Sheria Leo. Sheria za Kitaifa (Sheria za Ndani)

Utangulizi

Karibu sana kwa siku ya leo ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa wa Sheria Leo. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Tangu makala ya Sheria Leo.9 tumekuwa tukiangalia makundi ya Sheria na makala ya Sheria Leo.10 tulianza uchambuzi wa yale makundi kwa kuangalia Sheria za Kimataifa. Leo tunakuletea ufafanuzi juu ya sheria za Kitaifa au Sheria za ndani ya nchi. Karibu tujifunze pamoja

Maana ya Sheria za Kitaifa (Sheria za Ndani)

Ni mfumo wa kanuni, taratibu na mkusanyiko wa sheria zinazotumika katika nchi moja. Huu ni mkusanyiko wa sheria mbali mbali zinazotungwa na kutumika katika eneo la nchi moja. Tafsiri hii inatolewa kwa kutofautisha kati ya sheria za Kitaifa na Sheria za Kimataifa.

Mfumo wa sheria za Kitaifa katika utekelezaji unaundwa na vyombo vikuu vitatu vinavyojulikana kama Mihimili ya Dola ambavyo ni  Bunge, Mahakama na Serikali.

Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria ambazo zinatumika katika nchi, wakati Mahakama ni mhimili wa dola ambao unahusika na kutafsiri sheria zilizotungwa na Bunge. Hali kadhalika Serikali ni mhimili unaosimamia utekelezaji wa sheria.

Sheria hizi zinatungwa na Bunge zinahusu mambo ya Umma yaani yale yanayohusu jamii nzima mfano Katiba, sheria za utawala, sheria za jinai n.k. hali kadhalika Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu mambo binafsi, mfano wa sheria za mikataba, mirathi, na mali n.k.

Mipaka ya matumizi ya sheria hizi za Kitaifa ni eneo la kimamlaka kama inavyoainshwa katika Katiba ya nchi husika. Wanajamii na walio wageni wanawajibika kuzijua na kutii sheria hizi wakati wote. Uvunjifu au makosa yanayotokana na kutokutii sheria hizi yataamuliwa na Mahakama zilizopo kwa mujibu wa sheria.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwetu wananchi na wakaazi wa nchi ya Tanzania kuwa na ufahamu juu ya sheria zetu jinsi zinavyotungwa, kutafsiriwa na kusimamiwa na vyombo ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa Katiba ya JMT ili kujua namna ya kuchukua hatua endapo kutajitokeza jambo linalohitaji kutatuliwa la kisheria katika ngazi zote hizo ya utungaji, kutoa haki na kusimamia sheria.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili