5.Mikataba ya Ajira

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ya Kazi nashukuru tumeendelea  kuwa pamoja na kupata maarifa haya ambayo yanaletwa kwako kupitia www.ulizasheria.co.tz. Katika mfululizo wa makala hizi tutakwenda kuona jinsi sheria ya kazi ilivyoweka viwango ambavyo mwajiri anawajibika kuvizingatia mara anapomwajiri mfanyakazi katika ajira watakayokubaliana. Sheria ya kazi imeainisha maeneo kadhaa ambayo yamewekewa viwango vya ajira. Hii ina maana mwajiri analazimishwa na sheria kuzingatia viwango hivyo na endapo atakiuka basi itahesabika amekiuka sheria ya Kazi.

Leo katika makala ya mfululizo juu ya Viwango vya Ajira tunakwenda kuangalia suala la Mikataba ya Ajira.

Ndugu msomaji pamekuwa na kilio kikubwa sana kwa wafanyakazi wengi wa kada mbali mbali juu ya kufanya kazi pasipo mikataba ya ajira. Wengi wanakuja kushtuka mara baada ya kuachishwa kazi ndipo wanaanza kulalamika. Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza juu ya umuhimu wa mikataba ya ajira na namna sheria ya kazi inavyoainisha aina za mikataba ya ajira ambayo mwajiri na mfanyakazi wanaweza kuingia. Fuatana nami ili kuendelea kujifunza.

Maana ya Mkataba

Mkataba ni makubaliano baina ya pande mbele ambayo yana nguvu ya kisheria kwa kuwabana kila mmoja kutekeleza wajibu na kupata haki anazostahili kwa mujibu wa mkataba.

Nieleze mapema kuwa sheria ya kazi ni aina moja wapo ya zao la sheria ya Mikataba. Yaani mahusiano kati ya mwajiri na mfanyakazi yanajengwa katika sheria ya mikataba. Hivyo ulewa sahihi wa sheria ya mikataba unaweza kukusaidia ndugu msomaji kufahamu msingi wa sheria ya kazi.

Kama nilivyoeleza hapo juu inaonesha msingi wa mahusiano baina ya mwajiri na mfanyakazi ni mkataba. Mkataba wa ajira unaweza kuwa wa mdomo au maandishi. Ni vyema mwajiri na mfanyakazi kuwa na mkataba wa maandishi hii itasaidia pande zote kufahamu haki na wajibu wao.

Maelezo ya Maandishi kwa ajira yenye mkataba wa mdomo

Sheria ya kazi imeweka utaratibu wa mwajiri kumpatia maelezo ya maandishi mfanyakazi mara baada ya kuanza kazi pale ambapo mfanyakazi hajapewa mkataba wa maandishi. Mara nyingi masharti haya yanaainishwa ndani ya mkataba wa ajira.

Maelezo ambayo mwajiri anayopaswa kumpatia mfanyakazi ni kama ifuatavyo:

  • Jina, umri, anwani ya kudumu na jinsi ya mfanyakazi
  • Mahali alipoajiriwa
  • Maelezo ya kazi
  • Tarehe ya kuanza kazi
  • Aina ya kazi na muda wa mkataba
  • Sehemu ya kazi
  • Saa za kazi
  • Ujira, njia ya ukokotoaji wake na maelezo ya kina kuhusu mafao yoyote au malipo ya kitu/mali; na
  • Mambo mengineyo ya muhimu mfanyakazi kuyajua

Mwajiri anawajibika kumweleza mfanyakazi katika lugha atakayoelewa juu ya mambo haya muhimu na ikiwa maelezo haya yanabadilika ni lazima mwajiri ashauriane na mfanyakazi na mabadiliko yafanyike kwa maandishi.

Aina za Mikataba ya Kazi kwa mujibu wa sheria ya Kazi

Sheria ya Kazi imegawa mikataba katika aina kuu tatu ambazo mwajiri na mfanyakazi wanaweza kuingia katika kazi husika.

  • Mkataba usio na muda maalum

Mkataba huu usio wa muda maalum ni aina ya mkataba ambao ukomo wa ajira haujatajwa wazi wazi. Katika aina hii ya mkataba mfanyakazi anaweza kuendelea kufanya kazi mpaka kufikia umri wa kustaafu endapo haitatokea sababu yoyote ya kusitisha ajira kabla ya umri huo wa kustaafu. Kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umri wa kustaafu ni miaka 55 kwa hiyari na 60 kwa lazima.

 

  • Mkataba wa muda maalum

Huu ni aina ya mkataba ambao kipindi cha ajira kimewekwa wazi wazi na tarehe ya ukomo wa ajira ipo wazi na inajulikana. Sheria ya kazi inaeleza juu ya aina hii ya mkataba itawahusu wafanyakazi wa kada ya uongozi na weledi.

 

  • Mkataba wa kazi maalum

Hii ni aina ya mkataba wa muda maalum ambapo kigezo cha mkataba kumalizika ni kukamilika kwa kazi na mara nyingi malipo hufanyika kwa siku au baada ya kumalizika kazi husika.

 

Hitimisho

Katika mahusiano ya ajira ni muhimu sana kwa pande zote kuhakikisha kuna mkataba wa maandishi. Hii itasaidia kutambua haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa. Mkataba si kwa ajili ya kuonesha maslahi ya mfanyakazi tu bali mkataba unamsaidia mwajiri pia kwani utaeleza mipaka na miongozo ambayo inapaswa kuzingatiwa na mfanyakazi, ambapo ikikiukwa mwajiri anaweza kuchukua hatua stahiki dhidi ya mfanyakazi.

Usikose kufuatilia tena uchambuzi juu ya sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini kwa wafanyakazi wasio na mikataba maalum.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

 

2 replies

Comments are closed.