Je, unaijua Mihimili ya Dola?

Utangulizi

Karibu ndugu yangu msomaji na mfuatiliaji wa ukurasa huu. Tunaendelea kukuletea maarifa ya kisheria kwa uchambuzi wa masuala kadhaa ya kisheria. Kila siku tumeendelea kujifunza mambo ya msingi ya sheria na kuzitambulisha sheria mbalimbali ili uweze kuzitambua na kujua namna ya kuishi kwa mujibu wa sheria. Leo tutaitambulisha kwako Mihimili ya Dola.

Maana ya Mihimili ya Dola

Hivi ni vyombo au taasisi zilizoundwa kwa Katiba zenye mamlaka mbali mbali juu ya kuendesha masuala ya nchi kwa ujumla. Dola ni eneo la kimamlaka linalotambuliwa kitaifa na kimataifa lenye mipaka yake, watu wake, ardhi na uongozi wake. Mara kadhaa neno dola limekuwa likitumika badala ya nchi au taifa. Hivyo mihimili ya dola ni vyombo vinavyobainisha mamlaka ya kidola ndani ya nchi husika.

Katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) vyombo hivi vimeainishwa kama vyombo vikuu vyenye kushika mamlaka na uendeshaji wa Serikali katika shughuli za kila siku.

Tafsiri ya neno Katiba ni sheria kuu ya nchi au sheria mama ya nchi fulani. Katiba ni msingi wa uendeshaji wa mambo yote katika nchi. Katiba inamaanisha makubaliano au mkataba kati ya watawaliwa na watawala.

Msingi juu ya Mihimili ya Dola

Kama nilivyoeleza awali tafrisi ya dola ni eneo lenye mamlaka ambapo linahusisha ardhi na mipaka yake, watu, na uongozi. Hivyobasi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wa nchi mbili yaani iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika tarehe 24 April 1964. Hali hii ya Muungano inatambuliwa na Katiba ya JMT  Ibara 1 inayozungumzia juu ya Tanzania kuwa nchi moja na Ibara ya 2 ya Katiba ya JMT inaelezea eneo la Tanzania kuhusisha; eneo lote la Tanzania Bara (Tanganyika) na eneo lote la Tanzania Zanzibar na sehemu ya bahari inayopakana nayo. Huu ndio msingi mkuu wa uwepo wa Mihimili ya dola yaani liwepo eneo la mamlaka.

Mihimili ya Dola

Katiba ya JMT inaainisha mihimili ya dola ambayo itakuwa na wajibu wa kuendesha shughuli za siku kwa siku zinazohusiana na utawala wa nchi. Ibara ya 4 ya Katiba JMT inaaninisha juu ya mamlaka ya mihimili ya dola

‘Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji,vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma’

Ufafanuzi

  • Vyombo viwili vya mamlaka ya utendaji: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
  • Vyombo viwili vya mamlaka ya utoaji haki: Mahakama ya Jamhuri Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar
  • Vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za Umma: Bunge la JMT na Baraza la Wawakilishi.

Katika ufafanuzi huu tunaweza kuona uanzishwaji wa mihimili ya dola ambavyo

  • Serikali
  • Mahakama
  • Bunge

Katika pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaona uazishwaji na majukumu ya vyombo hivi ili kusimamia utendaji na mamlaka ya kila siku katika eneo la JMT.

Mihimili hii ya dola ni vyombo ambavyo vimeundwa kikatiba na vinatakiwa kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa Katiba ya JMT. Kila chombo kina mamlaka yake, majukumu yake na mipaka yake katika utendaji kazi. Mihimili hii inajitegemea na Katiba imeweka misingi ya kuhakikisha mamlaka zake haziingiliani katika kutekeleza majukumu yao.

Hitimisho

Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ndio msingi wa mamlaka zote za Tanzania ambapo kila chombo cha kisheria kunapata uhalali wa mamlaka na utendaji wake kutoka kwenye Katiba. Mihimili ya dola inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa misingi iliyoainishwa kwenye Katiba ya JMT.

Hivyo ni muhimu sana kwa mwananchi kuifahamu mihimili ya dola na mamlaka zake na namna inavyofanya kazi. Endapo mtu unatafuta utekelezaji wa jambo fulani mahali husika ni Serikali, endapo unataka haki mahali husika ni Mahakamani na endapo unataka mabadiliko au uanzishwaji wa sheria kukidhi haja fulani basi mahali pake ni Bunge.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili

2 replies
  1. Robert medson bala
    Robert medson bala says:

    Asanteni sana mumenisaidia kujua maana ya mihimili ya Dola, katiba na misingi juu ya mihimili ya Dola. Niko nanyi kila siku!

Comments are closed.