9: Ujira

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Ijue sheria ya Kazi nashukuru tumeendelea  kuwa pamoja na kupata maarifa haya ambayo yanaletwa kwako kupitia ukurasa huu wa Elimu ya Sheria.  Katika makala iliyopita tuliangalia viwango vya ajira katika eneo la Saa za Kazi za Ziada na mambo mengine yanayohusu saa za kazi. Tuliichambua sheria ya kazi na viwango vya ajira kuhusu saa za kazi za ziada, wiki ya kazi nyingi, kuwastanisha muda na kazi za usiku. Leo tunaendelea kuangalia mambo mengine kwenye Viwango vya Sheria hasa UJIRA. Karibu sana tuendelee na mfululizo wa makala hizi.

Ujira na Namna ya Kukokotoa

Sheria ya Kazi katika viwango vya ajira imezungumzia masuala ya Ujira au Mshahara. Katika sheria hii inatamka bayana kuwa mfanyakazi anastahili kupata mshahara usiopungua kima cha chini cha mishahara kilichopangwa kisheria.

Mshahara au ujira utapangwa kulingana saa za kazi za kawaida kupitia Jedwali la Kwanza kwenye Sheria ya Kazi ambapo imeanisha namna ya kupata hesabu ya ujira kwa saa, siku, wiki au mwezi.

Ili kupata viwango hivyo na kujua kiasi kinacholipwa unaweza kufanya hesabu hizo kama ifuatavyo;

Iwapo mfanyakazi anapokea mshahara kwa mwezi Tsh.300,000/- je anapata vipi mshahara wa wiki, wa siku na wa saa?

  • Mshahara wa mwezi Tsh.300,000/- gawa kwa 4.333 unapata Tsh.69,236.09/- mshahara wa wiki
  • Mshahara wa wiki Tsh.69,236.09/- gawa kwa saa 45 za kazi za kawaida katika wiki unapata Tsh.1,538.57/- mshahara wa siku
  • Mshahara wa siku Tsh.1,538.57/- gawa kwa saa 8 za kazi katika siku unapata Tsh.192.32/-

Iwapo mfanyakazi analipwa mshahara kwa vigezo vingine tofauti na kigeo cha saa za kazi, hivyo itachukuliwa kuwa mfanyakzi huyo analipwa mshahara kwa wiki na kwa utaratibu ufuatao;

  • Jumla ya kiasi alicholipwa katika kipindi cha wiki 13 kabla ya siku ya malipo gawa kwa 13; au
  • Kama amefanya kazi pungufu ya wiki 13, jumla ya kiasi alicholipwa gawa kwa wiki alizofanya kazi kabla ya malipo.

Mfano:

Maria katika kufanya kazi baada ya wiki 13 alilipwa kiashi cha Tsh.1,300,000/-. Hivyo kupata kujua mshahara wake wa wiki utagawa Tsh.1,300,000 kwa 13 ambapo kwa wiki ni Tsh.100,000/-. Iwapo alifanya kazi kwa wiki 10 akalipwa kiasi cha Tsh.130,000/- unagawa Tsh.1,300,000 kwa 10 na kupata kiasi cha Tsh.130,000/- kwa wiki.

 

 Ulipaji wa mshahara

Sheria inaagiza kuwa mshahara ulipwe

  • Wakati wa saa za kazi, mahali pa kazi kwa siku iliyokubaliwa
  • Kwa fedha taslimu isipokuwa kama kuna makubaliano ya kulipwa kwa hundi au kuweka kwenye akaunti ya mfanyakazi
  • Katika bahasha iliyofungwa kama malipo yamefanyika kwa hundi au fedha taslimu

Mwajiri analazimika kutoa maelezo ya kina ya maandishi katika fomu maalum (salary slip)

Makato na Mambo mengine yanayohusiana na Ujira

Mwajiri haruhusiwi kufanya makato yoyote kwenye mshahara wa mfanyakazi isipokuwa katika mazingira yafuatayo;

  • Kwa mujibu wa sheria kama vile kodi, michango ya pensheni n.k
  • Kwa amri ya mahakama au Tuzo ya Mwamuzi
  • Marejesho ya mkopo iwapo mfanyakazi ameelekeza au kuridhia kwa maandishi
  • Ada ya Chama cha Wafanyakazi baada ya kutoa idhini kwa Fomu TUF

Aidha kila mfanyakazi ana jukumu la kutunza mali za mwajiri, na endapo mafanyakazi ataharibu mali za mwajiri kwa uzembe, mwajiri anaweza kumkata mfanyakazi mshahara wake kufidia hasara iliyotokea. Sheria inaongoza hata hivyo kabla ya kuchukua hatua husika mambo ya msingi kuzingatiwa;

  • Mwajiri lazima azingatie utaratibu wa haki
  • Hasara au uharibifu umetokea wakati mfanyakazi akiwa kazini na kwa sababu ya kosa la mfanyakazi
  • Mwajiri anampa mfanyakazi maelezo ya maandishi ya kiasi cha hasara, chanzo cha uharibifu au hasara na hesabu za namna deni hilo lilivyofikiwa
  • Mfanyakazi anapewa nafasi ya kujitetea na kupinga deni hilo, chanzo na namna hesabu za deni hilo zilivyofikiwa
  • Jumla ya deni isizidi kiwango halisi cha hasara au uharibifu
  • Makato yasizidi ¼ ya mshahara wa mfanyakazi

Hitimisho

Ndugu msomaji leo tumechambua sheria ya Kazi katika eneo la Viwango vya Ajira: Ujira, kwa kuangalia maana yake, ukuokotoaji wa mshahara kwa mwezi, wiki, siku na saa, namna mshahara unavyolipwa na makato mbali mbali kwenye mshahara. Muhimu kuzingatia mshahara lazima uambatane na maelezo ya maandishi ‘salary slip’ kwa ajili ya mfanyakazi kuwa na kumbukumbu zake jinsi alivyolipwa na makato yaliyofanyika kwenye mshahara wake.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

2 replies

Comments are closed.