2.Ukiona Alama Hii unachukua Hatua gani?

Utangulizi

Ndugu msomaji wa ukurasa  nakukaribisha tena kuendelea kujifunza kwa lengo la kuishi kwa mujibu wa sheria.

Mara kadhaa katika shughuli zetu tunakutana na alama au maandishi au mabango ya matangazo iwe barabarani au maeneo mengi kuna alama muhimu huwa tunaiona na mara nyingi tunaipuuza hasa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo au madereva wa magari.

Unapita mahali pameandikwa ‘Amri: Hairuhusiwi kufanya biashara au shughuli yoyote eneo hili‘ au unaona tangazo/kibao kimeandikwa ‘Amri:Usiegeshe gari mahali hapa’

Wengi wetu tunadharau maonyo haya na tunajikuta tunafanya kile ambacho kimekatazwa kufanywa katika eneo husika. Sehemu yenye katazo la kutofanya biashara unakuta biashara zimejaa, sehemu ambayo ina katazo la kutotupa takataka unakuta rundo la taka hata kibao hakionekani, sehemu inayokataza kuegesha magari unayakuta yamejaa, hii imekuwa kawaida ya watu wengi sana.

Nikupe mfano kuna mahali nilikuta kuna kibao kimeandikwa hairuhusiwi kufanya biashara au kuegesha gari – Amri’
Nikaona yapo magari kadhaa yameegeshwa. Akaja dereva mmoja naye akaegesha mahali hapo ile anamaliza kufunga mlango ikaja gari ina madalali waliopewa kazi ya kukamata magari yaliyoegeshwa mahali pasiporuhusiwa. Wakamhoji sababu ya yeye kuegesha gari hapo akajibu kuwa hakusoma kibao hicho, pia akaanza kusema mbona wengine wameegesha. Wale watu wakalikamata gari kulipeleka yadi yao kwa ajili ya kumtoza faini.

Ndugu msomaji kisa hiki ni moja ya visa vingi vinavyotokea kila kukicha hasa kwenye miji mikubwa na watu kupata usumbufu mkubwa wa kupoteza muda na fedha kwa kutozingatia sheria zinazowataka kufanya hivyo. Wanajamii wengi wamekuwa watu wa kudharau miongozo na amri zinazotolewa katika ofisi za umma hata maeneo binafsi. Nimejiuliza ikiwa Amri hizi zinapotolewa kwenye maeneo ambayo ni ofisi au kambi za kijeshi mbona watu hawapuuzi amri hizo? Pitia maeneo ya jeshi bila hata ya kibao huwezi kukuta mtu anatupa taka au anaegesha gari lake na kuliacha hapo.

Ndugu msomaji ni lazima kutambua kuwa hatuishi tu kioholela na kila mmoja kufanya anavyotaka, zipo sheria ambazo vyombo kadhaa ni watekelezaji. Zipo sheria za Majiji ambazo zinasimamia masuala ya kuegesha magari, utupaji wa takataka na maeneo ya kufanya biashara. Siku hizi katika Jiji la Dar es Salaam zipo kampuni zinazotoa huduma ya kuegesha magari na yapo maeneo maalum. Ikiwa una shughuli itakayohitaji usafiri wa binafsi ni muhimu kutafakari mapema ni wapi gari utaegesha ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.

Ndugu msomaji ni muhimu sana kuchukua taadhari katika mienendo ya kila siku kwani kutenda kosa mara kwa mara pasipo kuchukuliwa hatua hakumaanishi kuwa sio kosa ipo siku hatua itachukuliwa dhidi yako na itakuletea hasara.

Mambo ya Msingi kuzingatia

  • Usifanye maamuzi kwa mazoea au kufuata mkumbo hata kama kila mmoja anafanya maamuzi hayo
  • Jiulize sheria inataka nifanye nini katika mazingira kama haya
  • Kama hufahamu sheria inakutaka ufanye nini chukua hatua ya kuuliza inawezekana mtu wa karibu yako akawa na taarifa za kukusaidia wewe kuchukua taadhari ili usivunje sheria.

Hivyo kila siku zingatia miongozo na makatazo yanayoainishwa iwe barabarani au maeneo ya wazi n.k. usifanye uamuzi kwa sababu wengine wanafanya fanya maamuzi baada ya kupima athari zake kwa maisha na ustawi wako.

Nakutakia siku njema sana leo.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies

Comments are closed.