8. Saa za Kazi za Ziada na Mengineyo

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Ijue sheria ya Kazi nashukuru tumeendelea  kuwa pamoja na kupata maarifa haya ambayo yanaletwa kwako kupitia www.ulizasheria.co.tz katika makala iliyopita tuliangalia viwango vya ajira katika eneo la Saa za Kazi. Tuliichambua sheria ya kazi na viwango vya ajira kuhusu saa za kazi za kawaida na mapumziko ambayo mfanyakazi ana haki ya kuyapata kwa saa, siku na wiki. Kama hukusoma makala hiyo angalia Uchambuzi wa Sheria.7.Saa za Kazi. Leo tunaendelea kuangalia mambo mengine yanayohusu Saa za Kazi. Karibu sana tuendelee na mfululizo wa makala hizi.

Saa za Ziada (Over time)

Kazi katika saa za ziada zitafanyika kwa mujibu wa makubaliano baina ya mwajiri na mfanyakazi, hii ina maana kuwa ili mfanyakazi afanye kazi saa za ziada lazima yawepo makubaliano. Katika makubaliano juu ya saa za ziada ni lazima yahakikishe hayazidi saa 3 kwa siku na saa 50 kwa mzunguko wa wiki 4.

Mfano: Saa za kazi za kawaida ni saa 9 kwa siku ikiwa mwajiri anataka mfanyakazi afanye kazi na saa za ziada kwa siku zitaongezeka saa 3 tu hivyo kufanya jumla ya saa za kazi kwa siku kuwa 12.

Masharti ya kuzingatia kuhusu saa za kazi

  • Lazima masaa ya kawaida yawe yamekamilika ikiwa ni saa 8 au 9 kwa siku
  • Mfanyakazi haruhusiwi kufanya kazi zaidi ya saa 12 kwa siku ikijumlisha saa za kazi kawaida na saa za ziada
  • Saa za kazi hazitakiwi kuzidi saa 3 kwa siku
  • Mfanyakazi atakayefanya kazi saa za ziada anastahili kulipwa 1.5 ya mshahara wake wa saa kwa kila saa ya ziada aliyofanya kazi.

Mfano

Mshahara wa Maria ni Tsh.300,000/- kwa mwezi. Maria amefanya saa za ziada 30 katika mwezi. Je, Maria atapata shilingi ngapi katika mwezi huo?

Mambo ya msingi kufahamu fomula ya mshahara

  • Siku za kazi kwa wiki ni 6 na masaa ya kazi kwa wiki 45
  • Hivyo siku za kazi ni 26 katika mwezi wenye wastani wa siku 30
  • Fomula: 26 /6 = 4.333

Kupata mshahara wa saa

300,000

4.333 x 45

300,000 = 1,538.46

195

Mshahara wa saa ni 1,538.46

Kupata ujira wa saa za ziada (overtime)

1,538.46 x 1.5 x 30 = 69,230.7

Hivyo Maria atapata Tsh.300,000 + 69,230.7 = Tsh.369,230.7

 

Wiki ya Kazi Nyingi

Kwa makubaliano ya maandishi, mfanyakazi anaweza kufanya kazi kwa saa 12 kwa siku ikiwa ni pamoja na muda wa chakula cha mchana bila kulipwa malipo ya saa za ziada, ili mradi mfanyakazi huyo asifanye kazi kwa zaidi ya saa 45 kwa wiki na si zaidi ya siku 5 kwa wiki na si zaidi ya saa za ziada 10 kwa wiki.

Mfano

Mfanyakazi anaweza kukubaliana na mwajiri kufanya kazi katika utaratibu ufuatao;

  • Jumatatu Saa – 12
  • Jumanne Saa – 12
  • Jumatano Saa – 12
  • Alhamis Saa – 9

Jumla Saa.          45

Mfano

Endapo wiki ya kazi nyingi itahusisha na saa za ziada basi utaratibu utakuwa huu.

  • Jumatatu Saa – 12
  • Jumanne Saa – 12
  • Jumatano Saa – 12
  • Alhamis Saa – 12
  • Ijumaa Saa –    7

Jumla Saa.          55

Alhamis kuna saa 3 za ziada na Ijumaa saa zote 7 ni za ziada.

 Kuwastanisha muda wa Kazi

Kutegemea mahitaji ya mwajiri bila kujali kizuizi cha muda wa kazi wa saa 12 kwa makubaliano ya maandishi Chama ca Wafanyakazi na mwajiri wanaweza kupanga muda wa kazi kwa wastani. Katika utaratibu huu mfanyakazi atafanya kazi kwa muda usiozidi saa 40 kwa wiki na saa za ziada zisizozidi 10 kwa wiki. Makubaliano haya ya pamoja hayatazidi kipindi cha mwaka mmoja. Katika utaratibu huu muada wa kazi unaweza kutofautiana katika wiki mbalimbali ili mradi saa za kufanya kazi zisizidi ukomo wa kisheria. Mfano wa maeneo ya kazi ambayo yanaweza kuingia makubaliano ya kuwastanisha muda wa kazi ni viwanda vya uzalishaji ambavyo vinafanya kazi kwa saa 24, maeneo ya mitambo ya umeme n.k.

Mfano

Mwajiri na Chama cha Wafanyakazi wanaweza kukubaliana kuwastanisha muda kwa kipindi cha miezi 3. Hivyo kwa kipindi cha miezi hiyo 3 kitakuwa saa za kazi za kawaida x wiki 4 x miezi 3:

40 x 4 x 3 = 480

Kwa hiyo mwajiri anaweza kupanga muda wa kazi kulingana na mahitaji yake ndani ya mzunguko wa miezi 3 kwa kuwataka wafanyakazi wafanye kazi kwa muda mrefu katika baadhi ya wiki na muda mfupi katika baadhi ya wiki. Jambo la muhimu la kuzingatia ni kuhakikisha wafanyakazi hawafanyi kazi kwa zaidi ya saa za kawaida 40 kwa wiki na saa 10 za ziada kwa wiki.

 

 Kazi za Usiku

Kwa tafsiri ya sheria ya Kazi, kazi za usiku ni zile zinazofanyika mara baada ya saa 2 kamili usiku na kabla ya saa 12 kamili alfajiri.

Masharti ya kazi za usiku

Sheria imeweka masharti na marufuku ya mwajiri kuwataka baadhi ya makundi ya wafanyakazi kufanya kazi usiku;

  • Wajawazito ambao wamebakiza miezi 2 kabla ya tarehe ya matarajio ya kujifungua au kabla ya hapo kwa ushauri wa Daktari
  • Wanawake wazazi miezi 2 baada ya kujifungua au zaidi ya hapo kwa ushauri wa Daktari
  • Watoto chini ya maika 18
  • Mfanyakazi yoyote mwenye udhibitisho wa Daktari kuwa hawezi kufanya kazi za usiku

Mfanyakazi anayefanya kazi za usiku atalipwa na mwajiri walau posho ya  asilimia tano (5%) ya mshahara wake wa saa kwa kila saa aliyofanya kazi usiku.

 

Mfano

Maria analipwa mshahara wa Tsh.300,000/- kwa mwezi amefanya kazi za usiku kwa siku 7 kwa mwezi na kwa kila siku alifanya kazi kwa saa 6. Je, atalipwa posho ya kiasi gani kwa kazi ya usiku.

Kupata mshahara wa saa

300,000

4.333 x 45

300,000 = 1,538.46

195

Mshahara wa saa ni 1,538.46

Kupata saa alizofanya kazi usiku;

Saa 6 x siku 7 =40

Posho ya usiku:    1,538.46 x 42 x 5 = 3,230.766

100

Hivyo Maria atalipwa Tsh.30,3230.76 ikiwa ni mshahara wa mwezi na posho ya usiku.

Hitimisho

Ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa sheria ya Kazi, leo tumejifunza mambo mengine juu ya Saa za kazi hasa saa za ziada, wiki ya kazi nyingi, namna ya kuwastanisha muda na kisha kazi za usiku. Hivi ni viwango vya chini vya ajira ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa sheria ikiwa mfanyakazi na mwajiri wanaweza kukubaliana zaidi ya viwango hivi sheria haiwazuii ila kwa kiwango kile kinachoruhusiwa. Mwajiri anaweza kuwa na posho ya saa za kazi za usiku zaidi ya 5% au malipo ya saa za ziada zaidi ya 1.5 ya mshahara wa saa.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

1 reply
  1. GODFREY PHILOSOPHER OPINO
    GODFREY PHILOSOPHER OPINO says:

    sheria inasema nini juu ya mtumishi wa umma ( askari) anaefanya kazi zaidi ya wiki mbili kwa kazi za usiku??

Comments are closed.