ya jinai matokeo yake ni faini au kifungo endapo mshtakiwa atatiwa haitiani.

4. Sheria za Haki na Wajibu na Sheria za Mwenendo ( Substantive and Procedural laws)

 Sheria za Haki na wajibu ni aina ya kundi la sheria ambazo zinatungwa kuonesha haki na wajibu wa watu wanaohusika na sheria hiyo. Mfano wa sheria hizo ni sheria ya Mikataba, sheria ya Mahusiano Kazini, Sheria ya Ndoa, Sheria ya Makosa na Adhabu.

Sheria za mwenendo ni kundi la sheria ambazo zinaainisha namna ya kuhakikisha haki na wajibu vilivyoainishwa kwenye sheria zinavyotekelezwa. Mfano wa sheria hizi ni sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Madai. Hizi zinabainisha mchakato wa kisheria unaotakiwa kuchukuliwa ili haki au wajibu fulani utekelezwe. Hizi ndizo zinaratibu taratibu za Kimahakama.

Hitimisho

Ndugu msomaji wa darasa la Sheria Leo kama tulivyojifunza leo aina au makundi ya sheria ni vyema tukayafahamu ili kuweza kujua namna ya kukabiliana na changamoto za kisheria na kuchukua uamuzi stahiki kwenye mazingira husika.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili