Ijue Sheria ya Mtoto

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Kutokana na uhitaji uliopo katika jamii na umuhimu wa kufahamu mambo ya sheria juu ya kundi la watoto, leo tunakuletea utambulisho wa Sheria ya Mtoto.

Msingi wa Uwepo wa Sheria ya Mtoto

Watoto ni kundi muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla. Hatma ya nchi na maendeleo yake ya baadae ipo katika kundi hili. Hata hivyo watoto wamekuwa kundi ambalo jamii kwa kujua au kutokujua wameacha kutimiza wajibu wao juu yao na kuwapatia haki na stahili zao kisheria. Awali hapakuwa na sheria maalum inayohusu watoto kwa ujumla mpaka mwaka 2009 ilipotungwa Sheria mahsusi kwa kuangalia haki na wajibu wa kundi hili katika jamii.

Sheria ya watoto imekuja kujibu changamoto mbali mbali ambazo wamekuwa wakikutana nazo watoto kama kundi lililotengwa na lisilo na msaada wala ulinzi wa sheria. Watoto wamekuwa wakibaguliwa, wakinyanyaswa, wakifanyiwa vitendo vya kikatili na wazazi au walezi au watu wao wa karibu bila hatua madhubuti kuchukuliwa. Watoto pia wamekuwa wakiingizwa kwenye ndoa mapema kabla ya umri wao kupevuka katika masuala haya.

Maana ya Mtoto                                      

Mtoto ni mtu yeyote chini ya umri wa miaka 18.

Sheria hii imekuja kujibu swali ambalo limekuwa likitatiza mara kwa mara juu ya tafsiri sahihi ya mtoto ni nani. Ipo sheria ya Ndoa ya 1971 ambayo iliruhusu mtoto kuingia kwenye ndoa chini ya miaka 18 kwa kibali cha wazazi, wakati huo huo sheria ya mikataba inasema mtu chini ya umri 18 haruhusiwi kuingia kwenye mkataba wowote. Wakati huo huo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mtu mzima mwenye haki ya kupiga kura anaanzia miaka 18.

Hivyo Sheria ya Mtoto kuja na tafsiri juu ya utambulisho wa mtoto imesaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuhakikisha haki na wajibu wa kundi hili na tafsiri sahihi kwenye sheria nyingine juu ya mtoto.

Lengo la Sheria

Yapo malengo kadhaa ya Sheria ya Mtoto ambayo imelenga kuyatimiza, hata hivyo malengo makuu mawili ni;

 • Kuunganisha masuala yote ya kisheria yanayohusu watoto.
 • Kuainisha haki za mtoto na kutunza ustawi wa watoto kulingana na mikataba ya kimataifa

Mambo Muhimu katika Sheria ya Mtoto

Yapo mambo kadhaa muhimu yaliyoainishwa kwenye Sheria ya Mtoto hata hivyo hapa tutayataja mambo muhimu;

 1. Haki za Mtoto

Sheria ya mtoto imeainisha haki mbali mbali za mtoto ambazo jamii inapaswa kuzizingatia  haki hizo ni kama; haki ya kutokubaguliwa, haki ya kuwa na jina na uraia, haki ya kutunzwa na kukua akiwa na wazazi wake, haki ya maoni, haki ya kulindwa kutokana na mateso au adhabu zilizopitiliza. Ukiukaji wa haki hizi za mtoto zinaweza kupelekea aliyekiuka akitiwa hatiani kulipa faini ya Tsh.5,000,000/- au kifungo cha miezi 6 au vyote kwa pamoja.

 1. Wajibu wa Mtoto

Pia Sheria ya Mtoto imempa mtoto wajibu wa kutekeleza mbele ya jamii ili aweze kuwa raia mwema na mwenye maadili mazuri katika jamii. Sheria imempa mtoto wajibu wa kufanya kazi pamoja na familia, kuwaheshimu wazazi, walezi,  na watu wazima na kuwasaidia wanapohitaji msaada, kutumikia jamii na taifa kwa kuwekeza nguvu zake, vipaji na akili zake na kutunza na kulinda umoja wa jamii kwa ujumla.

Kwa ujumla Sheria ya Mtoto imeanisha mambo mengine mengi kama;

 • Ulinzi wa Mtoto
 • Malezi na Matunzo ya Mtoto
 • Taratibu za Kuasili mtoto
 • Taratibu za Kuajiri Mtoto
 • Makosa ya kisheria ya Mtoto na namna ya kuyashughulikia.

Vyombo vinavyohusika na usimamizi wa Sheria ya Mtoto

Sheria ya Mtoto inahusisha Taasisi nyingi ambazo zipo kwenye Sheria ya Mtoto na nyingine zipo kwenye mfumo wa utekelezaji wa sera za Kiserikali kuhusiana na mtoto. Ndani ya Sheria ya Mtoto vipo vyombo vinavyohusika moja kwa moja na usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mtoto;

 1. Ofisi ya Ustawi wa Jamii

Ofisi ya Ustawi wa Jamii ina jukumu la kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Mtoto katika ngazi za kaya, mtaa na wilaya. Ofisi hii inahusika na utekelezaji wa Sera na kufuatilia utekelezaji wa Sheria.

 1. Serikali za Mitaa

Mamlaka ya Serikali ya Mtaa kuangalia ustawi wa watoto katika ngazi ya mtaa ambao watoto wanapatikana. Hapa Ofisa wa Ustawi wa Jamii anashirikiana na Serikali ya Mtaa kuangalia maslahi ya watoto wa eneo hilo.

 1. Mahakama ya Watoto

Hiki ni chombo cha Maamuzi kilichoundwa na Sheria ya Watoto kwa ajili ya kusikiliza mashauri mbali mbali ya makosa ya kijinai ambayo mtoto amehusika. Utaratibu wa uendeshaji wa mashauri haya hauruhusu watu wengi kuudhuria bali wahusika tu.

 

 1. Shule za Watoto (Gereza la Watoto)

Hii ni Taasisi muhimu kwa ajili ya kuwatunza watoto ambao walionekana na hatia katika makosa waliyoshtakiwa kwenye Mahakama ya Watoto. Hapa wanawekwa kwa ajili ya kujifunza kuondokana na tabia zinazoweza kuwasababishia hatari na kutokuwa raia wema.

 

 1. Vituo vya Kulea watoto

Sheria ya Mtoto pia inatambua vituo mbali mbali vya kulea watoto walio katika mazingira magumu. Vituo hivi vinaweza kuwa vya Serikali au Taasisi binafsi au mtu binafsi. Sheria imeweka utaratibu wa uanzishwaji na namna ya kuviendesha.

Umuhimu wa Sheria ya Watoto

Sheria hii ina umuhimu mkubwa kwetu kama jamii kwa kuifahamu na kuitekeleza ipasavyo. Ipo lugha ambayo watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wamepachikwa na jamii kuwa ni watoto wa mtaanimtazamo huu si sahihi kwani ‘mtaa haujawahi kuzaa mtoto’ watoto hawa walizaliwa na watu ambao ni baba na mama zao, watoto hawa wana ndugu na jamii ambayo inapasa kuchua wajibu wa kuwalinda na kuwatunza. Kama jamii itashindwa kuchukua wajibu huo mapema tutajenga taifa hatari zaidi kwa kuwa na watu wasio na elimu na maadili mema na wanaweza kuwa wahalifu wa  kudhuru hata wazazi, ndugu zao na jamii kwa ujumla. Kama methali ya Kiswahili inavyosema samaki mkunje angali mbichi’

Hitimisho

Ndugu msomaji Sheria ya Mtoto ni sheria muhimu sana katika ujenzi wa Taifa ambalo linazingatia dira na maono ya maendeleo kwa vizazi vya sasa na baadae. Ni muhimu kwetu kuifahamu ili tuweze kuwatendea watoto jinsi inavyostahili kila wakati. Sheria hii itatusaidia kufahamu madhila wanayopata watoto pindi wanapoondokewa na wazazi au wazazi wanapotengana. Muhimu kwetu kama raia mmoja mmoja kuchukua wajibu wa kuwatunza na kuwalea watoto.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili

4 replies
 1. Nasemba
  Nasemba says:

  Tunashukuru sana mheshimiwa Wakili Isack Zake kwa kuendelea kutuelimisha kuhusiana na sheria mbalimbali.

  Kazi nzuri sana na yenye uzalendo mkubwa.

  • ulizasheria
   ulizasheria says:

   Asante Nasemba

   Nashukuru kuwa natimiza wajibu huu ambao kila mtu kwa wadhifa wake au utaalam alionao anapaswa kutoa mchango kwa jamii ili kuyafanya maisha kuwa bora zaidi. Asante kwa kufuatilia mambo mbali mbali tunayojifunza.

 2. Meneja Shija
  Meneja Shija says:

  Habar MrIsaack, umeelezea kuhusu sheria na utunzaji wa watoto kwa ujumla katika jamii, swali langu, endapo wazazi wakatengana na mtoto hajafikisha umri wa miaka 18 ana miaka sita, sheria inasemeje kuhusu nani anatakiwa amtunze huyo mtoto ikumbukwe kua hawajafunga ndoa. Ahsante.

  • ulizasheria
   ulizasheria says:

   Asante ndugu Shija

   Swali lako lina mambo kadhaa ya kuangalia, umeeleza juu ya wazazi kuzaa mtoto ingawa hawajafunga ndoa. Majibu ya swali hili nimeshajibu kwenye moja wapo ya maswali kuhusu muda wa watu kuhesabiwa kuwa mke na mume ni angalau miaka 2 wamekaa pamoja.
   Sheria ya mtoto ya 2009 inaeleza mazingira ya matunzo ya mtoto kwamba ni wajibu wa mzazi wa mtoto au mlezi au mtu mwengine mwenye dhamana kuhakikisha mahitaji ya mtoto yanatimizwa mahitaji kama; chakula, malazi, mavazi, huduma za afya, elimu, uhuru na haki ya kucheza hii ni kifungu cha 8 cha Sheria ya Mtoto 2009.

   Hata hivyo suala la matunzo kwa maana mwenye wajibu wa kukaa na mtoto endapo wazazi watatengana (Custody of a Child) Sheria ya Mtoto inaruhusu mzazi yeyote au mlezi au ndugu anayemtunza mtoto kufanya maombi mahakamani ya kupewa mamlaka ya kukaa na mtoto (custody of child). Katika mchakato huo Mahakama itazingatia maslahi ya mtoto ambayo ni kuwa na mama yake mzazi akiwa katika umri wa chini ya miaka 7. Hata hivyo kigezo hiki kinaweza kisitumike kama kutajitokeza ushahidi kuonesha mama hawezi kukidhi jukumu hilo kutokana na sababu mbali mbali. Hii pia haimaanishi akiwa na miaka 7 ni lazima awe na baba, bali Mahakama itaangalia na vigezo vingine hasa kuzingatia maslahi ya mtoto kwanza. Kifungu cha 26,37, 38 cha Sheria ya Mtoto 2009.

   Kumbuka:
   1. Yeyote kati ya baba, mama au mlezi mwengine anaweza kuwasilisha maombi ya kupewa mamlaka ya kukaa na kumtunza mtoto
   2. Mahakama ina wajibu wa kuzingatia vigezo mbali mbali ikiwepo cha umri, jinsia, maoni ya mtoto n.k
   3. Mzazi au mlezi atakayepewa wajibu wa kukaa na mtoto (custody) atamruhusu mtoto kumtembelea na kukaa kwa mzazi mwengine wakati mtoto akihitaji. Hii ina maana mzazi au mlezi atakayepata haki ya kukaa na mtoto hatakiwi kumnyima mzazi mwenzake au mtoto huyo kwenda kwa mzazi mwenzake na kukaa naye kwa kipindi.

   Lengo la Sheria ni kuhakikisha maslahi ya mtoto yanazingatiwa kwa kiwango kikubwa na wala haingizwi katika migogoro ya ndoa inayowahusu wazazi wake. Ni muhimu kwa wazazi kujaribu kutunza mahusiano yao ya ndoa yasiharibike na ikitokea hivyo wajitahidi tofauti zao zisiende kwa watoto wao.

   Karibu sana

Comments are closed.