6. Wafanyakazi Wasio na Mikataba
Utangulizi
Ndugu msomaji wa makala za Uchambuzi wa Sheria ya Kazi nashukuru tumeendelea kuwa pamoja na kupata maarifa haya ambayo yanaletwa kwako kupitia www.ulizasheria.co.tz.
Leo katika makala ya mfululizo juu ya Viwango vya Ajira tunakwenda kuangalia suala la Wafanyakazi Wasio na Mikataba.
Ndugu msomaji pamekuwa na malalamiko ya wafanyakazi wengi juu ya kufanya kazi pasipo mkataba ikiwa ni wa maneno au maandishi. Hii imekuwa changamoto kubwa ambayo imepelekea migogoro mingi na watu wengi kupoteza stahiki zao za kiajira.
Mwajiriwa ni nani?
Ndugu msomaji ni vyema kufahamu tafsiri ya kisheria inayomtambua mwajiriwa ni nani. Nitangulize kusema si kila mfanyakazi ni mwajiriwa. Unaweza kufanya kazi katika ofisi ya mtu au kampuni lakini usiwe mwajiriwa. Hivyo sheria ya Ajira inatupa tafsiri juu ya nani ni mwajiriwa.
Mwajiriwa ni yule aliyeingia mkataba wa ajira au ameingia mkataba wowote na upande mwengine ambapo yeye binafsi (mwajiriwa) anamfanyia kazi huo upande mwengine(mwajiri) na kwamba upande mwengine (mwajiri) si mteja wa mwajiriwa kwa huduma ya kitaaluma au biashara yoyote.
Tafsiri hii inahitaji ufafanuzi kidogo ili kuielewa;
- Mwajiriwa ni yule aliyeingia mkataba wa ajira. Hii ina maana mwajiriwa anapewa mkataba maalumu wa ajira kulingana na aina za mikataba.
- Mwajiriwa ni yule aliyepewa mkataba ambao anafanya kazi yeye binafsi kwa upande mwengine ambaye si mteja wake kwa taaluma au biashara: hii ina maana kwamba Daktari hawezi kuwa mwajiriwa wa mgonjwa. Daktari anafanya kazi kwa taaluma yake kutibu hawezi kudai maslahi ya kiajira kutoka kwa mgonjwa anayetibiwa kwake.
Dhana ya mahusiano ya Kiajira
Sheria za Ajira kwa kutambua uwepo wa waajiri wasio waaminifu ambao wanakwepa kutoa mikataba huku wakiwafanyisha kazi wafanyakazi kwa masharti wanayoyajua wao tu, sheria imeweka mazingira au vigezo ambavyo vinaweza kusaidia kujua iwapo mfanyakazi alikuwa na mahusiano ya aina gani na mwajiri husika.
Vigezo hivyo vimewekwa kwa dhana inayoweza kukanushika ambapo vigezo hivyo au kimojawapo kikiwepo basi itachukuliwa kuwa uhusiano baina ya watu hao yaani mwajiri na mfanyakazi ni uhusiano wa kiajira. Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;
- Iwapo namna ya ufanyaji kazi wa mtu huyo unasimamiwa na kupata maelekezo kutoka kwa mtu mwingine. Mahusiano yanaweza kubainishwa ya kiajira au la pale mfanyakazi anasimamiwa katika majukumu yake na kupewa maelekezo na mwajiri juu ya utendaji wa kazi zake. Ikionekana kuna kigezo hicho basi mahusiano haya yatachukuliwa kuwa ya kiajira hata kama hakuna mkataba wa ajira. Mfano, nyumba nyingi zina wasaidizi wa kazi ambao hawana mikataba, jinsi ya utendaji wao wa kila siku unasimamiwa na wenye nyumba kwa kuwapa maelekezo juu ya majukumu wanayotakiwa kufanya.
- Saa za kazi za mtu huyo zinasimamiwa na kwa maelekezo ya mtu mwingine. Dhana hii inaonesha kuwa masaa ya kazi yaani muda wa kazi kuanza na kukamilika kama unasimamiwa na mtu mwengine basi mahusiano hayo ni ya kiajira. Mfano mfanyakazi unaambiwa unatakiwa uwe eneo la kazi kuanzia saa Moja asubuhi na utakuwa kazini mpaka saa Kumi jioni basi mazingira hayo yanabainisha mahusiano ya kiajira.
- Kwa mtu anayefanya kazi katika Shirika, mtu huyo ni sehemu ya Shirika. Hapa tunaangalia utendaji kazi wa mfanyakazi kwa maana ya majukumu ikiwa ni yale ambayo yanafanana na malengo au kazi za Shirika/Taasisi. Mfano mfanyakazi ni mwalimu na anafanya majukumu ya kufundisha katika Taasisi ya kutoa elimu labda Chuo au Shule basi itadhibitika kuwa uhusiano wao ni wa kiajira hata pasipo mkataba wa ajira.
- Mtu amefanya kazi kwa mtu mwingine kwa wastani wa saa 45 kwa mwezi katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Hapa katika kudhibitisha mahusiano masaa ya kazi yataangaliwa endapo mfanyakazi alifanya kazi kwa mtu/Taasisi kwa wastani wa saa 45 kwa mwenzi ndani ya kipindi cha miezi 3 ndipo itabainika kuwa mahusiano yao yalikuwa ya kiajira.
- Mtu huyo anamtegemea kiuchumi mtu anayemfanyia kazi au kumtolea huduma. Hiki ni kigezo cha utegemezi ambacho kinapimwa endapo mfanyakazi katika kutekeleza majukumu yake anategemea kupata fedha kutoka kwa mtu/Taasisi ili kutimiza majukumu basi huyo ni mwajiriwa. Mfano dereva anayeendesha kwenye Taasisi au mtu binafsi lakini anategemea chombo cha usafiri cha Taasisi au mtu binafsi na mafuta yanawekwa na mtu huyo au Taasisi basi mahusiano yao ni ya kiajira.
- Mtu huyo anapatiwa vitendea kazi na mtu mwingine. Hapa mahusiano ya kiajira yanaonekana endapo mfanyakazi hana vifaa vya kukamilisha kazi yake isipokuwa anapatiwa na mtu/Taasisi anayofanyia kazi. Hii ni tofauti na mtu ambaye anakamilisha majukumu yake kwa vitendea kazi vyake.
- Mtu huyo anafanya kazi au kutoa huduma kwa mtu mmoja tu. Kigezo hiki pia kinaweza kudhibitisha dhana ya uwepo wa mahusiano ya kiajira baina ya pande mbili. Mfanyakazi anapofanya kazi kwa mtu mmoja au Taasisi moja kwa wakati wote basi mahusiano yao ni ya kiajira.
Hivi ni vigezo ambavyo vinaweza kutumika kwa lengo la kudhibitisha au kukanusha juu ya mahusiano ya kiajira baina ya pande mbili. Kwa mujibu wa vigezo husika ikiwa kimojawapo au vyote vitaonekana katika mahusiano ya kazi baina ya pande mbili nasi itachukuliwa kuwa pande mbili zipo katika mahusiano ya kiajira mpaka hapo itakapodhibitishwa vinginevyo.
Hitimisho
Ndugu msomaji leo tumeangalia dhana za kisheria zinazoweza kubainisha uwepo wa mahusiano ya kiajira au la. Dhana hizi ni kinga kubwa kwa wafanyakazi ili waweze kupata stahiki zao mara baada ya kusitishiwa kazi zao au majukumu yao. Hivyobasi ikiwa mahali unapofanya kazi huna mkataba angalia vigezo hivi na kuweza kupima juu ya uhusiano wako na yule unayemfanyia kazi.
Kwa waajiri kutokutoa mikataba hakusadii bali ni kupoteza fursa ya kuweka mahusiano vizuri na wafanyakazi wako. Andika mkataba ili uweze kutambua haki zako na wajibu wako kwani sheria bado inaweza kukubana hata kama hukutoa mkataba wa ajira.
Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz
wako
Isaack Zake, Wakili