Ijue Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala  ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Tumeanza mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Tayari tumekamilisha kundi la kwanza la sheria za madai, sasa tunaanza kujadili sheria za Jinai kwenye kundi la pili la sheria 5. Katika kundi la pili la sheria za Jinai tumeshaangalia Sheria ya Kanuni ya Adhabu na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu. Karibu tujifunze.

Msingi wa sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu

Msingi wa kuwepo sheria hii ni kutokana na ongezeko la kiwango kikubwa cha uhalifu ambao unahusisha mali zenye thamani kubwa na viwango vikubwa vya fedha. Kama tunavyofahamu maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia urahisi wa kusafirisha fedha au kuhamisha fedha kutoka mahali kwenda mahali kwengine. Shughuli za wanadamu, serikali na taasisi binafsi zimekuwa zikijihusisha katika miradi mikubwa ya maendeleo au uchimbaji wa rasilimali kwenye ardhi kama madini na gesi asilia au miradi ya ujenzi ya miundombinu na masuala ya umeme. Maeneo haya yote yanahitaji kuwango kikubwa cha fedha. Hapa ndipo watumishi au wawekezaji wasio waaminifu wanatoa na kupokea rushwa ili kufanya maamuzi fulani ya kupendelea. Rushwa hizi ni za kiwango kikubwa cha fedha au maslahi kwenye mali fulani au mradi.

Wanaopata fedha hizi kupitia njia haramu kama nilivyoainisha hapo juu hutafuta njia kadhaa za kuzifanya fedha au mali zao kuonekana kuwa ni halali. Hivyo serikali nyingi zimeanzisha mfumo wa sheria wa kuweza kuzuia Utakatishaji wa fedha/Mali haramu.

Maana ya Utakatishaji Fedha

Maana ya utakatishaji fedha ni namna ya kujipatia fedha haramu yaani zimepatikana kutokana na shughuli isiyo halali kisheria na kutafuta njia mbali mbali kuziwezesha fedha hizo zionekane kuwa ni halali. Mfano mtu anapata kiwango kikubwa cha fedha za rushwa, anaamua kuziwekeza kwa kununua hisa, au kujenga majengo au kuziingiza kwenye uwekezaji wowote wa kibiashara au viwanda n.k. katika macho ya kawaida mnadhani uwekezaji wake ni halali lakini chanzo cha fedha hizo ni haramu.

Masuala ya kuzuia na kupambana na utakatishaji wa fedha yanaongozwa na Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu ya mwaka 2006 Sura ya 423.

 

 

Taasisi za Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu

Sheria imeunda vyombo vikuu 2 kwa lengo la kutekeleza majukumu ya Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu

  1. Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu

Hiki ni kitengo maalumu katika Wizara ya Fedha kitachojulikana kama Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu (FIU)

Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu kitakuwa na kazi ya kupokea kuchanganua na kusambaza taarifa zote za miamala yenye mashaka na taarifa muhimu zinazohusiana na utakatishaji wa fedha haramu au taarifa za ufadhili wa ugaidi zilizotelewa na mtoa taarifa au vyanzo vingine ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kitengo kitaongozwa na Kamishna  mwenye elimu ya kutosha na uzoefu katika uchumi, masuala ya fedha, usimamizi wa fedha, sheria, makosa ya jinai ya kuichumi au eneo lolote lenye tija katika utekelezaji majukumu kulingana na sheria hii, kama Kamishina wa Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu

  1. Kamati ya Taifa

Kamati hii ya Taifa itaundwa kwa lengo la kudhibiti biashara ya fedha haramu ambayo itajumuisha wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na wajumbe wengine watateuliwa kuwa kwenye kamati kutokana na nyadhifa zao.

 

Makosa yahusuyo Utakatishaji wa Fedha Haramu

Sheria imeanisha baadhi ya makosa ambayo yakitendeka na mtu au taasisi na kudhibitishwa mahakamani basi itachukuliwa wametenda kosa la Utakatishaji wa fedha haramu. Mfano wa makosa hayo;

  • Mtu yeyote atakaye jihusisha, moja kwa moja au kwa njia nyingine katika muamala unaohusisha mali itokanayo na ya mapato ya fedha haramu akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu mali hiyo ni ya mapato yatokanayo na makosa ya uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu;
  • Mtu yeyote atakaye badili,hamisha,safirisha, pitisha mali ikiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo ni ya mapato yatokanayo na uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu, kwa malengo la kuficha, kupoteza ukweli au chanzo halisi cha mali hiyo kuwa ni haramu au kumpa msaada mtu yeyote aliye husika katika kufanya kitendo hicho kwa lengo la kukwepa madhara ya kisheria;
  • Mtu yeyote atakaye ficha, funika ukweli, zuia upatikanaji wa ukweli, chanzo,mahali,Uhamishaji wa umiliki, mzunguko, au umiliki wa au haki kuhusiana na mali hiyo, akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo imepatikana kwa mapato yatokanayo na fedha haramu
  • Mtu yeyote atakaye jipatia, miliki, tumia au simamia mali, ikiwa anafahamu, au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu wa kupokea mali hiyo kuwa mali hiyo imetokana na makosa ya uhalifu amabyo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu; au
  • Mtu yeyote atakaye shiriki katika, jihusisha na, kula njama ya kutenda, jaribu kutenda, saidia au shiriki au wezesha na shauri utendwaji wa jambo lolote lililoelezwa katika aya (a) hadi (d) ya kifungu hiki atakuwa amefanya kosa la kutakatisha fedha haramu.

Adhabu za makosa ya Utakatishaji wa Fedha Haramu zinaanzia kiasi cha faini ya Tsh.100,000,000/- (Milioni Mia Moja) mpaka 1,000,000,000/- (Bilioni Moja). Hata hivyo itategemea na kiasi cha mali au fedha iliyotakatishwa.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwa wananchi kuwa na ufahamu na uelewa wa sheria hii ili kusaidia kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika. Watu wengi na mashirika mengi yamekuwa si waaminifu katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kujipatia fedha haramu. Tujifunze kutekeleza shughuli zetu kwa uaminifu na ziwe shughuli halali unaweza kudhani hutabainika kwa muda lakini siku ukibainika ni hasara kubwa na mahakama ina mamlaka ya kutaifisha fedha na mali ambazo umezipata kwa njia isiyo halali.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili