1.Ijue Sheria ya Usalama Barabarani

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Hivi karibuni tumekuwa na mfululizo wa makala za makundi ya sheria. Leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Usalama Barabarani. Karibu tujifunze.

Msingi wa sheria ya Usalama Barabarani

Msingi wa kuwepo sheria hii ya Usalama Barabarani ni kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na usafiri ambao binadamu ameubuni kurahisisha utendaji kazi. Katika miji mikubwa kwa sasa vipo vyombo vingi vya usafiri ikiwa ni wa anga, majini au kwenye ardhi. Matumizi makubwa ya usafiri yapo kwenye ardhi yaani matumizi ya barabara. Serikali nyingi zimewekeza katika ujenzi wa miundombinu ili kila mahali katika nchi paweze kufikika kwa urahisi. Ujenzi huu umeibua changamoto kubwa ya ongezeko la vyombo vya usafiri barabarani na watumiaji wa barabara kuwa wengi. Ongezeko la vyombo na watumiaji kumeibua tatizo la ajali barabarani na matumizi mabaya ya barabara ambayo yanasababisha hasara kwa Taifa kwa kupoteza nguvu kazi.

Hivyo basi Sheria inayohusu matumizi ya barabara ililazimika kutungwa na Bunge ili kusaidia udhibiti wa matumizi ya barabara na kuepusha makosa yanoweza kufanyika na watumiaji wa barabara.

Maana ya Sheria ya Usalama Barabarani

Sheria ya Usalama barabarani ni kanuni na taratibu ambazo zimewekwa kwa ajili ya watumiaji wa barabara ili kufanya matumizi ya barabara kuwa ya tija na manufaa. Sheria hizi zimewekwa kuepusha makosa ambayo yatasababisha hasara ya miundombinu na hasara juu ya maisha ya watu na mali zao wanapotumia barabara.

Masuala ya usalama barabarani yanaongozwa na na Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya  168.

Taasisi za Kusimamia Usalama Barabarani

Sheria imeunda vyombo vikuu 2 kwa lengo la kuratibu na kusimamia shughuli zote za Usalama barabarani.

  1. Msajili wa Vyombo vya Moto

Sheria inatamka kuwa kutakuwa na Msajili wa vyombo vya moto ambaye atateuliwa na Waziri anayehusika na masuala ya fedha. Msajili huyo atahusika na usajili wa vyombo vyote vya moto na kutoa leseni za udereva kwa watakaokidhi vigezo vya kuendesha vyombo vya moto. Kwa sasa jukumu hili linafanywa na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) wao ndio chombo kinachohusika na usajili wa vyombo vya moto na utoaji wa leseni.

  1. Baraza la Taifa la Usalama wa barabarani

Baraza la Taifa la Usalama barabarani litaongozwa na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na wajumbe wasiopungua 10 wanaoteuliwa na waziri anayehusika na masuala ya usalama barabarani.  Kazi kubwa ya Baraza ni kutoa mwongozo juu ya kuongeza maarifa na njia mbali mbali zitakazoweza kuimarisha hali ya usalama barabarani. Pia Baraza lina jukumu la kuchunguza vyanzo vya ajali na kushauri njia bora ya kuepuka athari hizo.

 

Makosa yaliyoainishwa na Sheria

Sheria hii imeanisha makosa mengi yanayoweza kutendeka Barabarani. Wasimamizi wa utekelezaji wa Sheria hii ni kikosi maalum cha Jeshi la Polisi- Trafiki. Kikosi hiki kimepewa wajibu wa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama Barabarani

Baadhi ya makosa yaliyoanishwa kwenye Sheria ya Usalama Barabarani;

  • Kuendesha gari au chombo cha moto ambacho hakijasaliwa na Mamlaka husika
  • Kushindwa kutembea kwenye chombo cha moto na hati ya usajili wa chombo hicho
  • Kutumia chombo cha moto kwa ajili ya kufundishia pasipo kufanyiwa usajili na kutambuliwa kama ni chombo kwa ajili ya mafunzo (kuweka alama ya ‘Learner’)
  • Kushindwa kusimama kwenye kivuko cha reli
  • Kuendesha gari taratibu sana pasipo sababu yoyote ya msingi. n.k

Haya ni baadhi ya makosa yanayoainishwa na Sheria ya Usalama Barabarani, yapo makosa mengi ambayo tunakutana nayo kila siku.

Makosa haya mara nyingi yanaadhibiwa kwa utozaji wa faini, kiwango cha chini cha faini kwa kosa moja ni Tsh.30,000/- viwango hivi vimekuwa vikiongezeka kutokana na matumizi mabovu ya barabara na uwezo wa wakosaji kulipa. Hata hivyo yapo makosa ambayo ni lazima mkosaji afikishwe mahakamani. Mfano kusababisha ajali ya vyombo au kugongwa kwa mtu.

Hitimisho

Ni muhimu sana kwako mwananchi kuijua sheria hii na kuzingatia kufuata sheria za bararani na alama kama zilivyoainishwa barabarani kwa lengo la kulinda maisha yako na watumiaji wengine wa barabara. Eneo ambalo limekuwa likisababisha vilio kila kukicha ni ajali za barabarani ambazo kwa kiwango kikubwa zinatokana na matumizi mabaya ya barabara kwa madereva huku wengine wakitumia vilevi au kuendesha kwa uzembe mkubwa. Tuna kila sababu ya kuwa makini na sheria hii ili kusaidia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili

1 reply

Comments are closed.