Elimu ya Sheria: Uchambuzi wa Sheria

Utangulizi

Ndugu msomaji wa mtandao wa uliza sheria na mfuatiliaji wa makala kupitia ukurasa wa Elimu ya Sheria nakukaribisha tena katika ukurasa huu. Kwa muda sasa ukurasa huu hatukuweka makala kwa sababu tulikuwa tunaangalia aina ya mambo ya kisheria yanayostahili kufundishwa kupitia ukurasa huu.

Habari Njema kwako

Ndugu msomaji pamoja na kutoa elimu ya sheria kupitia ukurasa huu na ule wa Sheria Leo, tumegundua bado wasomaji wetu wana kiu ya kutaka kujua mambo ya ndani kabisa kwenye sheria kwani ni jambo linalowahusu wote. Hata hivyo taaluma hii ina changamoto kubwa jinsi ya Sheria zinavyotungwa hasa lugha inayotumika si rafiki wa watumiaji wa sheria.

Sheria nyingi ambazo zimetungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza hii ni changamoto kubwa sana kwa jamii yetu ambayo asilimia kubwa ni wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili. Uliza sheria imejipanga kuitatua changamoto hii kwa kuanza kufanya Uchambuzi wa sheria mbali mbali kupitia ukurasa wa Elimu ya Sheria.

Malengo ya ukurasa wa Elimu ya Sheria

  • Kukupa maarifa ya kisheria katika maeneo mbali mbali
  • Kufanya uchambuzi wa sheria mbali mbali kwa lugha inayoeleweka na mwananchi yaani lugha ya Kiswahili.
  • Kutoa ufafanuzi juu ya maeneo mbali mbali ya kisheria.

Ndugu msomaji kwa kuanza kutoa Elimu ya Kisheria tutaanza na Uchambuzi wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini yaani Sheria ya Kazi. Hii inawahusu watu wengi sana na utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi sana kwa waajiri na wafanyakazi.

Pia tunakupa nafasi ya kuendelea kutoa maoni yako ni sheria gani ungependa tukuletee katika uchambuzi wa sheria, nasi tutafanyia kazi maoni yako.

Tunakukaribisha sana ndugu yetu msomaji wa ukurasa wa Elimu ya Sheria tujifunze kwa pamoja kwa kuzifahamu sheria ambazo tunawajibika kuzitii kila siku.

Angalizo kwa Wasomaji wetu

Uliza sheria inatoa mchango wake kwa kuelimisha jamii juu ya elimu ya Sheria, uchambuzi wowote utakaofanyika katika ukurasa huu ni kwa lengo la kuelimisha. Uliza sheria itajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kufanya uchambuzi kwa weledi wote. Hata hivyo ifahamike kuwa sheria hizi zinaweza kufanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara hivyo isichukuliwe na wasomaji juu ya kile kilichosemwa ndivyo kilivyo wakati wote, bali yanaweza kutokea mabadiliko ya kisheria. Hivyo ni muhumu kwa wasomaji kuendelea kufuatilia tafsiri sahihi na matumizi sahihi ya sheria kwa wakati husika. Uliza sheria haitawajibika kwa namna yoyote ile ikiwa mtu ametumia tafsiri au mafundisho haya kinyume na malengo yaliyoanishwa katika mtandao huu.

Ni vyema kwako msomaji kabla ya kuchukua hatua zaidi za kisheria kutokana na elimu uliyopata kwenye mtandao huu, kupata ushauri wa kisheria zaidi kutoka kwa Wataalam wa Sheria (Mawakili) ili wakushauri kulingana na hitaji/changamoto yako ya wakati husika na kuepuka madhara yoyote ya kisheria. Karibu sana.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Hamisi Juma
    Hamisi Juma says:

    Asante sana KWA kutuelimisha juu ya sheria Na umuhimu wake katika maisha yetu ya kila siku,naomba kuuliza swali ,sheria inasemaje KWA mfanyakazi alive umia kazini Na hatuagani anazo weza kuchukua ili kuweza kupata haki take(malipo ya kuumia)?Na je kama mwajiri amemfukuza mfanyakazi wake ni hata gani anastahili kuchukua mfanyakazi dhidi ya mwajiri wake?

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Asante sana Hamisi Juma kwa maswali mazuri nitaanza kujibu swali la pili kuhusu hatua anazopaswa mfanyakazi kuchukua endapo amefukuzwa kazi. Kwa ufupi Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004 inaeleza kuwa mwajiri haruhusiwi kusitisha ajira (kumfukuza kazi) ya mfanyakazi pasipokuwa na sababu za msingi na kufuata utaratibu wa haki. Hivyo mfanyakazi akiona amefukuzwa kazi pasipo mambo hayo mawili kuzingatiwa, anapaswa kufungua mgogoro wa kazi (kesi) kupinga uamuzi huo wa mwajiri ndani ya siku 30 tangu kupewa taarifa ya kuachishwa kazi. Sehemu ambayo mgogoro huo unafunguliwa ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation and Arbitratation) kwa kujaza Fomu maalum ya kufungua mgogoro, na Tume itasikiliza na kuamua hatma ya mfanyakazi endapo usitishaji wa ajira ulikuwa halali au la.

      Swali kuhusu hatua za kuchukua endapo mfanyakazi ameumia, kwa sasa kuna sheria mpya ya Fidia ya Wafanyakazi (The Workman’s Compensation Act) na umeanzishwa mfuko wa Fidia ya wafanyakazi ambao Waajiri wanawajibika kuchangia kwenye mfuko huo. Nitakuletea utaratibu kutokana na sheria mpya hivi karibuni.

      Ndugu yangu Hamisi Juma,nakukaribisha pia kuanza kufuatilia katika Ukurasa wa Elimu ya Sheria: Uchambuzi wa Sheria ambapo tumeanza kuchambua Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004. Naamini utajifunza mengi na kujibu maswali yako na ya wasomaji wengine.

      Karibu sana

Comments are closed.