Zijue Taratibu za Kisheria za Mirathi yenye Wosia

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala zilizopita tuliwahi kugusia kwa sehemu Sheria ya Mirathi. Katika makala iliyopita tumeona Umuhimu wa Wosia. Leo tunaangalia taratibu za kisheria zinazopaswa kuchukuliwa kwenye mirathi yenye wosia.

Msingi wa Taratibu za Kisheria

Sheria zinazohusu masuala ya mirathi zimeanisha taratibu zinazopaswa kuchukuliwa endapo marehemu aliacha wosia au hakuacha wosia. Taratibu hizi zimewekwa ili kuwasaidia wanufaika na wadai wa marehemu kupata stahiki zao kulingana na mali zilizoachwa na marehemu.

Kama nilivyosema sheria imeanisha namna kuu mbili za kushughulikia mali iliyoachwa na marehemu yaani;

 • Taratibu za kisheria kwa mali iliyoachwa kwa wosia
 • Taratibu za kisheria kwa mali iliyoachwa pasipo wosia

Leo tunakwenda kuangalia taratibu za kisheria kwa mali iliyoachwa kwa wosia.

Taratibu za kisheria zinazohusiana na Mirathi penye wosia

 • Usajili wa kifo cha marehemu: hii ni hatua ya kwanza ili kushughulikia taratibu za mirathi ya Kusajili kifo cha marehemu ndani ya siku 30 ofisi ya vizazi na vifo (RITA) ambazo zipo katika kila wilaya.
 • Ufunguzi wa shauri la Mirathi: Mara baada ya kusajili kifo, waombaji wanafungua shauri la mirathi mahakamani, wakiambatanisha wosia na cheti cha kifo.
 • Mahali pa kufungua shauri la Mirathi: Shauri linaweza kufunguliwa mahakama ya Mwanzo, Wilaya, Hakimu Mkazi au Mahakama Kuu kulingana na sheria inayotumika katika usimamizi wa mali (kimila au Kiislam), thamani ya mali, mali ya marehemu ilipo au mahali marehemu alipofanya makazi.
 • Tangazo: Mahakama itasababisha tangazo ambalo litakalotangazwa kwenye gazeti ndani ya siku 90.
 • Uthibitisho wa Mtekelezaji wosia: Baada ya siku 90 endapo hakuna pingamizi mahakama itamdhibitisha mwombaji.

Mtekelezaji wa wosia baada ya kudhibitishwa atafanya yafuatayo;

 • Kukusanya mali na madeni ya marehemu na kutambua anaowadai. Ni kazi ya Mtekeleza wosia kukusanya mali za marehemu ambazo ameainisha kwenye wosia.
 • Kutayarisha taarifa ya awali ya maelezo/ufafanuzi wa mali na madeni (inventory). Mtekeleza wosia ana wajibu wa kuandaa taarifa ya awali yenye ufafanuzi juu ya mali na warithi ambao wameusiwa mali hiyo.
 • Kugawa mali kwa mujibu wa wosia. Hii ni kazi kuu ya mtekeleza wosia yaani anagawa mali za marehemu kwa mujibu wa wosia ulioachwa na marehemu na si vinginevyo.
 • Kutoa taarifa ndani ya miezi 6 baada ya ukamilishwaji wa zoezi la ugawaji wa mali za marehemu mahakamani.
 • Kufunga jalada: Mahakama kufunga jalada la mirathi baada ya zoezi zima la urithishwaji na maelezo ya mtekeleza wosia kuwasilishwa mahakamani.

Hitimisho

Kama tulivyoeleza, hapo awali juu ya umuhimu wa wosia katika makala iliyotangulia na leo hivi tumeangalia utaratabu juu ya mirathi yenye wosia. Ndugu msomaji utaratibu wa ugawaji mirathi ambayo ina wosia hauna changamoto kuliko ugawaji wa mali isiyo na wosia. iwapo marehemu aliacha wosia mali yake itagawanywa kama alivyoelekeza pasipo kuleta mtafaruku baina ya ndugu na jamaa, hii itasaidia kutunza mshikamano wa familia na kuepusha kupoteza muda mwingi mahakamani kwenye mashauri ya mirathi. Tunaendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa uandishi wa wosia.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  • ulizasheria
   ulizasheria says:

   Asante Alvin

   Ni kweli kuna uhitaji mkubwa wa ufahamu wa masuala mbali mbali ya kisheria nasi ni kazi yetu kujaribu kutimiza mahitaji hayo. Ni vizuri ungetusaidia kwa kuweka swali maalum kuhusu hayo uliyosema nasi tutajitahidi kujibu kwa wakati. Kwa sasa tunaandika uchambuzi wa Sheria ya Kazi naamini tutapata nafasi ya kuzungumzia sheria ya Ardhi na mambo mengine.

   Karibu sana.

Comments are closed.