10: Likizo

Utangulizi

Ndugu msomaji wa makala za Ijue sheria ya Kazi katika ukurasa wa Elimu ya Sheria nashukuru tumeendelea  kuwa pamoja na kupata maarifa haya. Katika makala iliyopita tuliangalia viwango vya ajira kuhusu Ujira. Leo tunaendelea kuangalia mambo mengine kwenye Viwango vya ajira hasa Likizo. Karibu sana tuendelee na mfululizo wa makala hizi.

Maana ya Likizo

Likizo ni kipindi ambacho mfanyakazi anapata kupumzika kwa muda iwe katika mwaka wa kazi au kipindi fulani kwa makubaliano na mwajiri.

Likizo ni mojawapo ya haki ya mfanyakazi na ni sehemu muhimu ya viwango vya ajira. Hata hivyo sheria inabainisha makundi kadhaa ya wafanyakazi wanaostahili likizo ya malipo.

Makundi ya wafanyakazi wanaostahili kupata likizo ya malipo ni;

  • Waliofanya kazi kwa zaidi ya miezi 6 mfululizo
  • Wafanyakazi wa msimu
  • Wafanyakazi waliofanya kazi kwa kipindi tofauti kwa mwajiri mmoja katika mwaka iwapo vipindi husika vikijumlishwa vitazidi miezi sita

Aidha Sheria ya Kazi inatambua kuwa mfanyakazi ana haki ya kupata likizo zifuatazo;

  • Likizo ya mwaka
  • Likizo ya uzazi kwa akina mama
  • Likizo ya akina baba
  • Likizo ya ugonjwa
  • Likizo ya huruma au majukumu ya kifamilia

 

  1. Likizo ya Mwaka
  • Mfanyakazi anastahili kupewa likizo ya siku 28 mfululizo katika mzunguko wa miezi 12
  • Siku za likizo zinaweza kukatwa endapo mfanyakazi alipewa ruhusa mbalimbali
  • Mwajiri ana haki ya kuamua siku ya kuanza likizo kwa mfanyakazi ndani ya miezi 6 kuanzia siku ambayo mfanyakazi alistahili kuanza likizo
  • Muda wa kuanza likizo baada ya miezi 6 unaweza kuongezwa kwa makubaliano iwapo yapo mahitaji ya uendeshaji na nyongeza ya muda wa kuanza likizo isizidi miezi 12
  • Mfanyakazi hapaswi kufanya kazi wakati wa likizo
  • Hairuhusiwi kumlipa mfanyakazi fedha badala ya likizo (kununua likizo) isipokuwa wakati wa kusitisha ajira tu
  • Likizo ya mwaka haitakiwi kuchukuliwa wakati wa likizo nyingine au wakati wa kipindi cha notisi ya kusitisha ajira.
  • Mwajiri ni lazima amlipe mfanyakazi mshahara wake wakati wa likizo
  • Mwajiri anawajibika kumlipa mfanyakazi malipo mengine yanayoambatana na likizo kwa mujibu wa Tamko au Amri ya kima cha chini cha masharti ya ajira.

 

  1. Likizo ya Uzazi ya Wanawake
  • Mfanyakazi anastahili likizo ya uzazi ya malipo ya siku 84 akijifungua mtoto mmoja au siku 100 endapo atajifungua zaidi ya mtoto mmoja katika mzunguko wa miezi 36.
  • Mfanyakazi anapaswa kutoa notisi ya ujauzito kwa mwajiri miezi 3 kabla ya tarehe ya kutarajia kujifungua, ikiambatana na uthibitisho kutoka kwa Daktari.
  • Mfanyakazi anawaeza kuanza likizo ya uzazi wiki 4 kabla ya tarehe anayotarajia kujifungua au kabla ya hapo kwa uthibitisho wa Daktari
  • Mfanyakazi anaweza kuanza kazi wiki 6 baada ya kujifungua isipokuwa kama Daktari atathibitisha kuwa anaweza kuanza kazi kabla ya muda huo
  • Mwajiri anakatazwa kumtaka au kumruhusu mfanyakazi mjamzito au anayenyonyesha kufanya kazi zenye madhara kwa afya ya mfanyakazi au mtoto wake
  • Ikiwa kazi za kawaida za mfanyakazi zina madhara kwa afya yake au mtoto wake, mwajiri ni lazima amtafutie kazi nyingine kwa masharti yale yale ya ajira yake
  • Mfanyakazi anastahili kupewa saa 2 kila siku kwa ajili ya kunyonyesha
  • Mwajiri anawajibika kutoa likizo ya malipo ya uzazi kwa vipindi 4 tu likizo 1 kwa kila mzunguko wa miezi 36.
  • Endapo mtoto aliyezaliwa atafariki ndani ya mwaka 1 tangu kuzaliwa, na mfanyakazi akapata mtoto mwengine ndani ya mzunguko huo huo wa likizo, mfanyakazi atastahili kupata likizo nyingine ya malipo ya siku 84
  • Ni kinyume cha sheria kumwachisha kazi mfanyakazi kwa sababu ya ujauzito au majukumu ya kifamilia
  • Mfanyakazi aliyemaliza likizo ya uzazi ataendelea na ajira yake kwa masharti yale yele ya ajira.

 

  1. Likizo ya Uzazi kwa Wanaume
  • Mfanyakazi mwanamume aliyepata mtoto anastahili angalau siku 3 za likizo katika mzunguko wa miezi 36 bila kujali idadi ya matukio
  • Mfanyakazi atapoteza haki hiyo ya likizo endapo atashindwa kuchukua likizo hiyo ndani ya siku 7 baada ya mtoto kuzaliwa
  • Mfanyakazi analo jukumu lakudhibitisha kuwa mtoto aliyezaliwa ni wake.

 

  1. Likizo ya Ugonjwa
  • Mfanyakazi anastahili likizo ya ugonjwa ya angalau siku 126 katika mzunguko wa miezi 36
  • Katika siku 63 za kwanza mfanyakazi anastahili kulipwa mshahara kamili na katika siku 63 zinazofuata anastahili kulipwa nusu mshahara
  • Kabla ya kuchukua likizo ya ugonjwa mfanyakazi anapaswa kuwasilisha kwa Mwajiri udhibitisho wa Daktari
  • Endapo mfanyakazi anastahili kulipwa wakati wa likizo ya ugonjwa kwa mujibu wa sheria, mfuko wowote au makubaliano ya pamoja, mwajiri atakuwa hana jukumu la kumlipa mfanyakazi huyo wakati wa likizo.

 

  1. Likizo ya Huruma au Majukumu ya Kifamilia

Mfanyakazi anastahili angalau siku 4 za likizo ya malipo katika mzunguko wamiezi 36 bila kujali idadi ya matukio kwa sababu zifuatazo;

  • Kuugua au kifo cha mtoto
  • Kifo cha mume/mke, mzazi, babu, bibi, mjukuu au ndugu wa kuzaliwa

Mfanyakazi anaweza kupewa siku zaidi ya 4 na mwajiri kwa tukio moja au matukio mengine katika mzunguko wa likizo, siku ambazo zinaweza kupunguzwa katika likizo ya mwaka au kutolipwa mshahara wa siku hizo.

Hata hivyo ni muhimu kutambua siku za likizo zinaweza kuongezwa kupitia makubaliano ya pamoja au kanuni za mwajiri.

Hitimisho

Ndugu msomaji leo tumechambua sheria ya Kazi katika eneo la Viwango vya Ajira: Likizo, kwa kuangalia maana yake, vigezo vya mfanyakazi kupata likizo na aina za likizo ambazo mfanyakazi anastahili kuzipata. Ni vyema mwajiri na mfanyakazi kutambua haki zao na wajibu wao katika masuala ya likizo, na kwamba kwa namna yoyote likizo haiwezi kununuliwa hivyo mfanyakazi hakikisha unaenda likizo yako na kupata haki yako ya malipo.

Usisite kunitumia maswali yako yoyote kuhusu sheria katika mtandao wako  kumbuka ‘kutokujua sheria si utetezi iwapo utatenda kosa lolote’ tafuta maarifa sahihi ya kisheria yakusaidie kufanya maamuzi sahihi. Wasiliana nami kupitia www.ulizasheria.co.tz

wako

Isaack Zake, Wakili

9 replies
  1. isack Matonange
    isack Matonange says:

    mimi ni mfanyakazi ambaye nafanyakazi kwa siku 7 mchana kwa masaa 12 na usiku siku 7 nikimaliza mzunguko huo nina kwenda of siku 7 sasa likizo natakiwa kuiaza wakati gani je ofu au natakiwa niziuganishe na of

Comments are closed.