Ijue Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Tumeanza mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Tayari tumekamilisha kundi la kwanza la sheria za madai, sasa tunaanza kujadili sheria za Jinai kwenye kundi la pili la sheria 5. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Karibu tujifunze.

Msingi wa sheria

Rushwa imekuwa tatizo kwa jamii nyingi tangu enzi na enzi. Katika mfumo wa utafutaji haki kwenye maeneo mbali mbali rushwa imekuwa tatizo sugu sana. Rushwa imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya taifa lolote katika Nyanja za kidemokrasia, utawala bora na upatikanaji wa haki katika maeneo mbali mbali ya maamuzi. Rushwa imekuwa tishio la amani na utulivu wa jamii nzima. Hivyobasi kwa msingi huu sheria maalum inayohusiana na makosa ya rushwa ilipaswa kuanzishwa ili kusaidia mapambano dhidi ya rushwa.

Sheria inayohusika na masuala ya rushwa inaitwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya 2007 hii ilikuja kutungwa na Bunge baada ya Sheria iliyokuwepo awali kuonekana haiwezi kukidhi mahitaji na changamoto za kukabiliana na masuala ya rushwa katika maendeleo haya.

Maana ya Rushwa

Rushwa ina maana mbali mbali kama kutenda au kutokutenda jambo kwa misingi ya kupokea maslahi fulani.

Aidha rushwa inatafsiriwa kama hali ya mtu kutenda au kutokutenda jambo fulani kwa mtu au kikundi cha watu kwa nia ya kujipatia faida binafsi, baada ya kupatiwa au kuhaidiwa kupatiwa kiasi fulani cha fedha au vitu vinginevyo, kinyume cha matakwa  au misingi ya kazi. (Jarida: Yajue Makosa ya Rushwa, uk.5, NOLA, 2007)

Aghalabu mtoa rushwa hupaswa kuwa na mamlaka fulani, ama katika utumishi wa umma au utumishi katika kampuni au taasisi fulani. Rushwa pia huweza kujitokeza pale mpokea rushwa au mtoa rushwa anafanya hivyo kwa maslahi binafi, maslahi ya mtu fulani au kikundi cha watu fulani kinyume cha utaratibu uliowekwa. (Jarida: Yajue Makosa ya Rushwa, uk.5, NOLA, 2007)

Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)

Sheria hii ya rushwa ya 2007 imeanzisha chombo maalum chenye mamlaka ya kutekeleza sheria yaani Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Taasisi hii inaongozwa na Mkurugenzi ambaye anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taasisi hii ina majukumu kadhaa kama;

  • Kuchunguza na kupeleleza juu ya tuhuma mbali mbali za rushwa
  • Kuendesha mashitaka ya rushwa dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya rushwa.
  • Kupokea malalamiko na kuchunguza malalamiko yanayohusiana na makosa ya rushwa.

Aina ya makosa

Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imeanisha makosa kadhaa ya rushwa ambapo mtu akitenda basi mchakato wa uchunguzi na mashitaka ya rushwa utaendeshwa dhidi yake. Kwa ujumla sheria hii imeanisha makosa 14 ya rushwa yanayojitokeza kwa taswira mbali mbali. Mfano wa makosa ya rushwa ni kama ifuatavyo;

  • Kupokea rushwa, kushawishi au kulazimisha kupewa rushwa, kutoa rushwa au kuhaidi kutoa rushwa. Adhabu ni faini ya Tsh.500,000 – 1,000,000 au kifungo kati ya miaka 3 -5 au faini na kifungo kwa pamoja.
  • Kutoa au kupokea rushwa kwa ajili ya kupata mkataba wa kutoa huduma kwa idara ya umma au shirika la umma. Adhabu ni faini ni Tsh.1,000,000 – 3,000,000 au kifungo kati ya miaka 3 -5 au faini na kifungo kwa pamoja.
  • Rushwa ya ngono ambapo mtu mwenye mamlaka anatumia madakara kulazimisha au kushawishi mtu mwengine kufanya naye tendo la ngono kwa ahadi ya kumpatia ajira au upendeleo fulani. Adhabu ni faini Tsh.5,000,000 au kifungo kisichozidi miaka 3 au vyote kwa pamoja.

 

Hitimisho

Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ni kati ya sheria muhimu sana katika kupambana na makosa ya jinai, zinatakiwa kuchukua hatua kali sana dhidi ya watu wanaojihusisha na rushwa. Ugumu wa mapambano ya rushwa ni kwa sababu yanahusisha pande mbili yaani mtoa rushwa na mpokea rushwa hii inafanya upatikanaji wa taarifa ya matendo ya rushwa kuwa ngumu sana. Ni muhimu kwa wananchi kutambua kuwa wana haki ya kuhudumiwa kwa usawa na haki katika maeneo wanayopaswa kuhudumiwa, wachukue wajibu wa kutoa taarifa kwa vyombo husika ili hatua zichukuliwe kwa wakati. Sikuzote lazima tujue ‘Rushwa ni Adui wa Haki’ hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake na kulinda haki.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili