Je, Unazijua Sababu za kuifanya ndoa kuwa Batilifu?

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala za Sheria Leo ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Leo tunaendelea kuangalia kwa sehemu baadhi ya mambo yanayoweza kuifanya ndoa kuwa Batili. Karibu tujifunze.

Maana ya Ndoa Batilifu

Hii ni ndoa ambayo itachukuliwa kisheria kuwa ni halali hadi hapo amri ya kuibatilisha itakapotolewa na mahakama. Ndoa batilifu ni halali kama ndoa nyingine ambayo ilifuata taratibu za kisheria kama inavyotakiwa, hata hivyo kunajitokeza kasoro fulani wakati wa ndoa inaendelea ambazo zinaweza kusabalisha ndoa hiyo kubatilishwa.

Ndoa hii inaendelea kuwa halali mpaka upande ulioathiriwa na mojawapo ya sababu za kuifanya batilifu atakapochukua hatua za kisheria dhidi ya upande mwengine.

Sababu zinazofanya ndoa kuwa batilifu

Sheria ya Ndoa ya 1971 imeainisha baadhi ya sababu ambazo zinaweza kufanya ndoa ikawa batilifu ikiwa sababu hizo zitadhihirika na kudhibitishwa katika ndoa. Sababu hizo ni kama ifuatavyo;

  1. Maradhi ya Zinaa

Hii inajitokeza endapo mmoja wa wanandoa kabla ya kufunga ndoa alikuwa na ungonjwa wa zinaa na mwengine hakujua uwepo wa ugonjwa huo wakati wa kufunga ndoa basi pale atakapogundua anaweza kulalamika mahakamani juu ya suala hilo na mahakama inaweza kuibatilisha ndoa.

 

  1. Kukataa kwa makusudi kuitimiliza ndoa

Hii hutokea endapo mara baada ya kufunga ndoa mmoja wa wanandoa anakataa kwa makusudi kuitimiliza ndoa (kufanya tendo la ndoa) kwa mwenzake, basi aliyeathiriwa na kitendo hiki anaweza kufungua shauri mahakamani ili ndoa ibatilishwe. Kwa kawaida mara baada ya ndoa kufungwa wanandoa wana wajibu wa kuitimiliza ndoa kwa kushiriki tendo la ndoa. Kukataa kuitimiliza ndoa inaweza kuwa sababu ya msingi endapo anayekataa hana sababu ya kukataa na upande mwengine umetumia kila njia ya kuhakikisha suala hili linakamilika.

 

  1. Mimba ya mwanaume mwengine

 Ikiwa wakati wa kufunga ndoa imethibitika mwanamke ana mimba aliyopata kwa mwanaume mwengine, mume anaweza kuiomba mahakama kuibatilisha ndoa hiyo. Kama itadhibitika kuwa mume alijua hali hiyo wakati wa kufunga ndoa, lalamiko lake halitasikilizwa.

 

  1. Wazimu au kifafa cha vipindi

 Wazimu au kifafa cha vipindi inaweza kuwa sababu ya kubatilisha ndoa, endapo mmoja wa wanandoa ana hali hiyo ambapo mwenzake hajajua. Mwanandoa ambaye hakutambua hali hiyo ya mwenzake anaweza kuiomba mahakama kubatilisha ndoa husika. Hata hivyo katika hali hii lazima iwe ugonjwa unaojirudia rudia sio mtu aliyewahi kuugua na akapona.

 

  1. Kushindwa kutimiliza ndoa

Kushindwa kutimiliza ndoa ni hali inayomkuta mwanandoa aliyeshindwa kutimiza tendo la ndoa. Hii ni tofauti na ile ya kukataa, hapa inawezekana anataka kutimiliza lakini kutokana na maumbile anashindwa kutekeleza wajibu huu.

  • Kwa mwanaume kama anashindwa kutimiliza ndoa kwa sababu ya kukosa nguvu za kiume basi ndoa hiyo inaweza kubatilishwa lakini lazima ithibitike kuwa hali hiyo ilijitokeza kabla au wakati wa kufunga ndoa na si baada ya kufunga ndoa. Lazima kukosa nguvu hizo za kiume kudhibitishwe na Daktari kuwe hakuponi au kunapona lakini mwanaume hataki matibabu.
  • Kwa mwanamke anaweza kuwa na maumbile ambayo yatasababisha ndoa ishindwe kutimilika. Hii lazima idhibitishwe na Daktari kwamba hali hiyo haiponi au mwanamke amekataa matibabu.

Mambo muhimu kuzingatia

  • Mashauri yanayohusu kubatilisha ndoa ni lazima yafunguliwe mara baada ya kufunga ndoa yasichukue muda mrefu. Shauri likipelekwa zaidi ya mwaka mmoja itaonekana kuwa mwanandoa aliridhia hali hiyo
  • Lazima idhibitike kuwa mlalamikaji hakujua kasoro hiyo wakati wa kufunga ndoa hiyo na baada ya kuijua hajawahi kuingiliana na mwenzie
  • Sababu zinazohusika na ugonjwa au uwezo wa kutotimiza ndoa lazima vidhibitishwe na Daktari.

Ndoa batilifu huvunjwa na mahakama pekee baada ya kupokea malalamiko toka kwa mmoja wa wanandoa. Ikiwa hakutakuwa na malalamiko yaliyopelekwa mahakamani na aliyeathirika na kasoro hizo, ndoa hiyo itadumu ama mmoja wapo afariki au mpaka talaka itolewe na mahakama kama kuna maombi ya kuvunja ndoa (maombi ya kuvunja ndoa ni tofauti na maombi ya kubatilisha ndoa)

 

Hitimisho

Sheria ya ndoa imeweka misingi ambayo inaweza kuifanya ndoa kuwa batilifu kama tulivyoona sababu hizo zilizoainishwa. Kwa mtazamo sababu hizi zote zinajitokeza kwa pande mbili kutokuelezana ukweli juu ya hali zao. Nyakati hizi madhehebu yanashauri wanandoa kufanya vipimo kufahamu hali za afya zao kabla ya kuingia kwenye ndoa. Muhimu zaidi kwa wanandoa au wanaotarajia kufunga ndoa kupeana taarifa juu ya hali zao ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa upande mwengine utakuja kugundua juu ya taarifa fulani katika ndoa. Pia sababu hizi zisitumiwe vibaya kwa lengo la kubatilisha ndoa ni muhimu kuwaona madaktari kuhusu maradhi husika na mtu akipata matibabu na kufuata maelekezo yanayohusika.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

Wako

Isaack Zake, Wakili