Ijue Sheria ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Tumeanza mfululizo wa makala 10 za utabulisho wa baadhi ya sheria ambazo zina matumizi ya kila siku kwa mwananchi. Tayari tumekamilisha kundi la kwanza la sheria za madai, sasa tunaanza kujadili sheria za Jinai kwenye kundi la pili la sheria 5. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Kuzuia Udhibiti wa Madawa ya Kulevya. Karibu tujifunze.

Msingi wa sheria ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya

Msingi wa kuwepo sheria hii ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya ni kutokana na ongezeko kubwa la matumizi ya madawa haya duniani na kupoteza nguvu kubwa ya vijana ambao walipaswa kuwa wazalishaji. Huduma za usafiri na sayansi na teknolojia vimechangia biashara haramu ya madawa ya kulevya kushamiri kila mahali. Biashara hii si tishio kwa Taifa letu bali kwa ulimwengu mzima. Biashara hii imeleta hasara kubwa kwa watu wengi kupoteza maisha, kupoteza uwezo wa kufanya kazi, na kupata maradhi ambayo ni vigumu kupata matibabu. Serikali nyingi duniani zimeanzisha Sheria, taratibu na sera mbali mbali kudhibiti biashara haramu ya madawa ya kulevya. Tanzania ni moja wapo wa nchi ambazo zimekumbwa na tatizo hili hivyo kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitunga sheria ya Udhibiti wa madawa ya Kulevya.

Maana ya Madawa ya Kulevya

Dawa kwa kawaida ni kitu anachopewa mtu kwa nia ya kuhuisha afya yake yaani ni tiba kutokana na ugonjwa fulani. Kwa kawaida dawa ni kitu kizuri kinalenga kulinda maisha ya mwanadamu. Dawa huwa zinatolewa na wataalam yaani Madaktari baada ya kufanya vipimo maalum juu ya tatizo linalomkabili mtu.

Dawa za kulevya ni matumizi mabaya ya dawa kwa lengo la kumlewesha mtu na kumsababishia utegemezi (uteja) wa dawa hizo katika maisha yake ya kila siku. Dawa hizi mara nyingi zinatengenezwa na wahalifu kwa nia ya kufanya biashara haramu. Matumizi au biashara ya dawa za kulevya ni kinyume cha sheria.

Masuala ya udhibiti wa Madawa ya Kulevya yanaongozwa na Sheria ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya ya mwaka 2015, Sheria hii ilitungwa na Bunge kuchukua nafasi ya Sheria ya awali Sheria ya Madawa na Uzuiaji wa Usafirishaji wa Madawa Haramu Sura 95, ambayo ilionekana na mapungufu na kupitwa na wakati.

 

 Taasisi za Udhibiti wa madawa ya Kulevya

Sheria imeunda vyombo vikuu 2 kwa lengo la kuzuia na kudhibiti uzalishaji, matumizi na biashara ya madawa ya kulevya

  1. Mamlaka ya Udhibiti wa madawa ya Kulevya

Hii ni mamlaka iliyonzishwa na Sheria ya udhibiti wa Madawa ya Kulevya na inaongozwa na Kamishna wa Madawa ya Kulevya anayeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majukumu ya Mamlaka hii ni kubuni na kuendesha mbinu mbali mbali zitakazowezesha udhibiti wa kuzalisha, matumizi na usafirishaji wa madawa ya kulevya. Katika kutekeleza majukumu yake mamlaka hii itazingatia sheria za kimataifa zinazohusu udhibiti wa madawa ya kulevya, sheria mbali mbali za Tanzania, sera na miongozo ya Taifa juu ya udhibiti wa madawa ya kulevya. Mamlaka hii ndiyo inayoratibu shughuli zote za mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Dola.

  1. Baraza la Taifa la Udhibiti wa Madawa ya Kulevya

Sheria hii pia inaunda chombo kingine ambacho ni Baraza la Taifa la Udhibiti wa Madawa ya Kulevya. Mwenyekiti wa Baraza ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wajumbe wengine ni mawaziri wa Tanzania Bara na Zanzibar wanaohusika na wizara ya Katiba na Sheria, Waziri Mambo ya Ndani, Waziri wa Afya, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Vijana na waziri wa mambo ya elimu na wizara zote ambazo kwa njia moja ama nyingine zinahusika na utatuzi wa tatizo la madawa ya kulevya.

Majukumu makubwa ya Baraza hili ni kuangalia na kutathmini utendaji kulingana na Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya.

 

Makosa yaliyoainishwa na Sheria

Sheria hii imeainisha makosa mengi zaidi kuliko sheria ya awali hivyo na adhabu zimeongezeka makali yake tofauti na awali. Katika makala hii tutaangalia baadhi ya makosa na adhabu zinazotolewa kwa wakosaji kwa sheria hii. Ikumbukwe kuwa makosa yatokanayo na Sheria hii ni makosa ya kijinai ambapo Jamhuri ina wajibu wa kuchunguza na kuwashitaki waalifu.

Mambo ya msingi yaliyoainishwa na sheria hii katika masuala ya makosa na adhabu

  • Mtu ayelima au kumiliki mbegu zinazoweza kutengeneza dawa za kulevya, au anayesambaza mimea ambayo imepigwa marufuku (mfano Bangi) endapo akipatikana na hatia anaweza kufungwa hadi kifungo cha miaka 30.
  • Mtu yeyote atakayehusika na usafirishaji wa madawa ya kulevya endapo atapatikana na hatia anatufungwa kifungo cha Maisha.
  • Mtu yeyote atakayekutwa na mtambo au mitambo ya kuzalisha madawa ya kulevya endapo atapatikana na hatia atafungwa kifungo cha maisha na kulipa faini isiyopungua Milioni 200.
  • Mtu yeyote atakayekutwa akivuta au kutumia madawa ya kulevya kwa kunusa au kujidunga endepo atakutwa na hatia atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 3 na faini isiyopungua Milioni 1.

Haya ni baadhi tu ya makosa na adhabu zinazoanishwa katika Sheria hii ya udhibiti wa Madawa ya Kulevya. Hii ni sheria kali sana ambapo ikitekelezwa ipasavyo itatuma ujumbe mzito kwa wahalifu na wote wanaojihusisha na uzalishaji, matumizi na biashara haramu.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwako mwananchi kuifahamu sheria hii ili kujiepusha na ushawishi wa uzalishaji, au matumizi au biashara hii haramu. Muhimu kwako kufahamu madawa ya kulevya ni janga kubwa linalopoteza nguvu kazi ya Taifa ambayo ni vijana. Wengi wameingia huko wamepoteza dira na maono juu ya maisha na sasa wamekuwa mzigo kwa jamii yetu. Tusaidie wote kujitoa katika janga hili kwa kupinga uzalishaji, matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya ili kujenga Taifa la watu makini wanaofuata sheria na kufanya kazi kwa juhudi na vipawa tulivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili