Sheria Leo. Sheria za Kimataifa

Utangulizi

Karibu sana tena katika ukurasa huu wa sheria leo, ambapo tumekuwa tukijifunza mambo kadhaa ya sheria ambazo zinatawala katika maisha yetu ya kila siku. Kama tulivyoeleza kwenye makala ya utangulizi juu ya makundi ya sheria kwenye makala iliyopita. Karibu tuanze kujadili sheria hizi kwa kifupi tupate mwanga katika kila kundi kwa jinsi gani zinatuhusu katika maisha ya kila siku. Karibu sana.

Maana ya Sheria za Kimataifa

Sheria za kimataifa ni mkusanyiko wa kanuni, taratibu na tamaduni ambazo zinaratibu mahusiano ya kimataifa, na utendaji wa mashirika ya kimataifa, mahusiano yao,  mahusiano ya nchi na watu au kanuni baina ya watu ambao si raia wa nchi husika lakini wanahusishwa na masuala ya kimataifa. Pia zina maana ya kanuni zinazoratibu mahusiano ya kimataifa, maslahi na utatuzi wa migogoro na aina ya matumizi ya sheria mbali mbali.

Sheria za kimataifa zimejikita katika sheria za asili, sheria za utamaduni wa kimataifa na sheria za mikataba ya kimataifa.

Kama tunavyofahamu kuna chombo cha Umoja wa Mataifa (United Nations) ambacho kiliundwa na mataifa mara baada ya vita kuu ya dunia 1945. Moja ya malengo makubwa ya uwepo wa umoja wa Mataifa ni kuwa na namna ya kusaidia utatuzi wa migogoro na kuiepusha dunia kuingia katika vita kama zile zilizotangulia yaani ile ya 1914-1918 na 1939 – 1945. Hivyo katika uundaji wa chombo hiki cha kimataifa kilipewa mamlaka ya kutunga sheria na kutumia tamaduni za kimataifa ili kuboresha mahusiano baina ya mataifa duniani.

Sheria za kimataifa zimegawanyika katika makundi makuu mawili yaani sheria zile zinazohusu mataifa mengi mfano sheria zinazotokana na mikataba ya kimataifa inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa ua mashirika yake na sheria zile zinazohusu mataifa machache kwa mfano sheria zinazokubaliwa katika mabara au ukanda kama Umoja wa Afrika, Umoja wa nchi za Afrika Mashariki n.k.

Sheria za kimataifa kama tulivyoona katika tafsiri yake zinaratibu mahusiano ambayo yana asili ya kimataifa au maslahi ya kimataifa. Ndani ya sheria hizi kuna kanuni za namna ya mataifa kuhusiana, mashirika ya kimataifa ua makampuni ya kimatifa yanayofanya kazi katika mataifa mbali mbali yanavyoweka kuhusiana na nchi.

Pia katika sheria za kimataifa yapo makosa ya kijinai yanayotambuliwa kimataifa mfano uharamia, ugaidi, mauaji ya kimbari, usafirishaji wa binadamu na kutumikisha binadamu pasipo hiyari yao. Makosa kama haya yakibainika yanaweza kushtakiwa katika nchi yoyote ile duniani ambayo imeridhia mikataba ya kimataifa.

Hivyo ni muhimu sana kwako ndugu msomaji kufahamu uwepo wa sheria za kimataifa ambazo baadhi Tanzania kama nchi inawajibika kuzifuata na imeziridhia na kuzitekeleza. Mfano wa sheria hiyo ni tangazo la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa tangu 1948 ambalo limeingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1984.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili