Utetezi wa Dai la Haki kwa Uaminifu

Utangulizi

Karibu sana ndugu msomaji wa makala ambapo umekuwa ukipata maarifa juu ya sheria mbali mbali na dhana kadhaa za kisheria kila siku. Katika makala ya Sheria Leo.22 tulitambulisha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), ambapo tuliweza kuifahamu kwa uchache na juu ya makosa mbali mbali. Leo tunakuletea Utetezi wa Dai la Haki kwa Uaminifu (Bona fide claim of Right)

Msingi wa Utetezi wa Dai la Haki kwa Uaminifu

Sheria ya Kanuni ya Adhabu pamoja na kuainisha makosa mbali mbali imeainisha pia aina za utetezi ambapo mtuhumiwa anaweza kutumia kujitetea pale anaposhitakiwa mahakamani. Mtuhumiwa kwenye makosa ya jinai ana haki ya kuleta hoja za utetezi ambazo zinaweza kumwondolea tuhuma zinazomkabili.

Hoja ya utetezi wa dai la haki kwa Uaminifu ni mojawapo wa sababu za kuweza kumsaidia mtuhumiwa kutotiwa hatiani kwa kosa analoshitakiwa nalo.

Maana ya Utetezi wa Dai la Haki kwa Uaminifu

Kifungu cha 9 cha Kanuni ya Adhabu Sura 16 kinaeleza msingi na maana ya utetezi huu

‘Mtu hawi na jukumu ya jinai kwa ajili ya kosa lihusikalo na mali, iwapo kitendo alichotenda au alichoacha kukitenda kwa ajili ya mali hiyo alitenda ili kutimiza dai la haki kwa uaminifu na bila ya kusudio la kudanganya’

 

Kutokana na kifungu juu ya matumizi ya Utetezi wa Dai la Haki kwa Uaminifu ili utetezi huu uweze kusimama mahakamani ni muhumu mambo haya yathibitike;

  1. Dai ya Haki la Uaminifu lazima lihusike na mali

Ili mtuhumiwa aweze kutumia hoja ya utetezi wa dai la haki kwa uaminifu lazima kosa analotuhumiwa nalo liwe linahusu mali na si vinginevyo. Utetezi huu hauwezi kutumika kwa makosa mengine kama ubakaji au mauaji bali kosa lihusishwe na mali.

Mfano.

ABC ana eneo ambalo analitumia kwa kulima na kupanda mazao baada ya muda anakuja XYZ na kuanza kujenga eneo hilo. ABC anakuja kwenye eneo lake na kukuta vifaa vya ujenzi na kuviondosha eneo hilo. XYZ anaenda mahakamani kudai uharibifu wa vifaa vyake kwenye eneo ABC ana utetezi wa dai la haki juu ya mali hizo.

  1. Dai la Haki lazima liwe kwa uaminifu pasipo nia ya kudanganya

Mtuhumiwa lazima adhibitishe kuwa wakati anachukua hatua juu ya dai lake la haki hakuwa na nia ya kudangaya au kudhulumu upande mwengine kwa namna yoyote.

Mfano.

Andrew ni mfanyakazi wa Paul kwa muda mrefu. Paul anaamua kumwachisha kazi Andrew pasipo kumlipa mishahara yake ya miezi 3. Andrew katika harakati zake za kufuatilia madai yake anakutana na Isaack ambaye anampatia kiasi cha Tsh.300,000/- ampelekee Paul. Kiasi hicho ndio halisi cha mishahara yake ya miezi 3 ambayo anamdai Paul (Mwajiri). Katika mazingira haya Andrew anaweza kutumia utetezi wa dai la haki pasipo nia ya kudanganya.

  1. Mtuhumiwa lazima awe anaamini kuwa ni dai la haki yake kisheria

Mtuhumiwa katika kosa linalohusu mali wakati anatekeleza dai hilo lazima aamini ni haki yake kisheria. Kile mtuhumiwa anachodai si lazima kiwe kimeandikwa kwenye sheria kuwa ni haki yake bali aamini kuwa anastahili kuhusiana na dai hilo.

Mfano.

Oyat anatuhumiwa kwa kukamata ng’ombe 5 ambao waliharibu shamba lake. Mmiliki wa ng’ombe aliambiwa amlipe fidia Oyat kiasi cha Tsh.20 kwa uharibifu wa mazao ya shamba. Oyat akarudisha ng’ombe 4 na kubakisha mmoja ambaye alimuuza na kujilipa Tsh.20 na fedha zilizobaki amrudishie Mlalamikaji kabla ya kutekeleza hilo alikamatwa na kushtakiwa na kuhukumiwa kwa wizi. Oyat alikata  rufaa na mahakama ikamwachia kwa sababu ya kuwa na haki ya kupata fidia kutokana na shamba lake kuharibiwa. (Oyat vs Jamhuri [1967] A.E.827)

Hitimisho

Ndugu msomaji Utetezi wa Dai la Haki kwa Uaminifu ni moja wapo ya hoja za msingi zinazoweza kumsaidia mtuhumiwa kuondokana na hatia au tuhuma zinazomkabili kuhusiana na mali. Ni muhimu kuyafahamu mazingira ambayo yanaweza kukusaidia endapo unakabiliwa na tuhuma au kesi ambayo wewe au mtu unayemfahamu alikuwa na dai la haki kwa uaminifu na tumia hoja hiyo katika utetezi. Hata hivyo endapo unakabiliwa na changamoto za kisheria wasiliana na wataalam wa sheria (Mawakili) ili uweze kupata msaada mahsusi kwa tatizo lako kwani si kila shitaka unaweza kutumia utetezi huo.

Kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi kila siku. Wasiliana nami kwa kutembelea mtandao wako wa  www.ulizasheria.co.tz

Wako,

Isaack Zake, Wakili