Je, Unajua Umuhimu wa Wosia?
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala zilizopita tuliwahi kugusia kwa sehemu Sheria ya Mirathi. Tuliangalia mambo kadhaa fuatilia makala ya Sheria Leo.20 kujifunza zaidi. Leo tunakuleta somo juu ya umuhimu wa wosia. Karibu tujifunze.
Maana ya wosia
Wosia ni tamko au matamshi ya mtu kabla hajafariki yakielezea namna mali yake itakavyoshughulikiwa/itakavyomilikiwa baada ya kifo chake. Wosia ni maelezo ya marehemu kabla ya kifo chake juu ya maziko yake yatakavyokuwa, juu ya mali zake jinsi zitakavyorithishwa kwa warithi wake na maelekezo kwa wanafamilia wake.
Dhana ya kuandika wosia imekuwa inaambatana na hofu nyingi sana kwa jamii za kiafrika. Wengi wamekuwa na hofu kuwa ukiandika au ukisema wosia basi tayari umejichulia kifo au umejitamkia kifo cha mapema. Dhana hii haina ukweli wowote kwani sote tunajua kila aliyezaliwa ni lazima atakufa tu, hakuna mwanadamu anayeweza kukiepuka kifo. Uwepo wa wosia hauna uhusiano wowote na kifo cha mtu. Wosia una faida nyingi sana kwa mtu na warithi wake ukiandaliwa mapema utaepusha matatizo mengi kwa jamii.
Aina za wosia
- Wosia wa mdomo: haya ni matamshi ya mwosia (marehemu) kabla ya kufariki akieleza juu ya maziko yake, au mali zake na namna familia anoyoiacha itakavyoendeshwa.
- Wosia wa maandishi: haya ni maandishi yanayoandikwa na mwosia (marehemu) kabla ya kufariki akieleza juu ya maziko yake, na mali zake na namna familia anayoacha itaweza kuendeshwa.
Masharti ya wosia wa mdomo
Endapo mwosia anatoa wosia wa mdomo ili wosia huo uwe halali yapo masharti au vigezo ambavyo vinampasa kuzingatia
- Mwosia lazima awe na akili timamu
- Mwosia awe na umri zaidi ya miaka 20
- Mashahidi wasiopungua 4, kati yao 2 wawe wa ukoo wa mwosia
Masharti ya uandishi wa wosia wa maandishi
Endapo mwosia anatoa wosia wake kwa maandishi anapaswa kuzingatia vigezo vifuatavyo;
- Mwosia awe na akili timamu
- Awe ametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea
- Uoneshe tarehe, mwezi na mwaka
- Mwosia ausie mali zake binafsi si za mtu mwingine
- Ushuhudiwe na mashahidi 2, kwa asiyejua kusoma mashahidi 4
- Sahihi ya mwosia au alama ya kidole gumba
- Uandikwe kwa kalamu ya wino au kupigwa chapa
- Mwosia ataje mtu/watu watakaosimamia ugawaji wa mali.
Kulingana na nyakati na maendeleo tuliyonayo kwa sasa ni vyema zaidi mwosia kutoa wosia kwa njia ya maandishi hii itasaidia kutunza kumbu kumbu na wosia huo kuwa na uhalali zaidi kwani wosia wa mdomo mashahidi wanaweza wasikumbuke vizuri au wasiwe waaminifu.
Madhara ya kutokuandika wosia
Yapo madhara mengi yanayotokea kutokana na kutokuandika wosia kuliko madhara yanayotokea kwa kuandika wosia. Kama tulivyosema hakuna madhara wala udhibitisho kuwa kwa kuandika wosia basi mwosia atafariki. Madhara ya kutokuandika wosia;
- Kupoteza mali mara baada ya kifo: kama marehemu hakuacha wosia ni dhahiri kuwa kuna mali zitapotea. Wapo watu wengi wana mali ambazo familia zao au watu wao wa karibu hawazifahamu, mtu huyo akifariki pasipo wosia mali hizo zinapotea.
- Kuleta usumbufu kwa wanafamilia waliobaki: kufariki pasipo wosia mara zote kunaleta usumbufu kwa warithi na wanaukoo. Zipo taratibu za kukaa vikao vya kumchagua msimamizi wa mirathi na mara nyingine anapingwa, kuna utaratibu wa kufungua shauri la mirathi mahakamani, kukusanya mali ambazo hawazijui zilipo na umiliki wako ni kiasi gani n.k
- Kusababisha watu wasio warithi kuingilia mirathi:kufariki pasipo mirathi kunaweza kusababisha watu wasio warithi kujiingiza kwenye mirathi na kuwaondoa warithi halali. Kutokana na hali za kimaisha na uchumi, kifo cha mwenye mali kinakuwa faida kwa watu wengine nao wanajitafutia sehemu au uhusika ili wapate kurithi.
- Kusababisha ugomvi juu ya mazishi na mali ya marehemu: vifo mara nyingine vinaleta ugomvi wa wanafamilia au ukoo ikiwa marehemu alifariki pasipo kuacha wosia. Tumesikia mara kadhaa zipo kesi mahakamani ambazo wanafamilia wanagombea maiti ya marehemu nazo zinachukua muda mrefu sana haya miezi na miaka. Hii inasababisha hasara kwa Taifa na familia kukaa katika majonzi kwa muda mrefu na hata utengano baina yao.
Yapo madhara mengi sana yanayotokana na kufa pasipo kuandika wosia, kwa haya tuliyosema itoshe tu kuona umuhimu wa jambo hili na kuchukua hatua zinazostahili.
Hitimisho
Kama tulivyoeleza, kuwa wosia ni kitu muhimu sana, hii ni sehemu pekee inayompa fursa marehemu kuwa na kauli juu ya mwili wake, mali zake na familia yake ingawa amekufa. Tusiipoteze fursa hii, wasiliana na wataalam wa sheria (mawakili) waweze kukupa ushauri na kukuongoza kuandika wosia, huwezi jua yatakayojiri kesho. Wasiliana nasi uliza sheria nasi tutakushauri na kukusaidi kuchukua hatua stahiki.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz
Wako
Isaack Zake, Wakili