Mgawanyo wa Makundi ya Ardhi
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala ya Ijue Sheria ya Ardhi tuliitambulisha Sheria ya Ardhi kama hukupata nafasi pitia makala hiyo. Katika makala ya leo tunaangalia Makundi ya Ardhi. Karibu sana.
Msingi wa Utawala Ardhi
Sheria za Ardhi zinatambua kwamba ardhi ni mali ya umma na utawala juu ya ardhi utasimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana madaraka ya mwisho juu ya ardhi kama mdhamini wa ardhi ya umma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake juu ya ardhi anaweza kukaimisha madaraka hayo kwa wasaidizi wake ikiwa ni Waziri anayehusika na masuala ya Ardhi au Makamishna wa Ardhi na maafisa mbali mbali ambao watatekeleza majukumu kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makundi ya Ardhi
Ardhi ya Tanzania kwa minajili ya matumizi imegawanywa kisheria katika makundi makuu matatu ambayo ni; Ardhi ya Jumla, Ardhi ya Kijiji na Ardhi ya Hifadhi
- Ardhi ya Jumla
Ardhi hii si ya Kijiji wala si Ardhi ya Hifadhi. Kundi la ardhi hii linashughulikiwa na Sheria ya Ardhi Na.4 ya 1999. Ardhi hii ndiyo inatumiwa kwa shughuli mbali mbali mijini kama makazi, biashara na uwekezaji mbali mbali.
- Ardhi ya Kijiji
Ardhi hii imetambuliwa na kuelezwa kwa kina katika Sheria ya Ardhi Vijijini Na.5 ya 1999. Hii ni ardhi iliyo ndani ya mipaka ya vijiji ambayo imesajiliwa kwa kufuata sheria zilizowekwa. Zipo taratibu zilizoainishwa kisheria namna ya kumiliki na kutumia ardhi ya Kijiji.
- Ardhi ya Hifadhi
Hii ni ardhi ambayo imetengwa kwa madhumuni maalum nayo ni pamoja na
- Maeneno ya hifadhi ya misitu
- Mbuga za wanyama
- Hifadhi za maji (bahari, mito, mabwawa na maziwa)
- Ardhi ardhi yenye majimaji
- Hifadhi ya barabara
- Maeneo ya wazi
- Maeneo yaliyotangazwa kuwa ni ardhi hatari
Mamlaka ya Rais kufanya mabadiliko ya makundi ya ardhi
Sheria za Ardhi zinampa mamlaka Rais au mwakilishi wake kuweza kubadilisha sehemu ya kundi la ardhi kutoka aina moja kwenda nyingine. Mfano ardhi ya jumla inaweza kubadilishwa kuwa ardhi ya kijiji au ardhi ya hifadhi, na ardhi ya kijiji inaweza kubadilishwa kuwa ardhi ya jumla au ya hifadhi. Katika kufanya mabadiliko haya yapo mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa.
Kuhamisha Ardhi ya Jumla au Hifadhi kwenda Ardhi ya Kijiji
- Waziri wa Ardhi atahakikisha tangazo (notisi) linachapishwa kwenye gazeti la serikali na kupelekwa kwa Baraza la Kijiji husika angalau siku 60 kabla ya kufanyika uhamisho huo. Notisi hiyo itaeleza mambo yafuatayo;
- Eneo linalokusudiwa kuhamishwa
- Mipaka ya eneo lazima iainishwe
- Sababu zinazotokana na zoezi hilo
- Muda wa kufanya uhamisho
2. Ikiwa tangazo la kusudio la kuhamisha ardhi ya Hifadhi basi notisi hiyo inapasa kuwafikia wafuatao;
- Waziri mwenye mamlaka na ardhi hiyo ya hifadhi
- Mamlaka ya Mkoa au Serikali za Mitaa ambayo inahusika na ardhi hiyo
- Watu ambao wanafanya matumizi ya ardhi hiyo au wataathiriwa na uhamishaji huo.
3. Ikiwa tangazo la kusudio la kuhamisha ardhi ya Jumla basi notisi hiyo inapasa kuwafikia wafutao;
- Mamlaka ya Mkoa au Serikali ya Mtaa ambayo inahusika na ardhi hiyo
- Mtu yeyote mwenye hati mikili ya ardhi inayohusika
- Mtu yeyote mwenye umiliki wa ardhi kwa njia kimila (customary right)
- Mtu yeyote atakayeathiriwa na uhamishaji wa ardhi husika
4. Notisi husika lazima iwe katika lugha rahisi kwa wanaohusika kuweza kuelewa.
5. Wale ambao wataathiriwa na zoezi la uhamishwaji wa ardhi mara baada ya kupata notisi ndani ya siku 20 hadi 40 wanaweza kutoa maelezo yao mbele ya Kamishna wa Ardhi au Ofisa wa Ardhi na maelezo yao yatazingatiwa na ripoti itaandaliwa na kupelekwa kwa Rais kabla ya kufanya uhamisho.
6. Ikiwa zoezi la kuhamisha litaendelea basi wale ambao walikuwa na hati miliki za ardhi (kwenye ardhi ya Jumla) watalipwa fidia.
Hitimisho
Leo tumejifunza tena juu ya ardhi na tumeangalia mgawanyo wa ardhi katika makundi matatu yaani ardhi ya jumla, ardhi ya hifadhi na ardhi ya kijiji. Ni muhimu sana mwananchi kufahamu mgawanyo huu. Je, wewe unakaa na kutumia ardhi ipi kati ya hizi? Je, ardhi unayotumia au unayokaa una uhalali nayo kwa kiasi gani?. Hivi karibuni tumeshuhudia bomoa bomoa ya makazi ya watu na maeneo ya biashara, hii ni kutokana na baadhi ya watu kufanya makazi katika ardhi ambazo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria. Endelea kufuatilia makala za sheria Leo tukijifunza mara kwa mara juu ya sheria za ardhi na mambo mengine.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz
Wako
Isaack Zake, Wakili