Ijue Sheria ya Kanuni ya Adhabu


Utangulizi 

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Tumeanza mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Tayari tumekamilisha kundi la kwanza la sheria za madai, sasa tunaanza kujadili sheria za Jinai kwenye kundi la pili la sheria 5. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Karibu tujifunze.

Msingi wa sheria ya Kanuni ya Adhabu

Ndugu msomaji Sheria ya Kanuni ya Adhabu ni kati ya sheria kongwe tangu wanadamu wameanza kuishi katika jamii iliyo chini ya mamlaka. Sheria hii inahusisha mjumuisho wa makosa mbali mbali ya kijinai. Kama ilivyo lengo la sheria ni kuhakikisha watu wanaishi na kutenda matendo yao kwa mujibu wa sheria ili kutunza matakwa mapana ya jamii.

Msingi wa sheria hii ni hali ya wanadamu kuwa na utashi huru yaani kila mtu anaweza kutenda anavyoamua. Kutokuwepo kwa sheria inayotambua makosa ya Jinai ambayo Jamhuri ina wajibu wa kulinda wanajamii wenye nia njema kutafanya taifa liliweze kutawalika. Pata picha kama kungekuwa hakuna sheria inayokataza kuiba, kuua, kubaka, kula rushwa, n.k je, jamii yetu ingekuwa ya namna gani. Ni dhahiri kuwa jamii isingekuwa na utulivu na maendeleo yo yote.

Hivyo Sheria ya Kanuni ya Adhabu imekuja kwa lengo la kuainisha makosa mbali mbali ya kijinai na adhabu stahiki kwa makosa hayo, ili jamii iweze kujua na kuchukua taadhari juu ya matendo yao ya kila siku.

Maana ya Sheria

Sheria hii ya Kanuni ya Adhabu ni sheria inayoainisha kanuni mbali mbali na makosa ambayo hayapaswi kufanywa na mwanajamii yeyote. Aidha sheria hii inaainisha adhabu juu ya makosa husika. Sheria hii inaainisha makosa mbali mbali ya jinai na adhabu zake.

Zipo sheria nyingi ambazo ndani yake yapo makosa ya jinai, hata hivyo Bunge lilitunga sheria maalum ambayo imeainisha makosa ya kijinai na adhabu zake. Hii ni sheria mama ya makosa ya jinai.

Makosa ya kijinai yameainishwa katika sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code) Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.

Aina ya Makosa katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu

Katika sheria hii yapo makosa mengi yameainishwa na adhabu zake. Hata hivyo makosa hayo yameainishwa kwa mafungu mbalimbali  kama ifuatavyo;

  • Makosa ya kuvunja Utulivu
  • Makosa ya Uhaini
  • Makosa yanayoingilia Dola za Kigeni (Kuvunja Utulivu nchi za Nje)
  • Mikusanyiko isiyo halali na ghasia, kuvunja utulivu wa watu wengine
  • Makosa juu ya Usimamiaji wa Mamlaka Halali
  • Matumizi mabaya ya madaraka
  • Makosa yahusuyo usimamiaji wa haki
  • Makosa ya Kuzuia utendaji wa Maafisa wa Mahakama.
  • Makosa yanayodhuru watu kwa Ujumla
  • Makosa yanayohusu dini
  • Makosa kinyume na utu
  • Makosa yanayohusu ndoa
  • Makosa juu ya Mtu
  • Makosa ya kuua
  • Makosa ya kuhatarisha maisha au afya
  • Makosa juu ya Mali
  • Makosa ya wizi
  • Uvunjaji wa nyumba usiku na uvunjaji wa nyumba mchana
  • Kupokea mali iliyoibiwa

Sheria ya Kanuni ya Adhabu ina makosa mengi sana haya yaliyoainishwa ni baadhi tu ya aina za makosa ambayo yanapatikana katika sheria hii.

Hitimisho

Sheria hii ni ya umma yaani makosa yanayofanyika katika sheria yatailazimisha Jamhuri kumchukulia hatua mtu yeyote atakayetenda makosa yaliyoainishwa ikiwa ni pamoja na kumfungulia mashitaka katika mahakama husika na uwezekano wa kupata adhabu ya kifungo, au kunyongwa au faini. Ni muhimu sana wanajamii kufahamu makosa mbali mbali yanayoainishwa katika sheria hii ili kuepuka kuingia hatiani.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili