Je, unaijua Dhana ya Uwepo wa Ndoa?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Siku ya leo ninakuletea ufafanuzi wa Dhana ya Uwepo wa Ndoa. Karibu tujifunze.

 Msingi wa Uwepo wa Dhana ya Ndoa

Kama tunavyofahamu na tulivyojifunza kwenye makala ya Ijue Sheria ya ndoa ambapo ndoa ilitafsiriwa kama muungano wa hiyari kati ya mwanamume na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa maisha yao.

Ndoa ili iwe halali lazima ikidhi vigezo vya muungano kuwa wa hiyari, wanandoa wawe na umri unaokubalika kisheria, na vigezo vingine. Ndoa inaweza kufugwa kimila, kiserikali au kidini.

Hata hivyo yapo mazingira ambayo yamejitokeza katika siku hizi za mwanaume na mwanamke kuishi kwa pamoja kwa muda mrefu kama mke na mume pasipo kufunga ndoa rasmi. Maisha haya yameonekana sana kwa watu wa mijini hata vijijini. Changamoto hii inaibua maswali mengi katika jamii kuhusu hali ya kimaisha ya watu hao. Je, ni wanandoa au la? Watoto wakizaliwa kati yao hali yao inakuwaje? Endelea kufuatana nami kujifunza juu ya dhana ya uwepo wa ndoa.

Maana ya Dhana ya Uwepo wa Ndoa

Dhana ya uwepo wa ndoa ni hali ambayo inajitokeza baina ya mwanamke na mwanamume kuishi kwa muda mrefu na kuendelea hata kama watakuwa hawajafunga ndoa rasmi kimila au kidini au kiserikali itathibitika kuwa ni wanandoa.

Katika sheria ya Ndoa ya 1971, Kifungu cha 160 kinaeleza dhana hii kwa ndani zaidi kwa kuanishi vigezo vinavyoweza kuchukuliwa maanani ili kudhibitisha dhana ya uwepo wa ndoa.

Vigezo vinavyothibitisha Uwepo wa Dhana ya Ndoa

  • Udhibitisho wa kuishi kwa mwanamke na mwanaume kwa kipindi kisichopungua miaka 2 na zaidi. Ili dhana hii ithibitike ni lazima uwepo ushahidi wa maisha ya pamoja kati ya mwanamume na mwanamke.
  • Lazima kuwe na udhibitisho kuwa umma au jamii inayowazunguka wanawachukulia na kuwapa heshima kama mke na mume. Hapa swali la kijamii lazima lijibiwe ni kwa namna gani maisha yao yanaonekana mbele ya watu.
  • Lazima ithibitishwe kuwa watu hao walikuwa na uwezo wa kuwa mke na mume wakati walipoanza kuishi pamoja na kama walikuwa na umri unaokubalika kisheria. Umri wa kuweza kuingia kwenye ndoa ni miaka 18 hivyo walio chini ya hapo dhana hii haiwezi kusimama.
  • Ni lazima pia ithibitishwe kuwa kati yao au wote wawili hakuna aliye na ndoa iliyokuwa inaendelea. Hii ni muhimu dhana hii haitasimama pale mwanaume ana mke mwengine eneo lingine na akaende kuishi na mwanamke mwengine katika eneo lingine hata kama ni zaidi ya miaka 2.

Haki na wajibu unaotokana na Dhana ya Uwepo wa Ndoa

Endapo dhana hii itadhibitishwa mahakamani kulingana na vigezo vilivyoainishwa hapo juu basi haki na wajibu wa mwanamke na mwanamume utahesabika kama walio katika ndoa halali;

  • Haki ya mwanamke kudai matunzo kwa ajili yake na watoto waliozaliwa katika kipindi chote
  • Haki ya mwanamke au mwanaume kuomba mahakama kuvunja ndoa hiyo au kutoa amri ya kutengana
  • Haki ya kupewa kukaa na watoto
  • Haki juu ya mali na machumo yaliyopatikana katika kipindi chote walichokaa pamoja.

 

Hitimisho

Sheria ya Ndoa ya 1971 imeainisha dhana hii ya uwepo wa ndoa ili kutoa ulinzi kwa mwanamke na watoto watakaozaliwa katika mazingira hayo. Hata hivyo dhana hii haiondoi umuhimu wa wahusika kuchukua hatua na kufunga ndoa halali kwa mujibu wa sheria kwa taratibu za kidini au kimila au kiserikali kama watakavyoona inafaa.  Upungufu wa kufunga ndoa unaweza kusababisha matatizo makubwa endapo mmoja wapo atafariki na kupelekea watoto na mwenzi kutishiwa kupoteza haki zake za urithi kwa kigezo cha kukosa ndoa.

Hivyo ni rai yetu ndugu msomaji ambaye unaishi na mtu kwa muda wote au zaidi ya maika miwili ni vyema ukafunga ndoa na kuweka ulinzi wa kisheria kwa mwenzi wako na watoto na mali ambazo mmepata kwa pamoja.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Nusim Saidi
    Nusim Saidi says:

    kwanza tunashukuru kwa kujitolea kutufahamisha mambo kadhaa khs sheria, napenda kuuliza swali;”Ukiwa umefunga ndoa ya kiislam lkn taratibu za kuisajili ndoa,hiyo hazikufanyika, swali ni namna gani utaweza kuithibitishia mahakama kwa ushahidi tofauti na cheti cha ndoa?”

    • ulizasheria
      ulizasheria says:

      Karibu ndugu Nusim Said

      Asante kwa swali zuri, kama ulivyoona kwenye Makala ya Sheria Leo.27 Juu ya Dhana ya uwepo wa ndoa ni dhahiri hii ndio njia inayoweza kusaidia kudhibitisha juu ya uwepo wa ndoa yenu. Kwamba jinsi mlivyoishi na mwenzi wenu, namna jamii inayowazunguka wanavyowaelewa na kutafsiri kukaa kwenu.
      Muhimu zaidi kama mmefunga ndoa ambayo haijasajiliwa basi mfuate taratibu za kisheria ili kuisajili kwa msajili wa ndoa ofisi za RITA ambazo zinapatikana kila wilaya na mtapata maelekezo zaidi na nini hatua za kufanya ili ndoa yenu isajiliwe rasmi.

      Karibu sana

Comments are closed.