Je, Unazijua Ardhi za Hifadhi?
Utangulizi
Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala ya Sheria Leo.34:Makundi ya Ardhi.. Leo tunakuletea ufafanuzi wa kundi la Ardhi ya Hifadhi.
Msingi wa Ardhi ya Hifadhi
Sheria za Ardhi zinatambua uwepo wa Ardhi ya Hifadhi. Kwa haraka unaweza kufikiri ardhi hii inahusika na maeneo ya misitu au mbuga za wanyama tu. Ardhi ya hifadhi ni ardhi iliyotengwa kwa makusudi maalum. Kama tunavyofahamu makundi ya ardhi yapo matatu yaani ardhi ya Jumla, ardhi ya Kijiji na ardhi ya Hifadhi.
Hivi karibuni kumekuwa na zoezi la kuondoa makazi au shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya ardhi ya Hifadhi. Wananchi wamekuwa na malalamiko mengi, kesi nyingi zimefunguliwa na nyumba nyingi zimebomolewa, mashamba yameharibiwa kwa kufikia lengo la kurudisha ardhi ya hifadhi katika makusudi maalum.
Maeneo yanayotambuliwa na Sheria kuwa Ardhi ya Hifadhi
Sheria ya Ardhi Na.4 ya 1999, Kifungu cha 6 kinatamka juu ya aina za maeneo ambayo yatachukuliwa kuwa ni ardhi ya Hifadhi. Maeneo hayo yamegawanyika kama ifuatavyo;
- Maeneo yanayotambulika na Sheria maalum kuhusiana na hifadhi husika
- Maeneo ya Hifadhi ya misitu kwa mujibu wa Sheria ya Misitu
- Mbuga za wanyama kwa Mujibu wa Sheria zinazohusu maeneo hayo
- Maeneo ya hifadhi ya bara bara kwa mujibu wa Sheria za Barabara
- Hifadhi za maji (bahari, mito, mabwawa na maziwa)
- Ardhi ardhi yenye majimaji
- Maeneo ya wazi
2. Maeneo ya vyanzo vya maji.
3. Maeneo ambayo yamewekwa rasmi kwa shughuli za miundombinu ya kijamii kama maji,umeme, simu, gesi n.k
4. Maeneo yaliyotangazwa kuwa ni ardhi hatarishi.
Muhimu
Maeneo haya ambayo ni ya hifadhi kisheria hayaruhusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu mfano wa biashara, ufugaji au makazi. Watu wengi wamekuwa wakivamia na kutumia maeneo mbali mbali ya hifadhi iwe kujenga makazi au kufanya biashara ili hali maeneo hayo yanatambulika kisheria kuwa ni maeneo ya hifadhi.
Kwa msingi huu tumeshuhudia hasara kubwa inawapata watu kila siku ambao shughuli zao zimewekwa katika maeneo ya hifadhi mfano hifadhi ya bara bara wengi wamevunjiwa nyumba zao na biashara zao. Wakati mwengine Serikali ilishatangaza kuwa maeneo hayo ni ya hifadhi na waliostahili kulipwa fidia walishalipwa ila wanawauzia watu wapya nao pasipo kujua wanaweka shughuli zao mahali hapo na matokeo yake ni hasara.
Hitimisho
Leo tumejifunza tena juu ya ardhi ya hifadhi na kuona kwa mifano maeneo ambayo ardhi yake ni hifadhi. Tutoe rai tu kwa wananchi kuzingatia juu ya hatua za kuchukua ikiwa upo eneo fulani ambalo hujajua kama ni eneo la ardhi ya kijiji au eneo la hifadhi au ardhi ya jumla. Muhimu kuwasiliana na Mamlaka husika kama ni ofisi ya ardhi au Halmashauri ya eneo ili kujua matumizi ya eneo husika uepuke matatizo ambayo yanaweza kukupata. Vivyo hivyo kabla ya kununua eneo jiridhishe matumizi au kundi la ardhi husika kama linakidhi makusudi ya uhitaji wako wa eneo.
Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz
Wako
Isaack Zake, Wakili