7. Saa za Kazi

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Ijue sheria ya Kazi nashukuru tumeendelea  kuwa pamoja na kupata maarifa haya ambayo yanaletwa kwako kupitia www.ulizasheria.co.tz katika makala iliyopita tuliangalia viwango vya ajira katika eneo la Mikataba na tukafafanua juu ya wafanyakazi wasio na mikataba. Leo tunakwenda kuangalia eneo lingine katika Sheria ya Kazi katika  Viwango vya Ajira linalohusu Saa  za Kazi. Katika makala hii tutakwenda kuona jinsi sheria ya kazi ilivyoweka viwango vya saa za Kazi ambavyo mwajiri anawajibika kuvizingatia mara anapomwajiri mfanyakazi katika ajira watakayokubaliana.

Msingi wa Viwango vya Saa za Kazi

Kumekuwa na malalamiko juu ya wafanyakazi wakisema wanafanya kazi kwa muda mrefu au wanafanya kazi kwa saa za ziada pasipo malipo yanayostahili na kwa upande mwengine mwajiri analalamika juu ya wafanyakazi kuwa wavivu na kumwibia saa za kazi kwa sababu mbali mbali. Katika makala hii tutajifunza viwango vya ajira vinavyoainisha maswala ya saa za kazi. Sheria ya ajira kwa msingi huo imeainisha saa za kazi ambazo zinatakiwa kuzingatiwa na pande zote katika mkataba wa ajira.

Saa za kazi

Sheria ya kazi imeanisha viwango vya ajira katika eneo la saa za kazi ambazo mwajiri na mfanyakazi wanapaswa kuzingatia.

Sheria ya Kazi imetoa tafsiri kadhaa za kuwawezesha wadau wa ajira kufahamu mambo yahusuyo saa za kazi.

Tafsiri hizo ni kama ifuatavyo;

  • Siku ina maana ya muda wa saa 24 unaopimwa kuanzia muda wa kawaida wa kazi ambao mfanyakazi anaanza kazi. Tafsiri hii ya neno ‘siku’ inahusisha pia neno ‘kila siku’
  • Muda wa ziada: maana yake ni kufanya kazi zaidi na kwa muda wa ziada nje ya muda wa kawaida wa kazi
  • Wiki: ni muda wa siku 7 zinazopimwa kuanzia siku ya wiki ambayo mfanyakazi huanza kazi katika wiki ya kazi. Tafsiri hii inahusisha neno ‘kila wiki’

Saa za Kazi za Kawaida

Sheria inaainisha kuwa saa za kazi za kawaida kwa mfanyakazi kwa siku ni saa 9 na kwa wiki ni saa 45. Pia sheria ya Kazi imeainisha kuwa siku za kazi kwa wiki ni 6. Hivyo kwa ajili ya kufikia wastani wa saa 45 kwa wiki mfanyakazi anaweza kufanya kazi kwa saa 9 kwa siku 5 na kufanyakazi kwa saa 8 kwa siku 6. Hivi ndivyo viwango vya ajira kuhusiana na saa za kazi ambazo mfanyakazi anatakiwa kufanya.

 

 

Mfano wa saa za kazi kwa wiki

  • Jumatatu –  Saa 9                                                             Jumatatu – Saa 8
  • Jumanne –  Saa 9                                                             Jumanne –  Saa 8
  • Jumatano – Saa 9                                                           Jumatano – Saa 8
  • Alhamis –    Saa 9                                                             Alhamis –     Saa 8
  • Ijumaa –      Saa 9                                                             Ijumaa –       Saa 8

Saa.45                                                            Jumamosi – Saa 5

       Saa.45

Kwa mifano hii miwili tunaweza kuona mgawanyo wa masaa ya kazi unaohusisha kufanya kazi kwa siku 5 na siku 6 kwa wiki. Muhimu saa za kazi ya kawaida yasizidi saa 45 kwa wiki.

Mapumziko ya Siku

Mwajiri ni lazima ampe mfanyakazi mapumziko ya angalau saa 12 mfululizo kati ya muda anaomaliza kazi na muda atakaoanza kazi siku inayofuata. Mfano kama mfanyakazi anaanza kazi saa 1 asubuhi na kumaliza kazi saa 10 jioni, (saa 9 za kazi) mfanyakazi anatakiwa kwenda kupumzika mpaka siku inayofuata.

Hatahivyo sheria inaruhusu muda wa mapumziko kwa siku kupunguzwa mpaka saa 8 endapo;

  • Kuna makubaliano ya kimaandishi katika suala hilo
  • Saa za kawaida za kazi zimepishana angalau kwa saa 3; au
  • Mfanyakazi anaishi kwenye nyumba iliyo mahali pa kazi. Mfano watumishi wa nyumbani (House girls/house boys)

Mapumziko ya chakula

Mwajiri ni lazima ampe mfanyakazi mapumziko ya angalau dakika 60 (saa 1) mfululizo kwa ajili ya kupata chakula pale mfanyakazi anapofanya kazi mfululizo kwa kipindi kisichopungua saa 5. Mfano mfanyakazi anaanza kazi saa 1 asubuhi na anaendelea kufanya kazi kwa saa 5 mfululizo yaani mpaka saa 6 mchana, anatakiwa apumzike na kupata chakula kwa muda wa saa 1 yaani saa 6 mpaka saa 7 mchana.

Mwajiri anaweza kumhitaji mfanyakazi wakati wa mapumziko kama tu kazi haiwezi kuachwa bila uangalizi au haiwezi kufanywa na mfanyakazi mwingine. Ikiwa mfanyakazi atafanya kazi wakati wa muda wa mapumziko kwa kuhitajiwa na mwajiri, mwajiri atawajibika kumlipa mfanyakazi saa 1 ya ziada aliyofanya kazi katika muda wa mapumziko.

Mapumziko ya wiki

Mwajiri ni lazima ampe mfanyakazi mapumziko ya wiki angalau saa 24 kati ya siku ya mwisho ya kazi ya kawaida katika wiki na siku ya kwanza ya kawaida ya wiki inayofuata. Mfano siku ya kwanza kazi ni Jumatatu – Jumamosi kwa wastani wa saa 8 kila siku na Saa 5 kwa Jumamosi utapata saa za kazi 45. Mfanyakazi atapumzika Jumamosi na Jumapili  kwa zaidi ya saa 24.

Hatahivyo, kwa makubaliano ya maandishi muda wa mapumziko ya wiki unaweza kuongezwa hadi kufikia saa 60 mfululizo kila baada ya wiki 2 au muda wa mapumziko kupunguzwa hadi saa 8 katika wiki yoyote iwapo muda wa mapumziko katika wiki inayofuata utaongezwa kwa kiwango sawa.

Sheria ya Kazi imebainisha endapo mfanyakazi atafanya kazi siku ya mapumziko au siku ya sikukuu ambayo kwa kawaida ni siku ya mapumziko basi mwajiri lazima amlipe mara 2 ya mshahara wake wa saa kwa kila saa atakalofanya kazi siku ya mapumziko.

Mfano

Maria anapokea mshahara wa Tsh.300,000/- kwa mwezi, katika mwezi huo alifanya kazi siku ya mapumziko jumla ya saa 8.

Mambo ya msingi kufahamu fomula ya mshahara

  • Siku za kazi kwa wiki ni 6 na masaa ya kazi kwa wiki 45
  • Hivyo siku za kazi ni 26 katika mwezi wenye wastani wa siku 30
  • Fomula: 26 /6 = 4.333

Kupata mshahara wa saa

300,000

4.333 x 45

300,000 = 1,538.46

195

Mshahara wa saa ni 1,538.46

Kupata malipo ya kazi siku ya mapumziko: 1,538.46 x saa 8 = 12,307.68

Hivyo mwisho wa mwezi Maria atapokea kiasi cha Tsh.312,307.68

Hitimisho

Ndugu msomaji wa uchambuzi wa sheria ya kazi leo tumejifunza juu ya viwango vya ajira kuhusu saa za kazi, masaa ya kawaida ambayo yanatakiwa kuwa na wastani wa saa 45 kwa wiki, tumeona matakwa ya sheria juu ya mfanyakazi kupata muda wa kupumzika kwa ajili ya chakula, kupumzika kwa siku na kupumzika kwa wiki.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

 

 

 

2 replies
  1. Alex Mengo
    Alex Mengo says:

    Asante kwa elimu nzuri naomba kuuliza swal. Je ikiwa mwajiri atatoa muda wa mapumziko kwa ajili ya chakula je muda huo utahesabiwa kwenye saa za kazi?

Comments are closed.